Wanawake tisa wa Kijiji cha Mabwegere, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wamelishutumu Jeshi la Polisi wilayani humo kwa kuharibu ushahidi, baada ya kubakwa na kikundi cha vijana wa ‘mwano’ kilichovamia eneo hilo na kuteketeza nyumba kwa moto.
Wanawake hao pamoja na uongozi wa kijiji wamelithibitishia gazeti la JAMHURI kuwa Januari 18, mwaka huu, wakulima kutoka vijiji jirani wakiongozwa na kundi hilo, walivamia Mabwegere na kuteketeza kwa moto nyumba 38, kupora mifugo na kuwabaka wanawake hao wapatao tisa kwa zamu.
Kwa mujibu wa mwathirika wa tukio hilo la kubakwa, wavamizi hao walipofika katika kijiji hicho walikamata na kuanza kuwabaka kabla kuteketeza nyumba zao kwa moto na kuharibu vyakula vilivyovihifadhiwa.


Mwathirika huyo (jina tunalihifadhi kwa sababu maalum), anasema walipomaliza kufanya ukatili huo walipora mifugo ikiwamo ng’ombe na mbuzi na mingine kufyekwa kwa mapanga na wavamizi hao.
“Tulikwenda Polisi na kupatiwa fomu za PF 3 na kisha hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya vipimo, ushahidi kwamba tulibakwa uliandikwa katika fomu hizo ambazo tulitoa nakala na kupeleka nakala halisi Jeshi la Polisi na watuhumiwa walikamatwa na kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Wilaya,” anasema.


Anasema kesi dhidi ya watuhumiwa hao ilipofunguliwa, Jeshi la Polisi halikuwashirikisha chochote kilichokuwa kikiendelea kuhusu kesi hiyo kama mashahidi na waathirika wa tukio hilo, badala yake walifika kijijini hapo na kuomba wapatiwe nakala vivuli za PF 3 walizokuwa nazo kwa madai kuwa wanaendelea na uchunguzi, huku wakijua kwamba nakala halisi walikuwa nazo.
“Tuliwapatia nakala hizi kwa vile walidai kwamba wanataka kuendelea na uchunguzi na hakuna kilichoendelea baada ya hapo zaidi ya kupewa taarifa za kufutwa kwa shauri mahakamani hapo Aprili 16 mwaka huu, na watuhumiwa watano waliokuwa wanashikiliwa waliachiwa huru,” anasema mwanamke huyo kwa uchungu.


Hata hivyo, anaongeza kuwa kilichowashangaza ni polisi kwenda kuwalaghai na kutwaa vielelezo walivyokuwa navyo, vikithitisha kwa taarifa za kitabibu kwamba walibakwa na kuondolewa kwa shauri hilo bila ya wao kuelewa chochote kilichokuwa kikiendelea.
“Nchi haina haki, tunanyanyaswa sana hapa kijijini kama hatuko ndani ya Tanzania, na taasisi zinazohusika zimeshindwa kabisa kutenda haki kwa sababu za rushwa,” anaeleza mwanamke huyo huku akibubujikwa na machozi.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Leonard Paul, alipotafuwa na JAMHURI hakuweza kuzungumza chochote kwa maelezo kwamba yuko kwenye msiba. Hata hivyo, alipotafutwa tena kwa mara nyingine simu yake haikuweza kupatikana.
  Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mika Kashu, alieleza kusikitishwa na kitendo hicho walichofanyiwa wanawake hao na kwamba hakiwezi kukubalika kabisa.


Kashu anasema jambo hilo liko wazi lakini kuachiwa kwa watuhumiwa hao waliohusika na ukatili huo, kumewanyima haki wanawake hao na familia zao ambao kwa sasa wanaishi kwa hofu ndani kijiji hicho kwamba wanaweza kutendewa tena ukatili mwingine.
“Hapo tunaishi kwa hofu sana kama hatuko ndani ya nchi yetu, wakati migogoro hii haikuwa na sababu yoyote ya kuendelea kama Serikali ingekuwa makini kuheshimu mhimili wa Mahakama,” anasema.


  Anasema vikundi vinavyoendesha uhalifu wa kupora mifugo, kubaka na kuteketeza nyumba za wakazi wa kijiji hicho, vinahatarisha amani ya nchi na vinapaswa kudhibitiwa mara moja.
 Naye Shehe Lamanya, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ndagani, anasema kutoweka kwa amani kwa wakazi wa vijiji hivyo ni matokeo ya kukithiri kwa rushwa na ubinafsi unaoshika kasi miongoni mwa jamii.
Lamanya anasema kitendo cha kuvamia wakulima wanaoishi kihalali ndani ya kijiji chao na kuendesha vitendo vya kikatili, ni kinyume cha kuheshimu haki za binadamu, kwani kila mtu ana haki ya kuishi.

 
1985 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!