Na.Abel Paul,Jeshi la Polisi- Longido Arusha

Jeshi la Polisi kikiosi cha kupambana na kuzuia wizi wa mifugo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne pamoja na mifugo aina ya Punda Arobaini na sita wakisafirishwa kinyume na taratibu Kwenda nje ya nchi.

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi kikosi cha kuzuia wizi wa Mifugo nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi pamoja Wizara ya Mifugo na Uvuvi linawashirikilia watuhumiwa wanne wakisafirisha mifugo aina Punda ipatayo arobaini na sita kwenda nje ya nchi kinyume na taratibu.

SACP Pasua amesema kuwa watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku akibainisha kuwa majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi ambapo amesema kuwa pindi upelelezi utakapo kamilika watuhumiwa wote watafikishwa katika vyombo vya sheria kujibu tuhuma zao.

Kamanda Pasua ameongeza kuwa tayari serikali kupitia wizara ya Mifugo na Uvuvi ilishatoa maelekezo juu ya katazo la kusafirisha Punda na mazao yake kutokana na kupungua kwa idadi ya Punda huku akiweka wazi kuwa Jeshi hilo litaendelea kuwakamata wale wote watakao bainika kuhusika na usafirishaji wa Punda Kwenda Nje ya nchi.

Aidha amebainisha kuwa Jeshi hilo litaendelea kutoa elimu kwa Wananchi na kuwakamata wale wote watakao kaidi agizo la serikali la kuto kusafirisha Punda na Mazao yake Kwenda nje ya nchi kutokana na kupungua kwa idadi ya Mifugo hiyo aina ya Punda.

By Jamhuri