Na Kija Elias , JamhuriMedia, Mwanga
Wananchi wa Kijiji cha Kirya, Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wameiomba serikali kuwasaidia dawa za kuua popo waliovamia majengo ya Kituo cha Afya Kirya na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya ndani, hususan katika dari (ceiling boards).
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Saitoti Timoth, alitoa ombi hilo jana wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa Mwanga Marathon and Festival, Frida Mberesero, aliyefika kituoni hapo kwa ajili ya kufanya shughuli za usafi na upandaji miti kuzunguka majengo ya kituo.
Timoth alisema popo wamekuwa tatizo kubwa katika kituo hicho na wameharibu sana dari za majengo, huku gypsum zilizowekwa zikiwa zimeanza kuoza kutokana na kinyesi cha popo.

“Gypsum zilizowekwa kwenye dari zimeanza kuoza kabisa kutokana na kinyesi cha popo, hususani katika Jengo la mama na mtoto limeharibika kabisa na linaanza kutoboka, tunaomba serikali itupe msaada wa haraka wa dawa za kuua popo ili kuwaondoa kabisa,” alisema.
Naye Mjumbe wa Serikali ya Kijiji hicho, Elikana Razaro, alieleza kuwa uvamizi wa popo ni changamoto kubwa hal;i ambayo inahatarisha huduma za afya kwa wananchi, hasa akina mama na watoto, na kwamba hawana dawa wala mbimnu ya kuwaondoa popo hao.
“Popo wamejaa ndani ya majengo ya kituo, hatuna dawa ya kuwaondoa na kinyesi chao kimejaa kwenye vyumba vya kutolea huduma, tunahitaji msaada wa haraka,” alisisitiza.
Katika hatua ya kuonyesha mshikamano huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafi na Utunzaji wa Mazingira ya Al Bayanu ECO Services Limited, Abdalla Lusingu Mashombo, alitangaza kuwa kampuni hiyo itajitolea kunyunyizia dawa katika majengo yote ya Kituo cha Afya Kirya ili kuondoa popo waliovamia katuika majengo hayo.
“Tumesikitishwa sana na hali tuliyoikuta katika kituo hiki, Serikali imetumia zaidi ya Sh milioni 500 kujenga kituo hiki, lakini popo wamejaa na kuharibu ceiling board zote, Sisi, kama kampuni, tumeamua kujitolea kunyunyizia dawa katika maeneo yote ya dari ili kuwaondoa kabisa popo hawa,” alisema Mashombo.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Kiwamwaku Foundation, Ezekiel Dembele, alisema changamoto ya uvamizi wa popo inahitaji hatua za haraka, ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi bora wa mazingira.
“Uwekezaji wa serikali katika kituo hiki ni mkubwa, tunapongeza kwa jitihada hizo, lakini sasa tunahitaji kushirikiana kuondoa popo na pia kuimarisha mazingira kwa kupanda miti,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mwanga Marathon and Festival, Frida Mberesero, alieleza kusikitishwa na hali ya mazingira ya kituo hicho, akisema licha ya uwekezaji mkubwa wa serikali, bado maeneo ya kituo hayaonyeshi hadhi inayolingana na thamani hiyo.
“Uhamasishaji wa usafi na utunzaji wa mazingira umekuwa mdogo, Serikali ya kijiji inapaswa kuhakikisha maeneo yanayozunguka kituo yanatunzwa vizuri,” alisema Frida.
Aliongeza kuwa ipo haja ya kuwa na mbinu mbadala za upandaji miti kuzunguka kituo hicho kwa kushirikiana na taasisi kama Kiwamwaku, TFS, na Al Bayanu, ikiwa ni pamoja na kutafuta udongo, mbolea, na kuchimba mashimo kwa ajili ya miti, pamoja na kuhakikisha inamwagiliwa maji kwa wakati.
“Hospitali ni mazingira, majengo haya yameanza kuchoka, Serikali imetuwekea miundombinu, jukumu letu ni kuitunza ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu,” alisema.