Watu wawili wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka matatu ya kula njama na kuvamia, kuvunja makazi na kuiba fedha na vitu vyenye thamani ya Sh bilioni 1.4.

John Masatu (45) na Phinias Mang’ara (47) wamefikishwa mahakamani hapo kwa kuiba kinyume cha kifungu cha 258 na 265 vya Sheria ya Kanuni ya Adbabu Sura ya 16.

Imeelezwa kuwa Febuari 22, 2018 walitenda kosa la kuiba dola 220,000 sawa na Sh milioni 506, fedha za Tanzania taslimu Sh 50,000,000, vitu mbalimbali vyenye thamani ya dola 400,000 sawa na Sh 920,000,000 na sanduku la kuhifadhia vitu. Mali zote zilizoibwa zina thamani ya Sh bilioni 1.4.

Wakili wa Serikali, Silvia Mitanto, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, aliiambia mahakama kuwa Masatu, maarufu kama Paya mkazi wa Tabata Segerea na Mang’ara, maarufu kama Phina mkazi wa Kimara King’ong’o wanatuhumiwa kutenda makosa katika tarehe tofauti Februari mwaka uliopita.

“Katika shitaka la kwanza, tarehe 15, Februari na 22, Februari mwaka jana mshitakiwa namba moja, John Masatu Musita pamoja na mshitakiwa namba mbili, Phinias Mang’ara, walikula njama za kutenda kosa kinyume cha sheria,” amedai Wakili Mitanto.

Wakili huyo wa serikali amesema katika shitaka la pili chini ya kifungu cha 294 cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Musita na Mang’ara, Februari 22, 2018 walivunja nyumba ya Taoto anayefahamika kama David iliyopo Twins Tower Apartment, Wilaya ya Kinondoni na kuiba.

Washitakiwa wote wamekana mashitaka hayo na walitakiwa kudhaminiwa kila mmoja kwa fedha taslimu Sh milioni 200 au vitu visivyohamishika vyenye thamani ya Sh milioni 200.

Hata hivyo mshitakiwa namba mbili, Mang’ara, amerudishwa rumande baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ambapo Masatu amepata dhamana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 11, 2019 itakapotajwa tena mahakamani hapo.

By Jamhuri