Sakata la kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond iliyopewa zabuni na serikali kwa njia za ubabaishaji limeendelea kushika kasi huku likiibuliwa kwa sura tofauti likitumiwa na CCM kuomba kura kwa wananchi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Makada wa CCM, pengine kwa udhaifu wa kisiasa wameliibua tena suala hilo ambalo lililotokea zaidi ya miaka nane iliyopita, katika mikutano yao kampeni za urais za mgombea wao Dk. John Magufuli anayedai hana kashfa za ufisadi serikalini.

Kwa hoja hiyo inaonekana ufisadi ni ule wa Richmond tu. Kugawana nyumba za serikali, kazi aliyoisimamia mwenyewe wakati wa serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa kwake sio ufisadi, ununuzi wa boti chakavu ya serikali kwa mabilioni ya shilingi na mashine za kukatia tiketi kivukoni, hapa hakuna tuhuma za ufisadi.

Tuachilie mbali ukweli huo na sasa tujikite kuangalia mwisho wa filamu ya Richmond ambayo mkuu wa nchi ameingia kuicheza huku akituhumiwa kuhusika nayo. Wapumbavu na malofa wameipenda kweli hii.

Waigizaji wa picha hiyo ya ufisadi walianza kwa kutojiamini akiwemo aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe ambaye hajawataja waliokwapua mabilioni katika ununuzi wa mabahewa feki ya TRL na waliotuhujumu kupitia bandari zetu. Kwa mazingira haya huyu naye hana ujasiri.

Ametuficha kuhusu ukweli wa mhusika mkuu wa Richmond muda wote na sasa anatafuta kutuhadaa.

Kwa kukosa kujiamini wameamua “kumkodi” Dk. Willibrod Slaa amwage tuhuma za Richmond dhidi ya mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa, ambaye naye alishindwa kueleza ukweli, amezamia ughaibuni kuponda starehe kwa ujira wa ufisadi ule ule. Ameamua kuishi “chooni”.

Rais Jakaya Kikwete amesema anashangazwa na Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu aliyetaka amtaje mhusika wa Richmond wakati mwenye Richmond yupo na anatembea naye mikoani kwenye kampeni.

Rais Kikwete aliyasema hayo wiki iliyopita wakati akiwaaga wananchi wa Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika na kumtaka Lissu amtaje mwenye Richmond.

“Endapo Tundu Lissu atashindwa kumtaja mwenye Richmond, nitatoka hadharani na kumtaja mwenyewe,” anasema Rais Kikwete.

Rais Jakaya Kikwete aligeuza kibao kwa kumtaka Tundu Lissu amtaje mhusika wa Richmond anayezunguka naye kwenye kampeni, lakini Mbunge huyo wa Singida Mashariki ameibuka na kudai kuwa Rais huyo ndiye mhusika wa kampuni hiyo. 

Akihutubia mkutano wa kumnadi Lowassa, mwanasheria huyo amesema mkuu huyo wa nchi ndiye mhusika wa Richmond kutokana na mamlaka yake na si Lowassa anayedai natembea naye kwenye kampeni.

Siasa za namna hii unaweza kuzieneza ndani ya nchi ya “wapumbavu na malofa” tu wanaoshindwa kupambanua mambo tena wakiwemo wasomi wa ngazi kubwa za maprofesa na madaktari.

Kuendelea kusikiliza filamu ya Richmond iliyogeuzwa mtaji wa kisiasa kwa waliofilisika hoja na ushawishi kwa wapiga kura huo nao ni upumbavu na ulofa.

Filamu ya Richmond hata akirudishwa yule mzinzi kuicheza kabla ya wiki tatu au mbili za uchaguzi mkuu bado haina radha wala mvuto wowote zaidi ya kushangazwa mkuu wa nchi kuhusishwa na umiliki wa kampuni hiyo ya kitapeli.

Wapumbavu na malofa wameniagiza wanaomba waletewe filamu za EPA, Meremeta, Kogoda, Tegeta Escrow iliyochezwa hivi karibuni na wasanii maarufu akina joka la makengeza, vipesa vya mboga, waliopitishia fedha benki ya Stanbic na wakwapuaji wengine.

Nawashauri filamu hizi zichezwe mapema ili chama chetu kiongeze kura za mabadiliko badala ya kung’ang’ania filamu chafu inayoogopwa na wahusika wakuu miaka saba iliyopita.

Hatujachelewa kuwachezea wapumbavu na malofa filamu hizi na nyingine nyingi zinazoendelea ndani ya shamba hili la wote.

Pamoja na kuandaa filamu hizi kazi ile ya ibilisi inayotumiwa sana na chama chetu (divide and rule) au “gawanya na tawala” kama tulivyoindeleza tangu tuingie tena kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 nayo iendelezwe.

Kanuni hii imeendelea kutumika kwa kujaribu kuusambaratisha Ukawa kupitia kwa aliyekuwa mwenyekiti wa CUF, aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema na sasa kumfitinisha mwenyekiti wa NCCR mageuzi na viongozi wenzanke.kanuni hii pia imetumika kuimarisha pengo kati ya wapumbavu na waelevu, malofa walio wengi na matajiri wachache waliojimilikisha keki ya taifa.

1690 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!