Mkutano wa 20 wa Kawaida wa Waratibu wa Kitaifa wa Nchi za Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) umefanyika tarehe 10 Novemba, 2025 jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC.
Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali (SUMMIT) wa Jumuiya hiyo iliyopangwa kufanyika Novemba 13 na 15, 2025 mtawalia.

Mkutano huo umefunguliwa na Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa DRC, Mhe. Floribert Anzuluni Isiloketshi ambapo pamoja na masuala mengine, amewasihi waratibu hao kutumia mkutano huo kuja na mapendekezo yatakayoboresha utendaji kazi wa Sekretarieti ya Maziwa Makuu ili iweze kutekeleza kwa ufanisi zaidi majukumu yake ya msingi, ikiwemo kuleta amani, usalama na maendeleo katika nchi 12 Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Tanzania ikiwa moja ya nchi waasisi wa ICGL, inashiriki mkutano huo kikamilifu ambapo Mratibu wa Kitaifa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.

Naye, Katibu Mtendaji wa ICGL, Balozi João Samuel CAHOLO amesema, licha ya mafanikio ambayo Sekretarieti hiyo imepata chini ya uongozi wake, bado jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha amani ya kudumu na usalama vinapatikana katika Ukanda huo hususan katika nchi za DRC, Jamhuri ya Sudan, Jamhuri ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Amehusisha umasikini, ukosefu wa usawa na wananchi kutozifikia rasilimali za nchi zao kuwa ni baadhi ya vyanzo vya migogoro barani Afrika, na kutoa wito wa kukomesha migogoro kwa kuvishugulikia vyanzo vyake.







