RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuwasisitiza Watanzania waendelee kuliombea Taifa ili amani, upendo, ustahimilivu na mshikamano viendelee kudumu nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba leo (Jumapili, Novemba 16, 2025) alipowasilisha salamu za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa waumini na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kisasa, Mkoa wa Dodoma.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawasalimu sana. Yuko pamoja nanyi, na rai yake kwa Watanzania wote ni kuendeleza maombi kwa Taifa letu kuwa watulivu na kuiombea amani iendelee kudumu.”

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha amani ya nchi inaendelea kulindwa na kuenziwa, kwa sababu pasipo amani, Taifa halitoweza kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendesha ibada na shughuli nyingine za kijamii.

“Pasipo amani hatuwezi kutekeleza majukumu mengine yoyote, pasipo amani hatuwezi kuendesha ibada. Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuiombea nchi yetu. Pakiwa na amani tunaweza kutekeleza yale yaliyo katika matarajio yetu, tunaweza hata kutatua yale tunayoyaona kuwa ni magumu.”

Ibada hiyo imeongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma, Dkt. Christian Ndossa ambaye ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania waishi kwa kumtanguliza Mungu mbele na wawe na matumaini kwake na wajiepushe na maovu.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameambatana na Mwenza wake, Mama Neema Mwigulu Nchemba, katika ibada hiyo.

Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, Mbunge wa Kilolo, Ritha Kabati, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, Mbunge wa Viti Maalumu, Balozi Dkt. Pindi Chana, Mbunge wa Itigi, Yohana Msita na Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga.