Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita zilijitokeza picha mbili za mjongeo katika mtandao. Picha hizi, mtu mmoja amejitambulisha kama Kapteni Tesha, mwingine analalamika, ila zaidi ya kuonekana ameshika bunduki na amevaa sare za jeshi, hajitambulishi. Wote hawa wanazungumza lugha ya Humphrey Polepole. Wanataka kuwaaminisha Watanzania kuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa hawastahili kuchaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba.

Wakati Polepole ametaja majina ya watu mbalimbali, ambayo ameyarudia huyo anayejitambulisha kama Kapteni Tesha, taswira wanayotaka kujenga ni kuonyesha kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia maisha yamekuwa magumu na Tanzania imeachwa nyuma kimaendeleo na majirani zetu. Binafsi nimejiuliza maswali mengi sikupata majibu. Nimemuuliza mtu mmoja makini, kwamba haya yanayosemwa na Tesha na Polepole yeye anayaonaje? Naomba niweke neno kwa neno alichonijibu.

“Hawa wamejipanga. Walianza kwa lengo la kuchafua mchakato wa kuteuliwa kwa Rais Samia na Balozi Nchimbi ndani ya CCM. Walifikiri watafanikiwa kupindua matokeo waingize watu wao, wakakwama. Wakaona basi ngoja waingilie mchakato wa ubunge na udiwani wapenyeze watu wao, na wakaenda mbali watumishi waandamizi wa serikali na mabalozi wakaacha kazi wajipenyeze kwenye ubunge wamekatwa.

“Baada ya kukatwa kwao, wakavuka kambi. Wakawa wanawasaidia baadhi ya wapinzani kwa kuwapa matumaini hewa kuwa uchaguzi hautafanyika, mara wakaona vyama vimefanya uteuzi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeteua wagombea… wakaona watoe kauli za kijinai wakidhani wakikamatwa ‘kitanuka’, wakaona nayo haifanyi kazi ‘kimemnukia aliyekianzisha’.

“Wamejitahidi kuandaa maandamano Oktoba 29, 2025, lakini wameishabaini kuwa maandamano haya hayatatokea. Walianza kitambo, sema Watanzania hawakushituka mapema. Unakumbuka lile sakata la DP World… hiyo ilikuwa sehemu ya maandalizi. Walidanganya Watanzania kuwa Bandari ya Dar es Salaam imechukuliwa yote, leo kila mtu anafahamu kuwa ilikodishwa gati Na. 4, 5, 6 na 7. Hawajawaomba radhi Watanzania kwa kuwambia uongo kuwa bandari imechukuliwa yote.

“Leo aibu inawashuka, kwani Bandari ya Dar es Salaam wakati wanaingia DP World ilikuwa inakusanya Sh bilioni 800, kwa sasa inakusanya Sh trilioni 1.7. Haya hawayasemi. Kamishna Mwenda wa TRA alipoteuliwa TRA ilikuwa inakusanya chini ya Sh trilioni 2. Mwezi Septemba, mwaka huu imekusanya Sh trilioni 3.47. Wanajiuliza Rais Samia anawezaje haya yote? Hawafurahi.

“Tunakuwa wepesi wa kupoteza kumbukumbu. Kabla ya Rais Samia kuingia madarakani Machi 19, 2021, kila saa 7 mchana ilikuwa watu wanapandishwa mahakamani sehemu mbalimbali nchini kwa kesi za utungwa cha uhujumu uchumi. Kwa sasa hili halipo tena. Kariakoo ‘vyuma vilikaza’ hadi maduka mengi yakafungwa. Ilifika mahala Kariakoo unakuta nje ya jengo kumeandikwa nyumba inapangishwa. Kariakoo tangazo la nyumba imepangishwa, maduka yamefungwa…

“Watanzania hawakuwa na uhakika wa kuishi. Leo tunajisahaulisha ukweli, ila huyo Polepole atwambie ‘Watu Wasiojulikana’ na Noah nyeusi zilivyokuwa zinapoteza watu Rais Samia mbona amemaliza tatizo hili? Ilifika mahala kila mtu akitoka nyumbani hana uhakika wa kurejea. Leo Rais Samia kazuia yote hayo. Baadhi hawapendi. Wanataka kuturejesha huko katika hofu. Katika mkondo ambao ukizungumza lugha ya (imehifadhiwa) unapata kazi.

“Rais Samia amejenga madarasa mengi hadi shule nyingi zina madarasa ya ziada na anaendelea kujenga kwa sababu miaka miwili ijayo elimu ya msingi itakuwa inaishia sekondari. Shule zinapendeza hadi watu wanakwenda kupigia picha. Amejenga vituo vya afya usipime. Leo Dar es Salaam inatimka vyumbi. Kuna ujenzi wa barabara kila kona utadhani nchi inatoka vitani.

“Unawasikia wanaotaka kupotosha. Leo wapo wenye ujasiri wa kifisadi wasiotaka kukiri kuwa Reli ya Umeme ambayo ni ndefu kuliko zote Afrika ipo Tanzania na ameijenga Rais Samia. Wanakereka wakisikia anasema atajenga reli ya umeme kutoka Tanga – Kilimanjaro – Arusha hadi Musoma, wanaugua. Wanasikitika wakisikia anapanga kujenga reli yenye urefu wa kilomita 1,000 Mtwara.

“Wanasikitika wakisikia amekamilisha unjenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyererere linalozalisha umeme mwingi, yaani megawati 2,115 kwa wakti mmoja na sasa Tanzania inaongoza katika Afrika Mashariki kwa kuwa na umeme mwingi. Balile nilikusikia pale ITV ulipokuwa unatoa takwimu za umeme kwa nchi zetu niliipenda sana. Kwamba Burundi wanazalisha megawati 166, Rwanda megawati 406, Uganda megawati 2,490, Kenya megawati 2,651, DRC megawati 2,980 na Tanzania megawati 4,031. Wote hawa hakuna mwenye SGR ya Umeme.

“Kwamba Rais Samia ameulinda na kuuimarisha Muungano, kwao ni kero. Haya ni makundi ya uonevu. Wanaamini katika kuonea watu. Ndiyo maana hawana aibu kudiriku kulishawishi jeshi kuingia kwenye siasa na wanatamani kuona Tanzania inaingia kwenye mapigano waonee watu. Hawa wanajifanya hawafahamu yanayotokea Sudani, Libya au Afghanistani… Watanzania wasiwasikilize.

“Oktoba 29, 2025 watu wajitokeze kwa wingi wakapige kura. Tuwapuuze hawa wakaazi wa mitandao wanaofiwa na baba zao, wakasusa kuja hata kuzika wazazi wao. Tunayafahamu mashirika yanayowapa fedha kwa nia ya kuzalisha machafuko nchini. Mashirika hayo yanamiliki viwanda vya silaha. Wanasubiri nchi zetu tupigane wauze silaha. Tusikubali kutumika.”

Sitanii, baada ya maneno hayo, niwashukuru tu Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao baada ya kauli za Tesha wametoa kauli ya kuonyesha ukomavu na kwamba wao wapo kazini hawataki malumbano na mtu kwa kusema: “JWTZ linaendelea kutekeleza majukumu yake kikatiba kwa uaminifu, utii na uhodari kwa kuzingatia kiapo chetu.” Watanzania tusikubali machafuko. Tuwapuuze. Tushiriki uchaguzi Oktoba hii. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827