Na Mwandishi Wetu
Polisi mkoani Njombe inawashikilia watu watu akiwemo James Elias Nziku (41), Ahmed Abdalah Gunda (21) na Seleman Lameck Msiani (37) wakazi wa Makambako mkoani Njombe baada ya kukutwa katika ghala la mfanyabiashara wa pemebejeo anaejulikana kwa jina la Ayoub Sanga wakichakachua mbolea za kampuni ya INTRACOM kwenda kwenye mifuko ya mbolea za DAP zinazosambazwa na kampuni ya mbolea ya taifa TFC ili kuwauzia wakulima na kujitengenea faida zaidi.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kushikiliwa kwa watu watatu waliokuwa wakifanya kazi ya kuchakachua mbolea katika ghala la mfanyabiashara wa pembejeo Makambako Ayoub Sanga , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amesema watu watatu wamekamatwa wakiwa na mifuko 188 ya mbolea iliyochakachuliwa ,mashine ya kufungia mifuko na mifuko mitupu ya makampuni tofauti,hivyo wanaendelea na msako ili wahusika wote wafikishe katika vyombo vya sheria.
Betrice Tarimo ambae ni Afisa Kilimo Halmashauri ya Mji wa Makambako na Samwel Msongwe msimamizi wa kampuni ya TFC kanda ya kusini ni miongoni mwa maofisa wa serikali ambao wamefika eneo la tukio na hapa wanaeleza walichokiona gharani na hatua za haraka zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.
Kutokea kwa tukio hilo kunamuibua Mwenyekiti wa Mawakala wa Pembejeo za Kilimo Halmashauri ya Mji Makmbako Oraph Mhema na wakazi wa Makambako akiwemo Rashid Maltin ambae ni mwenyekiti wa mtaa wa Lumumba Makambako ambao wanasema hatua kali zinapaswa kuchukuliwa ili kuokoa sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa taifa letu.
Kwa upande wake Claudia Kimako mkurugenzi wa maendeleo ya biashara na masoko kampuni ya mbolea ya ITRACOM amezungumzia tukio hili, kwamba mfanyabiashara huyo ni wakala wa mbolea mbalimbali zikiwemo za FOMI lakini alichokifanya kinapingwa vikali hivyo tayari hatua za kisheria zimechukuliwa .
“Kitendo hiki tumekisikia kama wazalishaji wa mbolea hizo tumepinga vikali kitendo hicho ambacho ni kinyume na taratibu na makubaliano yetu. Hatua za kisheria zimeshachukuliwa na zitaendelea kuchukuliwa kwa mawakala wengine wote wenye tabia hizi “ amesema Kimako.
Kimako amesema mfanyabiashara huyo alitaka kujiongezea faida kwa sababu bei ya mbolea zao ni nafuu ukizilinganisha na DAP hivyo tuwatoe hofu wakulima na ma wakala kwamba mbolea zetu hazina changamoto yoyote. “Tumesitisha ushirikiano na wakala huyo na hatutasita kufanya hivo kwa yeyote yule ambaye atakiuka makubaliano yetu ya kibiashara” amesema.




