Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imeamua kutoa changamoto kwa watoa huduma za mawasiliano kwa kuanzisha tuzo ambazo zitaibua watoa huduma bora. 

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba (katikati), akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tuzo za watoa huduma za mawasiliano nchini zilizoandaliwa na mamlaka hiyo.

Akizungumza na wahariri wa habari wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, amesema tuzo hizo zinatarajiwa kuwa chachu itakayosaidia kuboresha huduma za mawasiliano zinazotolewa nchini.

“Ingawa huu ni mwaka wa kwanza lakini tunaamini jinsi tunavyoendelea mbele, watoa huduma watakuwa na hamu ya kushinda. Hilo litawafanya waongeze ubora wa huduma zao na kubuni huduma nyingine bora kama njia ya kuvutia wateja,” anasema Mhandisi Kilaba.

Mhandisi Kilaba anasema kuwa tuzo hizo zitawahusu watoa huduma ambao wamepatiwa leseni na TCRA.

“Ushiriki wenu wahariri na waandishi waandamizi ni wa muhimu sana katika kuhabarisha umma ili uweze kushiriki kikamilifu katika tuzo hizi. Inatosha kusema tangu zoezi hili lianze TCRA imepata ushirikiano mkubwa kutoka vyombo vya habari, ingawa bado TCRA inaamini ushiriki wa vyombo vya habari ungeweza kuwa mkubwa zaidi,” anasema Mhandisi Kilaba.

Anasema kuwa kuna mambo ambayo TCRA inegependa kushirikishana na vyombo vya habari na hii inatokana na utashi wao wa mkataba uliopo katika huduma kwa wateja ambao umekusudia kuimarisha utamaduni wa utendaji  bora unaozingatia mahitaji, matakwa na matarajio ya wateja na wananchi kwa ujumla.

Anaweka wazi kuwa mkataba huo umejitanabaisha kujali zaidi mteja wa TCRA na kutoa rai kwa kwa wahariri kuonyesha ushirikiano katika tuzo hizo ambazo wao ni sehemu kamili ya wadau wa mawasiliano.

Mhandisi Kilaba anabainisha kuwa moja ya malengo ya kuanzishwa kwa tuzo hizo ni kuwatambua na kuwatunuku watoa huduma bora zaidi za mawasiliano nchini.

Amesema hilo litaongeza ubunifu katika huduma za utangazaji, kuongeza ubora na ufanisi wa huduma za mawasiliano katika sekta  za posta, simu, utangazaji na intaneti na kuongeza chachu na mchango wa sekta ya mawasiliano katika kukuza uchumi na maendeleo ya teknolojia ya dijiti.

Lengo jingine la tuzo hizo ni kuwawezesha watoa huduma kujifunza kutoka kwa wenzao kwa kuangalia mambo ambayo yamewafanya washinde tuzo hizo na kwa nini wao wameshindwa.

“Tunaamini kuwa yule aliyeshindwa ataangalia ni jambo gani limemfanya mwenzake ashinde ili naye akalifanye kwa ubora zaidi ili mwakani ashinde. Hiyo itasaidia kuongeza ubora wa huduma na ubunifu,” anafafanua.

Aidha, amesema tuzo hizo zitawaongezea watoa huduma kujiamini hasa wale ambao watashinda kwani kura zitapigwa na wateja wa huduma hizo.

Ili kuboresha uandishi wa habari za mawasiliano, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevile Meena, ameishauri TCRA kuwa na kundi la waandishi ambao wataelimishwa kwa kina katika eneo hilo.

Amesema hilo litawezesha kuwepo kwa waandishi wabobevu katika sekta ya mawasiliano, hivyo kufanya ufikishaji wa ujumbe kuhusu masuala ya mawasiliano kwa jamii kuwa mzuri na wa ufanisi mkubwa.

Amesema itakuwa rahisi kwa waandishi hao wabobevu kuibua masuala ya msingi katika sekta hiyo badala ya utaratibu wa sasa ambapo waandishi husubiri matukio yanayohusu sekta ya mawasiliano ili kutoa habari zake.

Pia, Meena amebainisha kuwa waandishi hao wataweza kuripoti kwa kina masuala ya mawasiliano na ingawa suala hilo ni la kiteknolojia, lakini ubobevu wao utawawezesha kuripoti kwa lugha ambayo itaeleleweka kwa wepesi kwa Watanzania wengi.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Matumizi ya TEHAMA wa TCRA, Connie Francis, amesema kutakuwa na tuzo 17 zitakazotolewa kwa watoa huduma ambao, kwa wale watakaopenda kushiriki kwenye tuzo hizo, watawajibika kujiandikisha kwa kujaza fomu maalumu.

Akifafanua, alisema kutakuwa na vipengele kadhaa kama vile mtoa huduma bora za mtandao wa simu, mtoa huduma bora wa intaneti, mtoa huduma bora wa miundombinu ya utangazaji na mtoa maudhui bora wa blog.

446 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!