Wakati Watanzania wengi wakiwa wameamua kuwaanika hadharani nguli wa biashara ya dawa za kulevya, Balozi wa Tanzania nchini China, Philip Marmo, naye amepasua ukweli wa mambo akisema hali inatisha.

Anasema biashara hii inawahusisha “watu wakubwa”, na kwamba rushwa ndiyo inayofanya imashamiri. Ingawa Balozi huyo hawataji vigogo aliotajiwa na Watanzania waliofungwa na walio mahabusu nchini China na kwingineko, Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan (pichani), ni miongoni mwa walio kwenye barua iliyoandikwa na Mtanzania mmoja.

 

Mbunge huyo amejitokeza haraka haraka kukanusha taarifa hizo. Kana kwamba haikutosha, alikwenda polisi akiomba achunguzwe na akaahidi kuwa yupo tayari kujiuzulu ubunge endapo itathibitika kuwa anahusika.

 

Mtanzania anayejitambulisha kuwa yupo mahabusu huko Hong Kong, ameamua kuwataja baadhi ya vinara wa biashara hiyo haramu waliopo hapa nchini (soma barua yake tuliyoambatanisha hapa). China pekee kuna Watanzania zaidi ya 170 walio magerezani kutokana na biashara hiyo. Brazil wapo zaidi ya 100. Watanzania wengine 132 wapo katika magereza mbalimbali duniani kote.

 

Anawataja baadhi ya wahusika wakuu kuwa ni wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wanaoshika nafasi mbalimbali za uongozi katika Taifa letu. Kwa upande wake, Balozi Marmo amesema idadi ya Watanzania walio katika magereza na mahabusu huko China, Hong Kong na Macao, inatisha.

 

Alipoulizwa hatima ya Watanzania hao, Balozi huyo amesema, “Tunawapa ushauri nasaha kwa sababu kuna udanganyifu mkubwa kwenye magereza hayo (walimofungwa), wengine wanaambiwa kwamba kuna uwezekano wa kuwarejesha nyumbani ili wamalizie vifungo vyao, lakini huwa tunawaambia hili jambo haliwezekani kwa sababu Tanzania na China, Tanzania na Hong Kong na Tanzania na Macao hatuna mikataba ya kubadilishana wafungwa.

 

“Na wala hatuna sasa hivi uwezekano wa kufanya jambo hili kwa sababu mzigo ni mkubwa, laiti ingepita miaka miwili au mitatu bila kuwa na mtu au mhalifu wa kuleta dawa za kulevya, tungekuwa na mjadala na mataifa haya.”

Anasema Balozi Marmo, “Kunakuwa na uchunguzi mkali sana, unachukua wakati mwingine hadi miaka mitatu. Hujui (hao watuhumiwa) wanazielezea nini mamlaka za hapa.”

 

Vigogo wanahusika

“Wanawahusisha watu wakubwa kule kwetu nyumbani, wanahusisha mitandao mikubwa duniani ya dawa za kulevya. Hivyo nchi hizi zinasita, zinasita sana kuwarejesha kwa sababu wanadhani wakiwarejesha hawatapata adhabu wanayostahili.”

Kwa kawaida, adhabu katika mataifa hayo ni kunyongwa hadi kufa, vifungo vya maisha au vifungo vya maisha marefu. Sheria za Tanzania ni legelege, kiasi kwamba mtu anayetiwa hatiani anaweza kulipa faini na kuachiwa huru.

 

Wasafirisha dawa za kulevya

Balozi Marmo anasema biashara hiyo inawahusisha watu wa rika, jinsi na hali zote.

 

“Acha umri, lakini hali ya maisha yenyewe…ni watu masikini sana, au ni vijana wadogo sana, kwa kweli kuna kila aina, kutoka umri mdogo wa miaka 15 mpaka miaka 57 na kutoka watu wa maisha duni na watu ambao kwa hali ya Tanzania unasema ni watu matajiri.

 

“Nikutolee mfano wa binti mmoja sitaki kutaja jina lake, alikamatwa wiki mbili zilizopita huko Hong Kong na kwa sababu alikuwa na maisha mazuri, alikuwa na maduka kadhaa – Kinondoni maduka mawili, Mwanyamala maduka manne, maeneo ya Sinza maduka kadhaa, anaishi maeneo ya Mikocheni, ana magari mawili ya kifahari – aliposhikwa alikuwa na dola 10,000 (dola moja ya Marekani ni wastani wa Sh 1,620).

 

“Alichanganyikiwa, ilibidi apelekwe kwenye taasisi ya watu wenye magonjwa ya akili kwa watuhumiwa – kule kwetu ni kama Mirembe au Isanga.

 

“Hao ni watu wa aina moja – watu wenye uwezo kidogo, lakini wanashawishika kuja kufanya kazi hii. Wengine ni vijana wadogo – miaka 15; wengine watu wazima kabisa. Mtu mzima niliyemwona ni mwana mama kutoka Unguja ana miaka 57 na yeye wala hali yake si duni sana. Ana maduka Kinondoni, ana maduka pale Darajani (Zanzibar), na ameweza kuifanya kazi hii kwa muda mrefu.

 

“Kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba ni watu wa aina mbalimbali. Ni watu wenye maisha duni, watu wenye maisha ya kawaida huko nyumbani, wengine ni watu wenye maisha ambayo ni ahueni kidogo.”

 

Maeneo wanakotoka

Anasema wengi wanaokamatwa wanatoka mijini nchini Tanzania. “Kijiografia wengi wanatoka mijini, na hasa mji wetu wa Tanga ndiyo unaotoa watu wengi zaidi, ukifuatiwa na Magomeni, Kinondoni na Unguja.

 

“Kwa sababu watu wengi wanatoka kwenye miji mikubwa, katika majalada yao wanaandika ametokea Magomeni, Kiondoni, Tanga Barabara ya Nane, Tanga Makorora, Mjini Magharibi, lakini ni wachache nimewahi kuona mtu labda anatoka Moshi. Wapo wachache sana,” anasema.

 

Anataja viwanja vya ndege kuwa ndiyo maeneo makuu yanayotumiwa kusafirisha dawa za kulevya kutoka Tanzania.

 

“Hasa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam (Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere), uwanja wa ndege wa Zanzibar kutakuwa na hali kama hii kwa sababu wengine wanakuja na mizigo mikubwa zaidi ya kilo moja, uchunguzi wa kawaida kilo moja ingeweza ikagundulika pale uwanja wa ndege.

“Hakuna tukio kwa hapa China, Hong Kong na Macao kwa waliotokea Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro.”

 

Wosia wa wanaokamatwa

“Wengine wanatushauri, hasa wafungwa wenyewe wanatushauri tuwe tunaweka vibao pale uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, pale pa kuingilia, na uwanja wa ndege wa Zanzibar, kueleza kuwa tafadhali ukijaaliwa kuvuka na dawa za kulevya, unakoenda utakamatwa tu, kuna teknolojia ya kubaini hizo dawa.” Anasema wanaovuka kirahisi ni wanawake.

 

“Nimezungumza nao na taarifa walizonipa ni kwamba wanawezeshwa. Rushwa hasa ndiyo tatizo,” anahitimisha Balozi Marmo.

Please follow and like us:
Pin Share