Na Jovina Massano, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali kuwachukulia hatua watu na kampuni zinazoendelea kuzalisha bidhaa za mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku.

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Mhandisi Hamad Masauni ametoa onyo kwa wanaoingiza na kuzalisha bidhaa za mifuko ya plastiki wakiwemo wanaoingiza kupitia njia za panya.

Amesema serikali kupitia Mamlaka za usimamizi wa mazingira kufanya doria za kushtukiz katika viwanda vinavyozalisha vikiwemo viwanda bubu na Masoko ya bidhaa hizo ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika wote wanaojihusisha na biashara hiyo.

Ameeleza hayo leo jijini Dodoma kuelekea maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani ambayo kilele chake kitakuwa jijini humo mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan.

Uchukuaji wa hatua hiyo unatokana na kujitokeza kwa changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya mabomba (tubings) kutumika kama vibebeo visivyo na Sifa visivyokidhi matakwa yaliyowekwa na shirika la viwango Tanzania (TBS).

Hivyo basi Mhandisi Masauni amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira (NEMC),Mamlaka za serikali za mitaa na Mamlaka nyingine za Umma kuendelea kufuatilia na kuwabaini wahusika wote wanaaokiuka Sheria na kuzalisha bidhaa zza plastiki zilizopigwa marufuku hapa nchini.

Hakusita kuwakumbusha watanzania kuzingatia maelekezo ya serikali na kuachana na mifuko ya plastiki na badala yake watumie mifuko mbadala ambayo kwa sasa inapatikana nchini kote kwa ghalama nafuu.

Juni,2019 hatua zilichukuliwa ambapo serikali ilipiga marufuku uzalishaji,uingizaji,usambazaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki iliyoweza kusaidia kupunguza changamoto ya uchafuzi wa mazingira.

Katika kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu kutambua mifuko na vifungashio vya plastiki vilivyoruhusiwa serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma ikiwemo ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa mifuko mbadala iliyo rafiki kwa mazingira.

Maonyesho hayo yatachagizwa na maonesho ya wadau wa bidhaa,huduma na ubunifu kuhusu hifadhi ya mazingira yatakayoanza Juni mosi hadi 5,2025 jijini Dodoma sambamba na kongamano la Vijana litakalowakutanisha vijana mbalimbali wa vyuo,wajasiriamali na mabalozi wa mazingira litakalofanyikia jijini Dar es salaam Juni 3,2025.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Tanzania ijayo Tuwajibike Sasa,Dhibiti Matumizi ya Plastiki ” inayolenga kuikumbusha jamii kutambua umuhimu wa mazingira na rasilimali zake kuwa ni msingi wa uhai na maisha pamoja na ukuaji wa uchumi.