Na Meleka Kulwa, Dodoma
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) na kukabidhi magari 19 kwa ajili ya ofisi za makao makuu na wilaya mbalimbali nchini.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Waziri Aweso alisema RUWASA ilianzishwa kutokana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini, jambo lililopelekea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuona umuhimu wa kuanzishwa kwa wakala huo.

“Leo hii suala la ujenzi wa miradi ya maji vijijini siyo tatizo tena. Namshukuru sana Rais Samia kwa kuwa ujenzi wa taasisi hii unaenda sambamba na mazingira bora ya kazi kwa watumishi,” alisema Waziri Aweso.
Ameeleza kuwa Rais Samia alitoa kiasi cha Shilingi bilioni 24 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya RUWASA, na kupongeza juhudi hizo akisema: “Hakika Rais wetu ni mjenzi. Yote aliyotufanyia tutamlipa kwa kufanya kazi kwa bidii, kwani amefanya kazi kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini.”
Ameongeza kuwa watahakikisha wanamfuatilia mkandarasi kwa karibu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, na fedha zitatolewa kwa wakati ili kuondoa changamoto au malalamiko yoyote.
“Ujenzi bora wa miradi ya maji unaendana na usimamizi makini na ufuatiliaji wa karibu. Nitahakikisha RUWASA wanapata ushirikiano wote wanaouhitaji ili kukamilisha yote waliyokusudia,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Bi. Ruth Koya, alimshukuru Waziri Aweso kwa kuonesha uangalizi wa kipekee kwa taasisi hiyo, akisema magari 19 yaliyotolewa yataongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya RUWASA.
“Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kumtua mama ndoo kichwani na anaendelea kutekeleza hilo kwa vitendo. Waziri wa Maji naye anatekeleza wajibu wake kwa dhati. Magari haya yatasaidia kufanikisha lengo la Ilani ya CCM ya kuhakikisha huduma ya maji vijijini inafikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2025,” alisema.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Ushauri Elekezi wa mradi huo, Bw. Peter Salyeem, aliwasilisha taarifa ya maendeleo ya ujenzi, akieleza kuwa mchakato ulianza Machi 2022 kwa maandalizi ya michoro, tathmini ya gharama na mazingira. Ujenzi ulianza rasmi Novemba 2023.
Alieleza kuwa mradi huo unagharimu Shilingi bilioni 24.9, huku gharama za ushauri elekezi zikiwa Shilingi milioni 499. Fedha zote zinatolewa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maji.

“Mradi huu unahusisha ujenzi wa jengo kuu la ofisi ya RUWASA, kazi za nje, majengo saidizi kama mgahawa, kibanda cha mlinzi, jengo la jenereta pamoja na uzio wa eneo lote la kiwanja,” alisema.
Alibainisha kuwa mkandarasi wa mradi ni kampuni ya China Jiangxi International Economic and Technical Company Limited, huku mshauri elekezi akiwa ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12, kuanzia Novemba 2023 hadi Desemba 31, 2024, na hadi sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka RUWASA, Bw. Titus Mkapa, alithibitisha kuwa magari yaliyokabidhiwa ni 19 na yataelekezwa kwenye ofisi za makao makuu pamoja na wilaya ili kuongeza ufanisi wa shughuli za utoaji huduma za maji vijijini.

