Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Kigoma

Mgombea ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Zainabu Katimba, amewaomba wananchi wa Kigoma kumpa kura Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na mafanikio makubwa aliyopeleka kwenye mkoa huo.

Amesema Rais Samia amepeleka mafanikio katika sekta ya afya na kuufungua kiuchumi mkoani huo.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Katosho leo Septemba 14,20205 mkoani Kigoma Katimba amesema mkoa huo umepata baraka kubwa kupitia uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Rais Samia.

Amesema katika kipindi cha miaka minne, zaidi ya Sh trilioni 11.4 zimepelekwa Kigoma kwa ajili ya maendeleo mbalimbali, huku wananchi wa Kigoma Mjini wakiwa ni miongoni mwa wanufaika wakuu.

Amesema kupitia Ziwa Tanganyika, Rais Samia ameonesha dhamira ya kuligeuza kuwa kitovu cha biashara kwa nchi jirani za Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

“Hili linathibitishwa na fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa meli tatu, pamoja na kuimarisha masoko ya kimataifa na miundombinu ya bandari,”amesema.

Amesema Sh bilioni 16.4 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa soko la Mwanga, litakalowawezesha wafanyabiashara wa Kigoma kushirikiana na wenzao kutoka Burundi na Zambia, hivyo kuongeza mzunguko wa fedha na kukuza kipato cha wananchi.

Amesema Kigoma itanufaika pia na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa gharama ya Sh trilioni 7, itakayoiunganisha Kigoma na masoko ya Burundi na DRC.

Kuhusu afya, Katimba amesema Rais Samia amefanya uwekezaji mkubwa kwa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, kuimarisha Hospitali ya Maweni, na kujenga Chuo Kishirikishi cha Muhimbili , sambamba na vituo vya afya 26 vilivyoboreshwa na zahanati 65.

Amesema hatua inayolenga kuboresha huduma za afya na kuimarisha ustawi wa wananchi.

“Tochi tatu za maendeleo ya kwanza ikiwa ni Rais, ya pili Wabunge, na ya tatu Madiwani,Tukiweka kigunzi katikati, tochi ya maendeleo itazimika. Ndugu zangu wa Kigoma tumpe Rais Samia kura zote ili mwanga huu wa maendeleo uendelee kuangaza,”amesema.