Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Injinia Yahya Samamba kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Bw.Anthony Mavunde amezindua kamati ya Masoko na Mawasiliano ya Taasisi ya Umoja wa Watoa Huduma katika Sekta ya Madini nchini (TAMISA) na kuwataka wadau na wanachama kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta hiyo hapa nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ukiwa na kauli mbiu “Mchango wa Wagavi Wazawa kwenye sekta ya madini Nchini”, Injinia Samamba alisema kuwa wakati umefika kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta hiyo baada ya kamati hiyo kuzinduliwa.
“Tamisa inaenda kufungua fursa nyingi kwa Wazawa kama ilivyo azma ya Serikali katika kuhakikisha Watanzania wanafaidika kwanza kutokana na rasimali zilizopo hapa nchini,” alisema injinia Samamba.

Injinia Samamba aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 na 2014/2015, Serikali ilikuwa inakusanya bilioni 164/- , lakini baada ya maboresho mbalimbali kufanyika, matarajio ni kukusanya takriban trilioni moja.
“Haya yote ni kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika miaka minne ya utawala wale”, alisema.
Injinia Samamba aliongeza kuwa anaamini kupitia TAMISA, mapato ya nchi yataongezeka kwa wadau mbalimbali kushiriki katika mnyororo wa thamani.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi za Serikali, wanachama wa TAMISA na wamiliki wa migodi na watoa huduma kwenye sekta hiyo.

Injinia Samamba aliweka wazi kuwa Rais Samia ametumia 4R katika kuboresha Wizara ya Madini kwa kuwa na majadiliano na wachimba madini na kufanyia kazi maombi yao, ambapo pamoja na mambo mengine, wameondolewa kodi ya ongezeko la thamani pamoja na kodi ya zuio ili wafanye kazi kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wake, Kamishina wa Madini nchini Dkt Theresia Numbi alisema kuwa wazo la kuanzishwa kwa TAMISA ilikuwa ni ndoto ya muda mrefu ya Waziri Mavunde ya kuhakikisha wazawa wananufaika kwanza kupitia sekta hiyo .
“Lengo la Rais Samia ni kuona sekta ya madini inachangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa sekta nyingine” alisema Dkt Numbi.
Pamoja hayo, Dkt Numbi alisema Serikali iliamua kufanya marekebisho ya sheria ya Madini ya mwaka 2010, ambapo suala la ushirikishwaji kwa Watanzania (local content) limekuwa suala la kisheria na sio ombi, hivyo kuyataka makampuni ya madini kununua bidhaaa na huduma kutoka kwa wazawa.

Naye Mwenyekiti wa Tamisa Bw. Peter Kumalilwa alisema wao kama taasisi watahakikisha kazi na huduma za makampuni yao zinatekelezwa kwa ufanisi, weledi na ushindani katika soko la ndani na la kimataifa.
Bw Kumalilwa alielezea malengo makubwa ya TAMISA ni pamoja na kusaidia wanachama wao kukuza biashara ya watoa huduma migodini, kuwajengea uwezo ili waweze kushindana katika sekta ya madini na kutetea haki za wanachama wao .
Naye Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa TAMISA Dkt Sebastian Ndege alisema wataendelea kukuza ushirikiano kati ya wanachama wao na kujifunza namna bora ya utoaji wa huduma ili kuweza kufungua fursa za wazawa wengi katika sekta ya madini.
