WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuongeza rasilimali watu, bajeti, miundombinu na kufanya marekebisho ya kisheria ili kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya rushwa.


Amesema kwa juhudi hizo, TAKUKURU imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 60.2, ambazo zimeelekezwa katika huduma muhimu za jamii zikiwemo afya, elimu, maji, umeme na miundombinu.

Pia, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, Jamhuri imeshinda asilimia 68.8 ya kesi 489 zilizofikishwa mahakamani, ikionyesha ubora wa uchunguzi na ushirikiano kati ya TAKUKURU na Mahakama ya Tanzania.


“Rushwa inadhalilisha utu wa binadamu na inazorotesha utoaji wa huduma za jamii. Ni lazima tuchukue hatua za kuzuia kabla haijazalisha madhara. Rushwa ni ajenda ya kitaifa inayohusu pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisisitiza Dkt. Nchemba.


Ameyasema hayo leo Jumatatu, Januari 26, 2026, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Cate Convention Centre, mkoani Morogoro.


Aliongeza kuwa taasisi za Serikali lazima zibainishe na kuziba mianya ya rushwa hususan katika maeneo ya manunuzi ya umma, utekelezaji wa miradi, na usimamizi wa mikataba, kwani zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya Serikali hupitia katika maeneo hayo.

Waziri Mkuu pia aliwahimiza Watanzania kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, akisisitiza usiri wa watoa taarifa. Aidha, aliwahimiza kushirikisha sekta binafsi, wadau wa kimataifa, pamoja na vijana na wanawake katika jitihada za kupambana na rushwa.


Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa Serikali iko tayari kufanya marekebisho ya kisheria na kiutawala pale itakapobainika kuna vikwazo vinavyoathiri utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU, akiwataka viongozi wa taasisi hiyo kuwasilisha mapendekezo yao bila kusita. Pia aliagiza ushirikiano wa karibu kati ya TAKUKURU na Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma ili kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika utendaji wa watumishi wa umma.


Aidha, Waziri Mkuu alielekeza taasisi za Serikali kubaini na kuziba mianya ya rushwa hususan katika maeneo ya manunuzi ya umma, utekelezaji wa miradi, na usimamizi wa mikataba, akibainisha kuwa maeneo haya yanahitaji uangalizi wa karibu kutokana na asilimia kubwa ya bajeti ya Serikali kupitia hapo.


Akisisitiza mwelekeo wa Taifa, Dkt. Nchemba aliunganisha jitihada za TAKUKURU na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akibainisha kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni msingi wa kuimarisha ustawi wa wananchi, maendeleo endelevu, uadilifu, na uwajibikaji wa Taifa.

Vilevile, aliangazia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025–2030, ambayo inaweka wazi mapambano dhidi ya rushwa kama nguzo muhimu ya demokrasia, utawala bora, na ustawi wa wananchi.


Waziri Mkuu alimalizia hotuba yake kwa kutoa wito kwa viongozi wa TAKUKURU kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanakuwa chachu ya kuongeza bidii zaidi, huku akisisitiza kaulimbiu ya mkutano:
“Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”


Baada ya hotuba hiyo, Waziri Mkuu alitangaza rasmi ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2025 wa Viongozi wa TAKUKURU.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Katika ukumbi wa mikutano wa Cate Mkoani Morogoro (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akipokea kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa  Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Crispin Chalamila, tuzo kwa ajili ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutambua mchango na uongozi wake imara ulioiwezesha  TAKUKURU kujiimarisha katika  mapambano dhidi ya rushwa, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia  katika mkutano wa mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU, Katika ukumbi wa mikutano wa Cate Mkoani Morogoro (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)