Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Augustin Matata Ponyo, amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela pamoja na kufanya kazi ngumu, baada ya kupatikana na hatia ya ubadhirifu wa fedha za umma.
Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya Katiba ya DRC kufuatia mchakato wa kisheria uliodumu kwa karibu miaka minne. Mahakama hiyo ilibaini kuwa Matata alihusika na matumizi mabaya ya fedha za umma zenye thamani ya dola milioni 247 za Marekani.
Matata, ambaye aliwahi kuwania urais mwaka 2023 kabla ya kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho, amekuwa akikanusha tuhuma hizo akizielezea kuwa na msingi wa kisiasa.
Mbali na Matata, Mahakama hiyo pia imemhukumu mfanyabiashara mmoja raia wa Afrika Kusini kifungo cha miaka mitano jela na kufanya kazi ngumu, pamoja na Deogratias Mutombo, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Congo wakati wa tukio hilo.
Aidha, Mahakama imepiga marufuku kwa Matata na Mutombo kushika nyadhifa yoyote ya umma kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kumaliza adhabu zao. Kwa upande mwingine, mfanyabiashara huyo wa Afrika Kusini ameagizwa kurejeshwa kwao mara baada ya kutumikia kifungo chake.
