Wiki iliyopita wahariri wa vyombo vyote vya habari nchini walikutana mjini Morogoro kujadili mustakabali wa tasnia ya habari nchini. Mkutano huo ulipaswa kufunguliwa rasmi na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.  Waziri alikuwa na taarifa zaidi ya miezi miwili. Jumamosi ya wiki iliyopita ndipo akatuma ujumbe mfupi wa simu kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, akimweleza kuwa asingeweza kufika.
Kiungwana kabisa si tu kuwa Mukangara alieleza kuwa asingeweza kufika akaishia hapo, bali alisema amemteua Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Seth Kamuhanda amwakilishe kwenye mkutano huo. Siku hiyo hiyo ya Jumamosi, Kamuhanda akawasiliana na MCT akisema alikuwa haoni barua ya maombi na hotuba iliyopendekezwa kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano huo.

MCT wakafanya kila mbinu na kumjulisha nani aliyepokea barua na hotuba hiyo ya mapendekezo mahali ilipofikishwa wizarani. Kamuhanda hakusema jingine, ila siku ya Jumatatu ya wiki iliyomalizika wakati wanahabari wakiwa tayari ukumbini Morogoro, ndipo Kamuhanda alipompigia simu Mukajanga kumweleza kuwa asingeweza kufika kwenye ufunguzi wa mkutano huo.

Nikiwa mmoja wa wahariri, mbali na kukerwa na hatua ya vibosile hawa wawili, nilipata tafsiri ya dharau kwa wahusika wote wawili. Dharau hii ilitokana na ukweli kwamba baada ya Kamuhanda kushindwa kutekeleza agizo la bosi wake, alikuwa anawajibika kumtuma mkurugenzi yeyote kutoka wizarani kwake au mkuu wa Mkoa wa Morogoro au hata mkuu wa wilaya kwa ajili ya kushiriki mkutano huo.

Inawezekana kabisa wapo watu wenye kujiuliza kulikoni wahariri wakereke kwa Mukangara na Kamuhanda kutofika na kushiriki mkutano huo. Hoja ya msingi ni moja tu yenye kuzaa sintofahamu hii. Serikali ni mdau mkubwa katika tasnia ya habari nchini. Mkutano wa kiwango cha wahariri unapokaa, inakuwa ni serikali ya aina yake isiyopata si shauku ya kujua kilichojadiliwa tu, bali pia fursa ya kuwasiliana na wadau hawa muhimu.

Ikumbukwe kuwa Mukangara ndiyo kwanza amekuwa waziri mwenye dhamana na masuala ya habari. Kabla ya hapo alikuwa Naibu Waziri. Hakuwa na mamlaka kamili. Kwake hii ilikuwa ni fursa adhimu ya kufahamiana na wahariri na kujua jinsi atakavyoweza kufanya kazi na vyombo hivyo ambavyo ni nguzo ya maendeleo kwa taifa lolote lililoendelea duniani.

Inawezekana daktari huyu wa falsafa hajui umuhimu wa vyombo vya habari. Ndiyo maana baadhi ya wahariri kutoka magazeti mawili ya kila siku, wamewaambia wahariri wenzao kuwa Mukangara akiwa Naibu Waziri ametamka mara kadhaa kuwa angekuwa na mamlaka angeweza kulifuta gazeti la Mwananchi na Tanzania Daima. Sasa mamlaka anayo.

Kwa mujibu wa sheria ya sasa (hata kama ni mbovu) anaweza kujisikia tu hata akiwa usingizini nyumbani kwake, akaagiza kuwa magazeti hayo yafutwe au hata hili ikiwa linamkera pia na hatakiwi kutoa sababu. Napenda kumuonya mapema kuwa kama hayo ndiyo mawazo, bora aombea Rais Jakaya Kikwete atengue uteuzi wake mapema ama amuhamishe kutoka wizara hii au yeye aende huko Tandahimba akalime korosho.

Akitaka kuifahamu vyema nchi hii akamuulize mzee John Samuel Malecela. Alipoteuliwa tu kuwa Waziri Mkuu, alisema: “Dar es Salaam kuna joto la aina mbili. Kuna joto la asili linalofanya watu wapate upele, lakini pia kuna joto la magazeti. Hasa hili la pili linawasha kuliko upupu.” Ni kwa mantiki hiyo namuonya Mukangara kuwa kama amekuja na dhana ya kufuta magazeti, amekosea. Dhana hiyo ni sawa na kuingia Msikitini ukitanguliza mguu wa kushoto!

Sitanii, katika kikao kile tumeelezwa mambo mengi. Tumejulishwa kuwa Kamuhanda na Mukangara haziivi. Ndiyo maana Kamuhanda baada ya kupewa kazi, alipiga tena simu MCT kuomba atumiwe upya ratiba, barua ya maombi na hotuba wakati uhalisia vitu hivyo viliwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana.

Binafsi namshangaa mno Kamuhanda. Huyu amekuwa mwanahabari, amekuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Serikali, kwa kila kigezo nilitarajia awe wa mwisho kudharau wahariri wenzake. Naifahamu tabia yake binafsi. Kwamba alipokuwa Daily News hata upepo ukitikisa mapazia anaukemea. Chumba cha habari alikigeuza lango la Adolf Hitler kuingia Ikulu. Enzi Hitler akiwa katika Ikulu ya Wajerumani hata mjusi alikuwa hakatizi juu ya pa la White House.

Inawezekana usultani huu ndiyo alioubeba Kamuhanda na kwenda nao Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Anataka Waziri au Naibu Waziri ikiwa ana jambo amfuate yeye ofisini kwake na sisi yeye kama msaidizi wa viongozi hao awaendee wao. Kwa kila hali na ninavyoufahamu mfumo wa serikalini, ni lazima avune migogoro.

Sitanii, hoja ya wahariri ilikuwa ni kukutana na viongozi hawa wakuu ambao wangefahamishwa ulikofikia mchakato wa Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari na Muswada wa Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari, iliyopiganiwa kwa karibu miaka 10 sasa. Hapa tunataka kuishawishi Serikali ione nia ya dhati ya wahariri kudai miswada hii.

Nikiwa Morogoro niliwachekesha wahariri kwa kuwaambia hivi: Si aibu kutenda mambo ya aibu ila ni aibu kufahamika kuwa unatenda mambo ya aibu. Hii maana yake ni nini? Watendaji wa halmashauri za wilaya wanaokwiba fedha za umma kwao si aibu kuiba fedha hizo, lakini vyombo vya habari vikipewa zana za kufanyia kazi mapato ya serikali yataongezeka.

Sheria ikizibana kampuni binafsi, watendaji katika idara mbalimbali – iwe ni za Serikali au wakala na mamlaka kwa mujibu wa sheria wakatakiwa kutoka habari –  kasi ya maendeleo itakuwa kubwa. Kuna mtu alisema hivi karibuni halmashauri zote ambazo hakuna waandishi wa habari ndizo zenye hesabu chafu kupita kiasi. Kazi ya wanahabari ni kumulika yanayoendelea na hivyo kama ni matendo ya aibu yakifahamika kuwa wahusika wanayatenda, itakuwa aibu kwao na yatakoma.

Uhuru wa vyombo vya habari unatoa fursa ya watu kuchunguza mwenendo na utendaji wa vyombo mbalimbali, ikiwamo wimbi la wafanyabiashara wakwepa kodi. Wengi wa wafanyabiashara wanatisha wateja kuwa wakiwapatia risiti basi bei inaongezeka kwa asilimia 18. Hivi nani kawaambia kutangaza bei zisizojumuisha kodi kwenye bidhaa wauzazo.

Sitanii, hayo yote nayasema lakini hoja ya msingi ni kuwaeleza wakubwa hawa –  Mukangara na Kamuhanda – kuwa wao si wa kwanza kuwa katika wizara hii na wala wasitarajie kuwa wao ndiyo wa mwisho. Kazi iliyowaweka hapo ni kuwatumikia wananchi na wadau wao wakuu ni wanahabari.

Kwa bahati mbaya Serikali imekuwa na tabia ya kuvikimbilia vyombo vya habari pale tu yanapotokea matatizo. Likizuka jambo zito kama ndugu zetu Zanzibar walivyoanza kuchoma makanisa, hapo wanahabari wananyenyekewa. Ukifika uchaguzi wanakuwa tayari hata kuwaandalia magari ya kusafiri nao, mimi nasema hapana. Tunahitaji sheria na si upendeleo.

Uhuru wa habari tulionao sasa unatokana na huruma ya Rais Kikwete. Kama waziri anaweza kuwatamkia baadhi ya wahariri kuwa angependa kufuta baadhi ya magazeti, huyo unadhani ana moyo wa kufanya kazi na wahariri?

Mwisho, naomba kuhitimisha kama nilivyoanza. Taifa letu litajua kuwa Mukangara na Kamuhanda hawana mpasuko pale tu watakapotokea kwenye mkutano wa wanahabari wakiwa pamoja. Mtindo huu wa Kamuhanda kujitokeza peke yake na kusema hana mvutano, siamini kama unakidhi haja. Jukwaa la Wahariri nawasihi tuendelee na mpango wa kuwasilisha malalamiko yetu kwa Rais Jakaya Kikwete, kumweleza kuwa mwenendo wa wachungaji aliotukabidhi hauridhishi.

1257 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!