#Kiwanda kinauwezo wa kuzalisha tani 600 za chumvi kwa siku

#Kimetoa ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 500

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Wito umetolewa kwa wazalishaji wa madini ya chumvi nchini kupeleka malighafi hiyo katika Kiwanda cha Neelkanth Salt Limited kilichopo Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali leo Desemba 19, 2023 alipotembelea Kiwanda hicho akiongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah sambamba na Wataalam kutoka Wizara zote mbili kwa lengo la kujionea hali ya upatikanaji wa malighafi katika kiwanda hicho cha Chumvi.

Amesema kuwa ni fursa kwa wazalishaji wa madini ya chumvi kupeleka na kuuza bidhaa hiyo katika kiwanda hicho kwa kuwa kina mahitaji makubwa ya chumvi ghafi hali inayoweza kupelekea kupungua kwa uzalishaji wa kiwanda hicho.

“Tunatoa wito kwa mtu yeyote mwenye chumvi kuleta hapa, kiwanda hiki kimebakiwa na malighafi tani 500 inayotosha kutumika kwa siku moja tu, kwahiyo uhitaji ni mkubwa na tumefika hapa kuona hali halisi, kiwanda kinahitaji malighafi ili kiendelee na uzalishaji wake.” amesema Mahimbali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha Wawekezaji na Wafanyabiashara wanafanya shughuli zao bila kikwazo chochote ili kulinda ajira za watanzania walioajiriwa kwenye viwanda lakini pia Serikali inapata mapato yake stahiki kupitia kodi na hatimaye kila upande unapata faida kutokana na uwekezaji huo.

“Tumekaa kikao upande wa Serikali, mwenye kiwanda na wazalishaji na tumekubaliana tutoe mwezi mmoja kwa ajili ya mwenye kiwanda na wazalishaji wa Chumvi, kwanza kujadiliana njia bora ya kuendelea kufanya biashara, pili Chumvi iendelee kuletwa kiwandani kama mwanzo hivyo kila mwenye Chumvi alete hapa kiwanda hiki kitanunua ili kiendelee na uzalishaji pamoja na kulinda ajira za Watanzania walioajiriwa kiwandani.” amesema Dkt. Abdallah.

Naye, Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Ahmed Said Ahmed amebainisha kuwa kiwanda hicho kimeajiri zaidi ya wafanyakazi 500 kinazalisha tani 600 za Chumvi kwa siku hivyo uhitaji wa Chumvi ghafi ni mkubwa sana na kuomba Wazalishaji wa Madini hayo kupeleka kiwandani na kwamba kiwanda kitanunua kiasi chote cha chumvi kitakacholetwa kiwandani.

Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Wazalishaji wa Chumvi nchini (TASPA), Mwekahazina wa Chama hicho Aboud Noordin Hussein amesema kuwa kiasi cha Chumvi walichonacho kinatosha kulisha mahitaji ya viwanda vya Chumvi nchini na kwamba wako tayari kupeleka chumvi katika kiwanda hicho cha Neelkanth Salt Limited.

By Jamhuri