Kamati ya wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inayosimamia dharura za afya kimataifa imeamua kwamba ugonjwa wa Mpox bado ni dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi duniani.
Uamuzi huu ulifikiwa katika mkutano wa tatu wa Kamati ya Kanuni za Afya za Kimataifa, ambapo ilimshauri Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, kuendeleza hali ya dharura kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa na kusambaa kwa ugonjwa huo.
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, juhudi za kudhibiti Mpox zimeathiriwa na changamoto za usalama na ukosefu wa rasilimali. Katika miji ya Goma na Bukavu, zaidi ya wagonjwa 400 walikuwa wanapata matibabu, ingawa baadhi yao tayari wametoka hospitalini. Hata hivyo, kuna hofu kuwa wagonjwa ambao hawajajitokeza wanaweza kuwa wakisambaza ugonjwa huo miongoni mwa jamii.
Mpox bado ni tishio barani Afrika, ambapo mataifa 22 yameripoti visa 21,067 vilivyothibitishwa na vifo 74. Nchi 14 kati ya hizo zinaendelea kukabiliwa na mlipuko, huku Afrika Kusini ikishuhudia ongezeko la maambukizi ya homa ya nyani.
Shirika la USAID limepunguza msaada wake, jambo ambalo limeathiri juhudi za kukusanya sampuli kwa ajili ya uchunguzi. Hata hivyo, WHO imefanikiwa kushawishi mataifa tajiri kama Ulaya na Japan kufadhili chanjo kwa nchi za Afrika.
Tangu mwaka jana, mataifa matano ya Afrika yameanza kutoa chanjo dhidi ya Mpox katika juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.
