Na Lookman Miraji

Asasi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya Misingi ya Jamii ya Kiraia (FCS) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mashirika ya kimataifa imetangaza ujio wa wiki ya azaki inayotarajiwa kufanyika jijini Arusha mapema mwezi Juni.

Wiki hiyo ya Azaki imekuwa ikiandaliwa kila mwaka ikiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kijamii na kimaendeleo. Kwa miaka ya hivi karibuni tukio hilo limeendelea kugusa watu wa makundi mbalimbali kukutana pamoja na kuangazia masuala ya kimaendeleo.

Ujio wa tukio hilo linalotarajiwa kufanyika kwa mara ya saba mwaka huu, umetangazwa katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na waandaji wakuu wa tukio hilo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya kijamii ya FCS (Foundation of Civil Society), Justice Rutenge ameeleza kuwa tukio hilo kwa mwaka huu linatarajia kuwakutanisha wadau wa maendeleo kutoka kila kona kujadili njia zitakazoweza kutumika katika kuyaelekea maendeleo.

Wiki hiyo ya Azaki itahusisha mijadala kuhusu masuala mengine ya kimaendeleo kama ,kujadili njia mbadala za kukuza wajasiriamali, majadiliano kuhusu demokrasia nchini pamoja kujadili kuhusu suala zima la ubia wa maendeleo.

“Wiki ya Azaki itajikita kujadili njia za kupita katika kuielekea dira ya taifa ya maendeleo. Tukio hilo litahusisha wadau wa maendeleo kutoka taasisi mbalimbali watakaokutana kushiriki mijadala mbalimbali.”

Nesia Mahenge akiwa kama mwenyekiti wa kamati ya azaki nchini na Mkurugenzi mkazi wa taasisi ya kimataifa iliyojikita kuimarisha mifumo ya maisha kwa jamii ya watu wenye ulemavu (CBM, Christian Blind Mission) , amesema kuwa kupitia tukio hilo, watu kutoka kila sekta watapata fursa za kujifunza kwa namna watakavyoweza kuchangia katika kupelekea maendeleo nchini.

“Tunashirikiana na serikali kwa karibu ili iweze kutuongoza vyema katika kujadili maendeleo nchini.” alisema.

Tukio hilo ambalo kwa mwaka huu limewezeshwa kwa ushirikiano mkubwa na taasisi nyingine mbalimbali zikiwemo za kifedha na za kijamii. Walipozungumza kwa niaba ya taasisi wanazoziongoza nao wameeleza kuhusu mchango wao katika tukio hilo kwa mwaka huu.

Doreen Dominic akiwa kama mkuu wa kitengo cha taasisi za umma wa mashirika binafsi kutoka benki ya Stanbic, amesema kuwa ushiriki wao katika tukio ni sehemu ya dhamira yao ya kuchochea maendeleo ya jamii.

Mbali na ushiriki huo benki hiyo pia itakuwa ikitoa elimu ya fedha kwa mtu mmoja mmoja, mashirika na wajasiriamali katika wiki nzima ya azaki kwa lengo la kuongeza maarifa na kuboresha maamuzi ya kifedha.

“Stanbic bank Tanzania ni mdhamini rasmi wa wiki ya azaki kwa mwaka 2025 kwa mchango wa shilingi milioni 40, kama sehemu yetu ya kuchochea maendeleo ya jamii kwa ushirikiano wa kweli” alisema.

Aidha nae Ismail Biro, akiwa kama Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Tanzania bora, ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kuthibitisha ushiriki wao katika wiki hiyo ya Azaki.

Maadhimisho ya wiki ya Azaki yanatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 2 mpaka Juni 6 mwaka huu jijini Arusha.