Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Bunge la bajeti likiwa linaendelea Jijini hapa,Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewasilisha ombi la bajeti ya shilingi bilioni 476.7 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2025/2026, lengo likiwa ni kuendeleza shughuli za sekta hizo muhimu nchini.

Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 101.5 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida huku shilingi bilioni 375.1 zikiwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo,Matumizi ya kawaida yanahusisha mishahara ya wafanyakazi (PE) ambayo ni shilingi bilioni 47.3 na matumizi mengineyo (OC) yenye jumla ya shilingi bilioni 54.3.

Katika fedha za maendeleo, Dkt. Kijaji amesema shilingi bilioni 228 zinatarajiwa kutoka ndani ya nchi, huku shilingi bilioni 147.1 zikitarajiwa kutoka kwa wahisani wa nje.

Wizara imesisitiza kuwa fedha hizo zitalenga kuboresha mifumo ya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya mifugo na uvuvi, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa masoko kwa wafugaji na wavuvi nchini.