Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Wizara ya Viwanda na Biashara imeomba kuidhinishiwa na Bunge kiasi cha shilingi bilioni 135.7 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya maendeleo na matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Hayo yamebainishwa leo Mei 14,2025 Jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jafo, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma.

Dkt. Jafo amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 93.9 zitatumika kwa matumizi ya kawaida, huku shilingi bilioni 41.8 zikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Amefafanua kuwa kati ya shilingi bilioni 93.9 za matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 75 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa wizara, na shilingi bilioni 18 zitatumika kwa matumizi mengineyo.

Aidha, kati ya shilingi bilioni 41.8 za matumizi ya maendeleo, shilingi bilioni 14 zinatarajiwa kutoka kwa wahisani wa maendeleo ikiwa ni fedha za nje.

Dkt. Jafo amebainisha kuwa bajeti hiyo inalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji wa viwanda, kukuza uzalishaji wa bidhaa za ndani, pamoja na kuimarisha mifumo ya biashara katika soko la ndani na nje ya nchi.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje.

Aidha, amesema mpango wa wizara hiyo pia unajumuisha kuendeleza maeneo maalum ya viwanda (industrial parks), kukuza matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji, pamoja na kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa njia ya mafunzo, mitaji na masoko. Alisisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda unaojumuisha watu wengi zaidi.