Tangu nilipozaliwa hadi leo, sijapata kujiridhisha kama kweli naweza kula kitu ambacho kimetengenezwa kwa kemikali na mbwembwe nyingine, lakini kikawa na afya na virutubisho vya kweli katika mwili wangu.
Sijawahi kufikiria kuwa naweza nikapata huduma mbalimbali kwa njia ya mkato bila kufanyiwa kazi au kufanya kazi, haya ni mawazo ya kwangu ambayo yanakita katika kichwa changu.


Maendeleo yanakuja na mengi, sisi watu wa zamani hatujui mambo mengi ya dotcom, leo unaweza kufanya kila kitu ndani ya chumba chako, utakula, utapata fedha, utaishi, utaiba, utastarehe, utafanya kazi na kadhalika. Haya ndiyo maisha ya dotcom, maisha ambayo yanakuja na maendeleo yake.
Leo nimesukumwa kuandika barua hii baada ya kuona kila kitu kinanipita mimi mtu wa S. L. P, mtu wa kungoja kila kitu kwa muda mrefu, mtu wa matumaini yanayochelewa, mtu wa subira yavuta heri, mtu mwenye taratibu lakini yenye maana na manufaa.


 Nimeamua kuandika barua baada ya kufanya fikra tunduizi na kubaini kuwa kila siku iendayo inakuja na makovu ya maendeleo na hasa katika nchi maskini zinazoendelea kama za Afrika. Nchi ambazo zimechukuliwa kuwa ni majalala ya majaribio kwa dawa, vyakula na bidhaa nyingine kwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Tanzania ni moja kati ya mataifa yaliyofungua milango ya kibiashara na mataifa mengine, na wakati ikifungua milango ni dhahiri bila hofu kuwa iliweka malengo na mipaka ya biashara hii huru kutoka nje, ndiyo maana baadhi ya bidhaa za ndani zilianza kupotea ama kutokana na gharama yake au ubora wake.
Naandika barua hii nikiwa ni mwenye simanzi kubwa huku nikijua kuwa kama kuna nchi ambayo imegeuzwa kuwa dampo la kutupa bidhaa feki ni Tanzania, hapa ndipo unapoweza kupata dawa za kutumia binadamu zilizopitwa na wakati, au dawa ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.


Hii ndiyo nchi ambayo unaweza kuona bidhaa zilizothibitishwa na vyombo vinavyohusika lakini ni feki na ikawa ipo sokoni kwa kipindi kirefu kabla haijatolewa ufafanuzi wa kuikataa wakati imekwishaleta madhara kwa binadamu au mazingira.
Hii ndiyo Tanzania ninayowiwa nayo leo kuisemea kwa madhara yake, nchi ambayo mipaka yake iko wazi kwa bidhaa na huduma zote kuingia bila kipingamizi ilhali tukijua kuwa zinadhuru afya zetu, utamaduni wetu, uchumi wetu na mazingira yetu.


Kwa takwimu ambazo tunaziona kwa macho na kusimuliwa na watu wengine, tunashuhudia jinsi ambavyo bidhaa nyingi feki na huduma feki zilivyozagaa katika Taifa letu, na wakati mwingine tunashindwa kuchukua hatua kwa kuwa kuna vipengele vingi vya kulindana kisheria.
Kitu ambacho kinakera ni pale tunapoamini vyombo vyetu vya usalama katika kutulinda sisi, lakini vyombo hivyo vinageuka kuwa kisu kwetu, wanaotakiwa kudhibiti bidhaa kabla hazijaingia wanatakiwa kufanya hivyo, wanaotakiwa kuangalia dawa kabla hazijaanza kutumiwa wafanye hivyo hali kadhalika katika kila sekta kunatakiwa kuwa na chombo makini ambacho kinadhibiti bidhaa na huduma feki.


Leo nazungumzia juu ya bidhaa feki na soko huru la kuuza bidhaa hizo hapa nchini. Tumesikia juu ya mayai, vipodozi, televisheni, simu, dawa, vyakula mbalimbali, mafuta na kadhalika. Zipo bidhaa ambazo athari yake huonekana moja kwa moja, lakini zipo bidhaa au huduma ambazo madhara yake hayapatikani na kuonekana moja kwa moja.


Leo nasikia kuna mayai ambayo yanachanganywa kemikali tu na yanapelekwa kwa watumiaji; kuna vyakula ambavyo ni sumu na vinaliwa na watu wote bila kujali kama vipo katika viwango vinavyokubalika kiafya; kuna huduma ambazo zinatolewa lakini huduma hizo hazina viwango ambavyo tumethibitishiwa kuwa ni halali kwa mahitaji ya Mtanzania.


Wazo langu; tujaribu kurejea Tanganyika kwa utaratibu wake uliokuwa na faida ya afya. Tanganyika ya kujiridhisha kwa bidhaa na huduma, Tanganyika ya kuadhibiana kwa makosa ya kijinga, Tanganyika ya ulinzi wa wote, Tanganyika ya kutokubali rushwa.
Yapo mengi sana katika biashara ya soko huru na hasa katika Taifa letu, cha msingi tukatae kuwa dampo la bidhaa feki, tukatae rushwa kwa ajili ya wanaotaka kunufaika na bidhaa na huduma hizo.

Wasaalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.

By Jamhuri