Kama kuna kitu kinanikera ni hii tabia ya mtu kukurupuka kutoka nyumbani kwake na kuita watu wachache wanaomjua na aliowanunua wa mtaani kwake, na kutangaza nia ya kuomba ridhaa ya wananchi kuwa kiongozi wao.
Kuna watu nadhani huwa hawajiangalii hata katika kioo achilia mbali kuuliza watu wenye akili kama wanatosha wanachotaka kufanya, au wataonekana vioja kwa hicho cha kutaka kutangaza nia ya kugombea kiti cha udiwani, ubunge na hata kile cheo kikubwa.
Kuna watu wanajijua dhahiri kuwa hawafai na dunia nzima inajua hawafai, lakini bila haya  wanakurupuka kutoka watokako na kuja kudai kuwa wana wito wa uongozi na wanataka kutukomboa kutoka  hapa tulipo kwa umaskini tulionao.


Kuna watu bado wana akili ndogo ya kuamini kuwa wanafahamika na watu wengi kwa hiyo kwa kufahamika huko wanaamini wanaweza wakapata ridhaa ya wanaowafahamu na kupita katika uchaguzi. Kwa hili silikatai la kupita kwa sababu hata wanaowachagua ni wenzao kwa maana ya uelewa wa mambo.
Inasikitisha sana unapoona mchezaji mpira, tena aliyemaliza vibaya darasa la saba na kwa kuwa ana mashabiki wenzake wa mpira ambao uwezo wao wa akili uko sawasawa, wanaamua kumuunga mkono kwa jambo ambalo yeye amekurupuka nalo.
Kibaya zaidi unamuona mtu mzima uliyedhani  mwenye akili timamu anamuunga mkono, hapa ndipo ninapokumbuka maneno ya Julius kwamba mtu huyo hatufai aende akasimamie mashamba yake lakini kwa uongozi hatufai kabisa.


Hivi sasa kuna wimbi la watu wa kaliba mbalimbali za vichekesho, wasanii, wapiga debe na kadhalika ambao wameonesha nia ya uongozi, lakini sijui wametumwa na nani na kama ni akili zao au siyo zao!
Kwa jinsi ninavyofahamu mimi uongozi ni karama, uongozi ni kipaji, uongozi ni wito, uongozi ni kuombwa siyo kuomba, uongozi siyo kuongoza familia au marafiki zako ni kuongoza jamii yote, uongozi si suala binafsi ni suala la jamii inayokuzunguka.
Leo nimeamua kusema wazi kuwa ikiwa tunataka mabadiliko ya kweli ni vema sisi wapiga kura na sisi tunaotangaza nia kujipima tunataka nini kwa Taifa letu, lakini pia vyama vinatakiwa viwe makini na wanaotaka kuwasimamisha katika chaguzi hizo kama lengo lao litakuwa kuleta idadi kubwa ya viongozi wasioweza itakuwa na tija kwa maendeleo.


Napenda moyo wa kujiamini na kujituma lakini pia kujiamini lazima kuwe sanjari na uwezo wa uongozi, kiongozi ni kioo cha jamii anayoiongoza, kiongozi anatakiwa kutoa uamuzi mzito kwa ajili ya mustakabali wa jamii yake, kiongozi anatakiwa kuyajua matatizo ya wananchi pasi na kuelezwa.
Siku za hivi karibuni tumeshuhudia jinsi ambavyo baadhi ya viongozi ambao tuliwapa dhamana ya kutuongoza wanavyopoteza muda kusutana wao binafsi badala ya kuzungumzia masuala ya kitaifa, tumeshuhudia ushabiki ukifanyika katika mambo makini  na ya msingi kwetu na badala yake baadhi ya viongozi wasio na wito wanaingiza utani.


Ni kweli kwamba kuna haki ya kupiga kura na kupigiwa kura, kuna haki ya kuwa kiongozi na kuwa mtawaliwa, lakini pia ni lazima tukubali kuwa tuna haki ya kuwa na kiongozi makini kwa faida yetu sote, kila mtu afanye kile ambacho anadhani anaweza kukifanya vizuri.
Hali tuliyofikia sasa ya kila anayedhani anaweza kuwa kiongozi ni janga la kitaifa, haiwezekani tukapambanisha watu wa kaliba mbili tofauti katika uwanja wa siasa, wanasoka wacheze mpira, wasanii wafanye usanii, wapigadebe waendeleze debe lao na viongozi makini ndiyo tunaowahitaji na siyo kujulikana kwa mtu.
Ni vema pia tukajua wazi kuwa kujulikana kuna namna nyingi, mtu anaweza akajulikana kwa upumbavu wake, ujinga wake, ufedhuli wake, uvivu wake, ulevi wake, umaskini wake, uongo wake, uzuri wa sura yake, ulafi wake, elimu yake, utajiri wake lakini kwa uongozi hatufai.
Ni vema pia wanaofanya  uteuzi wakalijua hili. Taifa linaangamia kwa staili ya kipekee, kuwa na mambumbumbu katika sekta ya uongozi ni kulikaribisha Taifa kuwa maskini zaidi. Viongozi ndiyo wanaotunga sheria, viongozi ndiyo kioo cha jamii, viongozi ndiyo baba na mama wa taifa, sasa Taifa letu linataka kuwakabidhi akina nani hivi sasa.
Nimechukia sana.

Wasaalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.

 

By Jamhuri