Kuna msomaji wangu mmoja wa safu hii wiki jana alinipigia simu na kunisimulia hadithi moja nzuri, alianza kwa kujinasibu kuwa umri wake hauna tofauti sana na wangu japokuwa hakusema ana miaka mingapi.

Anasema zamani kabla ya kuanza kushuhudia soka la Ulaya kupitia runinga, aligundua kuwa sheria nyingi sana za soka zilikuwa zikipindishwa na kukosewa na pengine hata kutofuatwa kwa sababu nasi tulikuwa na sheria zetu za soka la kikoloni.

Niliipenda hii hadithi kwa sababu nyingi; kwanza inanihusu, pili nimeshuhudia mitanange ya namna hiyo kiasi cha kutosha, nimeshuhudia soka la mwanzoni mwa miaka ya 1970, kwamba mpira ni sehemu ya vita baina ya kijiji na kijiji, mpira ni sehemu ya amani baina ya kijiji na kijiji.

Kuna raha ya kufuata sheria na karaha ya kutofuata sheria, raha ya kufuata sheria ni kwamba pande zote mbili zinaridhia, wanaridhia wachezaji na pia mashabiki nao wanaridhia hali kadhalika mwamuzi hana lawama na anafarijika na kazi aliyofanya kwa kuwa kila mtu anawapongeza.

Enzi zetu tukicheza soka la kikoloni kulikuwa na sheria nyingi onevu na za kutafuta ushindi kwa maana ya lolote liwalo na liwe. Moja ya sheria ambazo zilikuwa zinanikera ni ile ya kila mchezaji kucheza namba ambayo ipo mgongoni, kama ni namba 5 maana yake wewe ni beki na ni lazima ucheze nafasi yako, vyovyote vile ukishika mpira hata kama ni katikati ya uwanja inayohusika hapo ni penalti.

Kipa hakuruhusiwa kucheza mpira na miguu, ilikuwa kama ana ahadi na kucheza na mikono tu, hata ikiwa katikati ya uwanja ni ruksa kudaka lakini kupiga mbele ni shurti arudi golini kwake, hizo ni sheria zilizokuwa wazi hazihitaji majadiliano na mabadiliko ya kujua kuwa tulikuwa tunafanya makosa yalianza miaka ya mwishoni mwa miaka ya 1970.

Miaka ile ilikuwa tunajua rasmi kwamba pambano hili la leo tunahitimisha kwa ndondi, na dalili zilikuwa wazi hata wiki moja kabla ya pambano, ulikuwa ni ujinga na ushamba wa kupeleka mwili katika kijiji kingine huku ukijua kuwa baada ya mpira kwisha kunaanza vita, vita ambayo hujui litatoka jicho au utavunjwa mguu.

Miaka ile tulikuwa wajinga kwa sababu tulikuwa tunajua kuwa lazima tushinde iwe tunacheza katika kijiji chetu au kijiji cha jirani, iwapo tunashindwa basi dakika za majeruhi lazima tuvunje pambano la mpira kwa kuanzisha vita.

Vita ile haina macho, unaokota jiwe na kulitupa katika halaiki bila kujua litamkuta nani, anaweza akawa babamkwe wako au mdogo wako, anaweza akawa adui au mpiganaji mwenzako, na hiki ndicho kinachoweza kutokea iwapo tutaamua kupitwa na wakati na kufuata sheria za mkoloni.

Kwanini leo nimezungumzia suala la kuzingatia sheria na kuheshimu matokeo, hivi sasa tunaelekea katika kipindi kizuri cha uchaguzi ambacho ni dhahiri lazima apatikane mshindi na wote tukubali matokeo, iwe kukubali kushindwa au kukubali lolote lile litakalotamkwa na msimamizi mkuu wa uchaguzi.

Kutokubali matokeo ni ishara kuwa hatujawiva kisiasa na tuko tayari kuivisha siasa kwa kumwaga  damu ya wapiga kura kwa manufaa ya wachache ambao wangelipenda wanufaike na matokeo ya kushinda, kutokubali matokeo ni ishara ya kucheza mpira wa siasa kwa kanuni za kizamani pasi na maendeleo ya kibinadamu.

Kutokubali matokeo ni dalili za kuamua kuingia katika mapambano ambayo tayari uamuzi umeupanga kwamba liwalo na liwe, umepanga kupata ambacho hakina ridhaa ya wengine bali wewe pekee kutokana na hisia zako.

Nimetoa mifano hiyo ya mechi za mchangani ambazo tulikuwa tukicheza huku tukijua hatima ya filimbi ya mwisho ya refa, ningelipenda nitoe tahadhari hata sasa tukiwa tunaelekea katika kipindi cha kupiga kura kwamba tusijiwekee malengo ya kuvutana baada ya matokeo kutangazwa, tusifikirie kuanza kutayarisha silaha kama zile za mpira wakati tukingoja matokeo.

Kutokubali matokeo ni ishara  tosha kwamba hufai kuingia katika kinyang’anyiro tena kwa kuwa ushiriki wako umeupanga kwa nia ya ushindi hata kama hukubaliki. Baada ya uchaguzi maisha yanaendelea na Taifa kama Tanzania litaendelea kuwapo na kuwapo kwetu kusiifanye Tanzania ya wanetu iharibike kwa tamaa zetu za madaraka ya leo.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu 

Kipatimo.

1303 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!