Sasa hivi najaribu kutafakari maisha baada ya awamu ya tano kushika dola ya nchi, ikiwa na mipango yake ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, chama ambacho kimekuwapo madarakani kwa miongo kadhaa ya utawala kama huu.

Kuanzia mwezi Julai mwaka jana yaani miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi, hali ilikuwa tete sana kwa wanaogombea nafasi mbalimbali ikiwamo ya urais. Wapo walioenguka kutoka CCM wakidai mfumo ni uleule na viongozi ni walewale, wapo wengi tu walioondoka kwenda kujiunga na wengine ili kuondoa mfumo uliosemwa mbovu.

Tangu ulipoingia madarakani Magufuli umebadilika, siyo wewe tuliyekuwa tunakujua kama mwenzetu kutoka Chato, mwenzetu mwanaCCM, mwenzetu mzee wa mfumo, mwenzetu usiyetaka mabadiliko, mwenzetu wa kulindana, mwenzetu wa kubebana, mwenzetu wa yaleyale, mwenzetu wa kuzembea, mwenzetu wa kuvumila, mwenzetu wa…na kadhalika. Kwa kubadilika huko nahisi umelogwa.

Ulikuwa mwenzetu hata kabla ya kuapishwa pamoja na maneno yako yote ya kampeni, tulijua wewe ni mwenzetu, mzee wa ‘kuzungusha’ mara hamsini, tulijua ni mwenzetu wa gwanda letu la kijani na kwamba tulijua wale wa kusoma namba wataisoma lakini siyo sisi.

Baada ya kuapishwa tu, tulishangaa mwenzetu uliposema wewe ni Rais wa awote, yaani hata wale ambao hawakukuchagua, tulishangaa kuona unasema wewe unatuongoza nchi nzima na siyo sisi wenzako wa ile CCM yetu ya tangu enzi na enzi.

Tukashangaa uliposema chama na maendeleo ya nchi ni vitu viwili tofauti, tukashangaa uliposema sasa yatosha masuala ya uzembe kwa sisi wanaCCM wenzako ambao tulizoea yale mambo ambayo hata wewe unayajua, ya kujuana, kubebana, kulindana, kuchukuliana yaani ndiyo sisi sisi.

Tukashangaa tulipoona mabadiliko yanazidi kuliko yale ya wenzetu waliokuwa wakinadi mabadiliko, hata wao wakalalamika unaiba sera zao, yaani walitaka uwe mzembe kidogo wapate cha kuongea na kuingia nacho katika uchaguzi ujao wa ngazi hiyo na nyingine.

Tukashangaa sisi wenye chama tuliokuwa tunafanya mambo kwa mazoea tunakumbwa na mabadiliko makubwa zaidi kuliko wale walioko nje ya chama, tukashangaa mfumo wa ndani ya chama unaanza kubomoka kwa kuchongeana yale ya gizani ambayo wengine ndani ya chama tulikuwa hatujui.

Tukashangaa Serikali yetu ikaanza kuwajibika pasi na mazoea yetu, wale ambao tuliwaweka kwa maslahi yetu wakawa wakali kwetu tena, wakakataa kusikia amri zetu na kudai kuwa wanataka kuwatumikia wananchi na siyo sisi tuliowapa madaraka kwa faida yetu.

Tukashangaa kuona uwajibikaji wa Serikali mpya ukiwa tofauti na zamani, Serikali inafanya kazi kama kwa Mhindi au kampuni binafsi, hayo hayakuwa mazoea yetu, nadhani hata wewe unajua. Swali tulilobaki nalo ni je, umelogwa na nani hadi umesahau mtindo wetu wa maisha?

Sasa hivi hakuna huyu mwenzetu kama zamani, hakuna konakona ambazo tulikuwa tunaishi kwa mtindo wa udalali unataka tukalime au kufanya kazi, unataka vijana wafanye kazi na wazee wafanye kazi, unataka kila mtu afanye kazi, unataka tulipe kodi, unataka Serikali yako iwajibike kwa wananchi, nani aliyekutuma Ikulu kufanya mabadiliko ambayo sisi hatukuwa tayari? Nani kakuloga?

Leo naandika barua hii kwa kuwa umeingilia sera za vyama vingine, nasikia aliyekuloga amekuloga ugonjwa uitwao mabadiliko ya vitendo, hakukuloga mabadiliko ya mdomoni, aliyekuloga amekutoa kwenye mfumo uliokuwa unawatesa Watanzania. Nani amekuloga? Nataka uwapeleke na wasaidizi wako nao wakalogwe.

Aliyekuloga amewasaidia Watanzania, aliyekuloga tunapenda afe ili asije akakupa dawa ya kukurudisha kwenye maisha yale ya kubebana, aliyekuloga kama hakulipwa, Watanzania wako radhi kumlipa. Ndiyo maana sasa hata kelele za kule mabadiliko wamekosa ajenda wanajadili mishahara na marupurupu yako.

Ndiyo maana wapigakura wanajiuliza unapaswa kugombea tena mwaka 2020 kwa kuzunguka nchi nzima au unadi sera zako kwa kutumia televisheni siku ya mwisho tu! Naamini ombi lao la mganga kufa linaweza kutimia.

Mheshimiwa Rais, kazi kubwa umeshafanya ya kuonesha wewe uko upande gani na huna ile ajenda ya walewale na mfumo uleule, kweli tunabadilika lakini cha moto tunakiona na namba tunaisoma vizuri bila mbwembwe. Narudia, kama kuna mtu kakuloga ubadilike basi mtu huyo afe asije akakuzindua, kama hakulipwa aseme Watanzania watamlipa.

Tanzania mpya naiona, tutaheshimiana, tutaendelea, tutakula matunda ya uhuru, tutaishi kama wenzetu walioanza kuishi, aluta kontinua, pambana, hapana angalia mtu usoni wala madaraka yake, rangi yake, dini yake au umri wake.

 

Wassalaam 

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1985 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!