Nimeamua kuandika waraka huu maalum kwenu kizazi cha dotcom, kwa lengo la kutaka kuwakumbusha sisi tulifanya nini katika kuhakikisha nchi hii inafika tulikokuwa tunataka kabla ya ninyi kuamua kulivunja Azimio la Arusha.

Leo ni siku maalum ya kumkumbuka ya shujaa wa uzalendo na si siku ya kumkumbuka ya mwasisi wa Taifa hili, mimi kamwe sikubaliani na sifa anazopewa Julius kama mwasisi wa Taifa, nakubaliana na sifa kubwa zaidi ya uzalendo wa kujitolea nafsi yake kwa Taifa la Watanzania maskini.

Julius ninayemfahamu mimi alikuwa shujaa wa kujali watu wengine maskini na si matajiri, alikuwa na muda mzuri wa kukaa na maskini zaidi na si matajiri, alikuwa na wageni maskini na marafiki maskini. Kwa bahati mbaya sana marafiki zake wote waliobakia hai wakiwa na itikadi ya Azimio la Arusha bado ni maskini!

Leo tunawaona viongozi wengi wa taasisi za umma, Serikali, vyama vya wafanyakazi, vyama vya kujitolea, na kadhalika wakimiliki ukwasi usiosemeka miongoni mwa Watanzania maskini wa kutupwa, na tukihubiriwa uwezekano wa kuishi maisha ya asali na maziwa katika kipindi kijacho kirefu. Hizo ni ahadi ambazo kamwe hazitawezekana, ni hadithi za Alinacha, tunawekeza katika matabaka ya walionacho na wasionacho.

Leo nawaandikia barua hii kuwaelezea Julius ninayemfahamu mimi alikuwaje. Ni Julius aliyeongoza Taifa hili kwa robo karne, Taifa lililokuwa na utajiri wa kila kitu duniani, lakini hakutaka kuufanya utajiri huo kuwa mali yake ama ya viongozi wenzake isipokuwa ni mali ya Watanzania. Alikuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote la kujineemesha yeye na familia yake kutokana na akili zetu na uchanga wetu wa Taifa.

Hakuwa tayari kuona tunatumia rasilimali ya Taifa kwa manufaa ya watu wachache kama ilivyo kwenu enyi dotcom, na mkiamini kuwa hayo ndiyo maendeleo. Maendeleo yenu ni kumiliki mahekalu, magari ya kifahari, mashamba makubwa, vitegauchumi vya Taifa, mali za umma na kuwa na hisa kwa watu wachache wateule kwa maana ya vigezo vya ubinafsi.

Nasikitika kumpoteza Julius, Julius ambaye hakupata kumiliki nyumba ambayo angeweza kusimama mbele ya Watanzania na kusema kajenga yeye binafsi kwa mshahara wake, au akajitapa kuwa aliweza kununua gari lake binafsi kwa mshahara wake na hata baiskeli zote mbili hakupata kununua kwa fedha zake.

Baskeli ya kwanza alinunuliwa na wazee wa TANU Mkoa wa Dar es Salaam na ya pili alipewa zawadi katika uzinduzi wa kiwanda chetu cha baiskeli hapa nchini. Aliishi Butiama katika nyumba aliyojengewa na TANU, kisha akakopa fedha THB na kuanza kujenga Msasani, almanusra ashindwe kumaliza kulipa deni, akasaidiwa na Serikali, akajengewa nyumba ya tembo na jeshi letu na mauti yakamfika.

Maskini Julius kwa uzalendo wake kifo kikamuumbua, ikajulikana kuwa alikuwa na pea nane tu za viatu, hakuwa na fedha nyingi katika akaunti za benki na alishindwa kununua hisa hata zile za CRDB.

Huyu ndiye Julius ninayemfahamu mimi na siri zake za umaskini zaidi nazijua. Hivi leo ni nani maskini kati ya hao walioko madarakani?

Shujaa wangu mzalendo wa kweli umeacha historia ya kukalia utajiri kwa ajili yetu, lakini sisi  tunautapanya, leo mimi lofa mwenzio nakukumbuka na kujuta tungetumia nafasi kama hawa, wao wangejuta kuwa maskini, sasa tunajuta sisi.

PUMZIKA KWA AMANI MZALENDO WA DHATI, MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE.

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.


By Jamhuri