Yah: Siasa isiwepo kila mahali

Kuna siku moja katika waraka wangu huu niliwahi kuonya juu ya mambo ya kitaalamu kuwaachia wataalamu wayafanye, wale ambao ni wanasiasa wajitahidi kutembea katika nafasi yao ya kupambana na masilahi na uwezeshaji wa kupanga vipaumbele kutokana na umuhimu.

Kuna mambo mengi ambayo huwa nawaza inakuwaje siasa iingie katika masuala ambayo kimsingi siasa haiwezi kutoa matunda ya moja kwa moja bila kutumia utaalamu na uwezo wa rasilimali tulizonazo, nafasi ya siasa ni katika kutuweka kuwa kitu kimoja na kutuwezesha kujenga ari ya kupata mafanikio katika amani na mshikamano, mpaka leo bado sijapata maana halisi na ya kisayansi juu ya maana ya siasa.

Mataifa makubwa duniani yanatumia siasa kama mlengo wa kutekeleza mipango yao ya kimaendeleo, iwe katika afya au elimu, iwe katika ulinzi wao au amani yao, nadhani hata sisi tunafuata mazingira hayohayo ya kupita ili tufike huko, na ndiyo maana dalili za kuanza kutumia wataalamu katika mambo ya kitaalamu zinaonekana kila iitwayo leo kwa serikali yetu.

Lakini pamoja na hayo bado kuna viongozi wa kisiasa au kitaaluma ambao wanaleta upofu katika masuala ya  utekelezaji wa mapambano ya kimaendeleo kupitia mfumo wa utendaji, kama kuna mwanasiasa ambaye anajua kwamba yeye ni mwanasiasa na  wajibu wake ni kutuunganisha na kutusukuma tukiwa wamoja kutekeleza masuala ya kitaalamu akaamua kwa makusudi kuvaa utaalamu, atakuwa hajatutendea haki ya kitaaluma katika uamuzi wake.

Dunia ya sasa ni tofauti kabisa na dunia ile tuliyoishi sisi tukiwa vijana na tukijiwekea malengo ya miaka kumi mbele, dunia ya sasa inahitaji watu ambao wanaangalia malengo ya miaka mia mbele lakini wakizingatia changamoto za dakika tano mbele, ni dunia ya mchakamchaka wa akili na kutatua changamoto zinazokuja kwa kasi ya ajabu kwa maendeleo ya watu wengine.

Nilikusudia kujadili mambo mengi ya mfano lakini si vibaya nikatoa mifano michache ya kawaida kabisa kwa uelewa wetu, tunapowakaribisha wawekezaji ambao wanakuja na teknolojia na mtaji wao ni kipi bora kwa wakati huo, kuna mikataba na umiliki wa teknolojia na mtaji wao, katika mazingira kama hayo ni vizuri wanaotuunganisha kama wamoja wakakaa pembeni na kuwaachia wataalamu wa sheria na uwekezaji wakafanya uamuzi sahihi kwa taifa lao na kuwaeleza wanasiasa hatima ya jambo hilo ili waliseme kisiasa kwa faida ya wananchi.

Haipendezi kuwaona wanasiasa wakijihusisha na masuala ya kitaaluma na kisha kugeuza utaalamu kuwa siasa, haipendezi wanataaluma kuwadanganya wanasiasa ili kuliingiza taifa katika hasara ya kutufanya tusiwe wamoja, nafasi ya kila mtu kufanya anachokijua kwa manufaa ya taifa letu ndio msingi mkubwa wa uzalendo tunaopaswa kusimama nao.

Watanzania tumeonekana tukikerwa sana na siasa katika mambo ambayo hayahitaji kufanyiwa siasa, lakini pia tumeona viongozi wengi wa serikali wakipinga kuleta siasa katika mambo yahusuyo taaluma na matokeo yake kumekuwa na msigino mkubwa wa kiuamuzi na kutuchanganya wananchi.

Ningefurahi zaidi kuwaona wanasiasa wakiparuana katika hoja baada ya kupewa dondoo za kitaalamu na wataalamu wao wapange vipaumbele, ningefurahi sana kuwaona wananchi wakichangia mjadala kama sehemu ya siasa yao katika kujadili hoja za kisiasa ili wataalamu waweze kuchanganua na kupambanua vipaumbele kwa wakati huo.

Ni jambo la heri kwamba taifa letu halina mjadala wa kujadili hatima ya amani na mshikamano tulionao lakini pia ni kweli kwamba tukiacha malumbano ya wanasiasa na wataalamu yakatamalaki ni kama tutakuwa tunaanza kutafuta chokochoko za kupoteza amani tuliyonayo.

Huu ni wakati pekee ambao tunatakiwa kuwaangalia walioendelea wamefanya nini hadi kufikia hapo, sina hakika kama wamefika hapo kwa kufanya siasa katika mambo ya kitaalamu, lakini pia sina hakika kama wamepata maendeleo bila kuwa na siasa madhubuti katika nchi zao.

Huu ni wakati wa kuacha majungu na fitina, ukandamizaji na kutafuta vyeo kwa nguvu, ni wakati wa kuangalia nani anaweza kufanya nini kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu, ni wakati wa kuinua wenye vipaji na kuwajengea mazingira mazuri ya uwezeshaji, hapo ndipo safari ya kuelekea uchumi wa kati utakapowadia.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.