Yawezekana kadiri miaka inavyozidi kwenda, itafika wakati nitashindwa kushika kalamu na kuandika barua kama nifanyavyo sasa.

 

 

Hata hivyo kwa faida ya kuacha kumbukumbu kwa kizazi chenu, nafikiria kutafuta eneo zuri na kubwa ili niweze kukaa katika kigoda na kutoa hadithi ambayo mwenye masikio na kalamu anaweza akaandika kwa niaba yangu.

 

 

Huwa nafikiria mambo mengi sana, inawezekana inatokana na kutokuwa na kazi au kuwa na uchungu na nchi yetu. Hii inatokana na vile sisi tulivyoishi, na nyie kizazi kipya mnavyoishi kwa manufaa yenu binafsi au ya kizazi kijacho.

 

Huwa nafikiria Tanzania yenyewe ilivyokuwa yapendeza wakati wa ujana wetu na Tanzania yenu ambayo sijui niite yapendeza pia kwa kizazi chenu, au la! Nasema hivi nikiwa na mambo ambayo yanakinzana na ukweli wa kukubali kuwa sasa yapendeza.

 

Naikumbuka Tanzania ya kijani kibichi katika kila kitu kama kilimo na uoto wake, madini, akiba ya serikali, mapato ya serikali, huduma za jamii, viwanda na uzalishaji, usalama wa taifa na ukombozi wa nchi za Afrika. Siikumbuki Tanzania katika ukijani wake katika uzazi wa mpango.

 

Tanzania ninayoijua mimi ni ile Tanzania ya kufanya kazi na kwamba Siasa ni Kilimo, Tanzania yenye miliki kubwa ya viwanda vya uzalishaji wa bidhaa zetu wenyewe na Tanzania ambayo haikuwa ikiagiza zaidi bidhaa kutoka nje, bali Tanzania ambayo ilikuwa ikiuza zaidi nje bidhaa zake tofauti kabisa na leo.

 

Wanangu, nimeanza na usuli huu kwa sababu niliwahi kuandika siku za nyuma nikijaribu kuwakumbusha ukweli wa Tanzania ile ambayo mimi huwa hainitoki kichwani. Hivi leo naona kama niko katika jehanamu ambayo sijui nitatoka lini!

Wanangu, naandika barua hii nikiwa na kumbukumbu nzuri ya uwakilishi wa bungeni, tena wakati huo Bunge likiwa pale Karimjee hapo Dar es Salam; Bunge lililokuwa la chama kimoja, lakini likitenda kazi kwa niaba ya Tanzania yote na ukubwa wake.

 

Ni Tanzania iliyokuwa na majimbo machache sana yawezekana robo ya majimbo ya sasa yaliyotokana na kigezo cha idadi ya watu, na si ukubwa wa eneo la kutumikia kama ilivyokuwa enzi zetu. Wanangu, bado nakumbuka usiri wa taarifa za vikao vya Bunge tofauti na sasa ambako mambo yapo “live” runingani.

 

Wanangu, muungwana hatakiwi kutukana, lakini ashakumu si matusi nawakumbuka wabunge wetu wa enzi hizo na ulofa waliokuwa nao na majukumu mazito waliyokuwa wakikabiliwa nayo katika kutimiza wajibu wao, sina hakika na posho kama walikuwa wakipewa chini ya Spika Chifu Adam Sapi.

 

Miaka hiyo niliwahi kupata lifti kutoka kwa ndugu mbunge (siku hizi mnawaita waheshimiwa) mmoja kutoka Njombe hadi Iringa. Mbunge yule alikuwa akijua kuwa mimi ni mpigakura wake, lakini alinitoa Njombe hadi Iringa pasi na kunipa hela hata chakula cha njiani hakununua. Wakati ule sehemu maarufu kwa chakula njia ile ilikuwa Malangali katika Hoteli ya Zimbabwe.

 

Siwezi kuisahau Hoteli ya Zimbabwe katika maisha yangu. Ina historia ndefu katika kichwa changu. Kwanza tulikuwa tukishushwa hapo na mabasi ya Relwe ili basi liweze kupeleka barua za posta Shule ya Sekondari Malangali.

 

Jambo hilo halikuzingatia kipeto kilichofungwa kilikuwa na barua ngapi, yawezekana hata barua moja ilikuwa ikipelekwa.

Haya ndiyo maisha ya Ujamaa na Kujitegemea yanayokiumiza sana kichwa changu ninapoangalia mfumo wa kufikisha huduma za jamii hata pale palipokuwa labda hapahitaji kufanyiwa hivyo – kwa lugha nyingine nakumbuka wimbo wetu wa Mwenge kwamba utapeleka matumaini pale yalipopotea.

 

Ile Tanzania yetu yapendeza iko wapi siku hizi? Tanzania yenye wabunge mia tatu na ushei, Tanzania yenye wasomi waliobobea, Tanzania yenye miundombinu inayoitwa ya kisasa, Tanzania yenye demokrasia iliyopitiliza kiasi cha wenye nchi yaani kizazi cha “dotcom” kuamua kuweka mawazo yao halisi hata kama ni matusi.

 

Wanangu, nawaandikia barua hii nikiwa na kumbukumbu nyingi za uzalendo na moyo wa kujitolea. Nawaandikia fikra za kizamani juu ya moyo tuliokuwa nao, nawaandikia nikikumbuka mambo tuliyoifanyia nchi hii bila kudai posho au nyongeza ya mishahara, nawaandikia nikikumbuka tulivyoamua kukatwa mishahara ili kuendeleza huduma za jamii nchini na mwisho tulivyojitolea katika Vita ya Kagera.

 

Wanangu, wiki jana kumetokea tafrani ya daktari mmoja kutekwa na kufanyiwa unyama, kwa madai kwamba inatokana na kudai nyongeza ya mishahara na kuboreshwa kwa huduma za afya. Inasemwa kutekwa kwake kunahusishwa na mgomo uliopo wa madaktari nchini.

 

Inanipa tabu sana kuona haya mabadiliko ya kiutendaji yalivyo, kama vyovyote na iwavyo jambo hili linatokana na migomo ya madaktari, basi wanangu tuendako kuna ukomo mbaya; ukomo utakaotupeleka katika migongano ya Kimagharibi ambayo hatukuzowea na hatukuitarajia.

 

Sitaki kupingana na hoja zilizopo sasa za madaktari na wala wanasiasa kwa sababu sisi hatukulelewa hivyo na chama cha TANU, bali waliopo ni nyie wa Chama Cha Mapinduzi na mustakabali wa posho au mishahara minono bila kuangalia vipaumbele vya taifa letu.

 

Siku za hivi karibuni Rais alikataa nyongeza ya posho za wabunge, walimu wakadai nyongeza za mishahara baada ya kuona mchanganuo wa posho za zamani za waheshimiwa wabunge, hali kadhalika madaktari nao wakaja juu wakitaka huduma za afya ziboreshwe na wapewe posho zao za kufanya kazi katika mazingira magumu.

 

Kwa mtazamo wangu wa kizee yawezekana wote wako sahihi katika madai yao – iwe wabunge, walimu, madaktari na kada nyingine ambazo ziko njiani katika kuandaa rasimu ya kuifikisha serikalini ili watangaze mgogoro na serikali wa kudai nyongeza ya mapesa.

 

Mzee Zuzu napata tabu sana kuafikiana na haya maendeleo ya ‘fedha mbele’ badala ya kujitolea; moyo tuliokuwa nao wakati wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na kwamba fedha si msingi wa maendeleo, bali ni matokeo ya kazi kwa sababu nchi hii tulikubaliana kuwa ni ya wakulima na wafanyakazi.

 

Sasa nchi yenu mmeigeuza kuwa ya wafanyabiashara na wafanyakazi. Wakulima mmewasahau. Kumbukeni kuwa hawa hawafikirii kugoma wakaamua kulima chakula chao tu na familia zao itakuwaje au wakiamua kula mbegu kabisa kieleweke huko majukwaani na maofisini kutakalika?

 

Mwenda tezi na omo marejeo ngamani. Jiulizeni kila mtu kwa kada yake akileta jeuri tutafika wapi? Kumbukeni sisi wazazi wenu katika mifumo yetu ya ujima na baadaye ujamaa kwa maana ya kujitegemea, tuliwezaje kukabiliana na hizi changamoto pasi na kumwaga damu?

 

Chonde chonde wanangu, mnaposikia Wahabeshi wanakufa katika mafuso ni ishara tosha ya kutwambia kuwa jeuri ya amani tuliyonayo ni ishara ya kumvuta shati Mwenyezi Mungu, kwamba na sisi tunataka siku moja tusafiri na mafuso huko Congo, Malawi, Zambia na kwingineko. Nyumbani patakuwa kituo cha polisi.

 

Wasalaam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

 

1196 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!