Iran inapanga kufanya misafara kadhaa ya maombi kwa ajili ya Rais Ebrahim Raisi na maafisa wengine waliofariki katika ajali ya helikopta.

Msafara wa kwanza umeanza leo saa 09:30 kwa saa za huko (06:00 GMT) katika jiji la kaskazini-magharibi la Tabriz.

Makamu wa Rais wa Masuala ya Utendaji Mohsen Mansouri alieleza katika mahojiano na IRINN kwamba mwili wa Raisi kisha utahamishwa hadi katika mji wa kidini wa Qom, ambako raia watakuwa na fursa ya kuuaga saa 16:30 kwa saa za huko (13:00 GMT).

Miili hiyo itapelekwa katika mji mkuu wa Tehran, Mansouri anasema, akiongeza kuwa ibada itafanyika huko siku ya Jumatano, huku Kiongozi Mkuu Khamenei akiongoza maombi ya jamaa kwa Raisi na wengine.

Jumatano pia imetangazwa kuwa siku ya mapumziko nchini Iran.

Kwa mujibu wa Mansouri, mwili wa Raisi baadaye utahamishwa Alhamisi asubuhi hadi Birjand, mji mkuu wa jimbo la Khorasan Kusini, ambako rais alikuwa amechaguliwa tena kuwa mwakilishi wa baraza la waangalizi wa uongozi Bunge la Wataalamu.

Ibada ya mazishi ya Raisi itafanyika katika mji wa kaskazini-mashariki wa Mashhad, katika makaburi ya Imamu wa nane wa Shia Reza siku ya Alhamisi jioni.