Ukienda mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam yalipo Makao Makuu ya Klabu ya Yanga utawakuta viongozi, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo hawana presha yoyote kuhusiana na mwenendo wa timu yao, wanakunywa tu kahawa.

Wanaamini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera,  ameiweka timu hiyo vizuri pamoja  na kushika usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kujikusanyia pointi 50, baada ya kucheza mechi 18 za mzunguko wa kwanza wa ligi bila kupoteza mechi yoyote zaidi ya kutoka sare mechi mbili dhidi ya Simba SC na Ndada FC.

Kimsingi Klabu ya Yanga inakabiliwa na ukata, hali inayosababisha kuomba michango kwa wapenzi na wanachama wa klabu hiyo ili iweze kusonga mbele.

Katika hii dunia Yanga SC inaweza kuwa klabu pekee licha ya ukata walionao lakini bado wanashika usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) na bila kupoteza mechi yoyote.

Bila kupepesa macho lazima tukubali Kocha Zahera anaiongoza vizuri Yanga kwa kuimarisha nidhamu ndani ya timu na wachezaji kuwa na mshikamano, kwa kuifanya klabu kuwa juu na mchezaji kuwa chini na kufuata maelekezo ya mwalimu.

Ukitaka kujua Zahera anapenda wachezaji wawe na nidhamu, angalia nyota wa timu hiyo, Ibrahim Ajibu, anavyodumisha nidhamu kwa sasa. Bila shaka ulikwishawahi kusikia kuhusu kilichomkuta kipa tegemeo wa timu hiyo, Beno Kakolanya, baada ya kuonyesha nidhamu mbovu.

Kulikuwa na maneno kwamba golikipa huyo alikuwa anayo madai yake kwa Klabu ya Yanga, akagoma kuungana na timu, lakini aliporudi Kocha Zahera alikataa kumpokea, kwani anaamini mchezaji kuigomea timu ni utovu wa nidhamu na mpaka leo anaisoma Yanga magazetini.

Wapenzi wa Yanga hawawezi kukasirishwa na hali hiyo kwa sababu kwa sasa timu inakabiliwa na ukata lakini kutokana na hali ya nidhamu inayosimamiwa na Kocha Zahera bado timu inapata matokeo mazuri katika mashindano yote ambayo inashiriki.

Bila shaka umesikia lilichomkuta aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Kelvin Yondani. Amevuliwa unahodha kwa kile kilichoelezwa na kocha wake kwamba amegomea mazoezi mara kadhaa na kuchelewa kwenda mazoezini bila kutoa taarifa yoyote kwa uongozi wa timu, kutokana na hali hiyo Ibrahim Ajibu ametangazwa kuwa nahodha mpya wa klabu hiyo.

Kocha Zahera ni muumini wa nidhamu, anaamini nidhamu ndiyo itaipa timu yake ubingwa. Mwaka uliopita aliwahi kunukuliwa akisema: “Ni bora nifungwe nikiwa na wachezaji wanaokuja na kuwahi katika mazoezi.”

Kutokana na nidhamu vijana kadhaa wameweza kujituma na kujihakikishia namba za kudumu katika kikosi cha kwanza cha  timu hiyo. Wachezaji hao ni Paul Godfrey, Ramadhani Kabwili na Abdallah Shaibu (Ninja).

Vilevile mshambuliaji wa timu hiyo, Heritier Makambo, amechaguliwa  kuwa mchezaji bora wa mwezi Desemba kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPL).

Ikumbukwe Ligi Kuu ya Tanzania Bara imesimama kutokana na mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea kufanyika Zanzibar. Timu za Yanga na Simba zimeshinda katika mechi zao za kwanza katika hatua ya makundi lakini Azam walitoka suluhu dhidi ya Jamhuri.

Please follow and like us:
Pin Share