Mwanamke mmoja kati ya watano, na mwanamume mmoja kati ya 10 wamewahi kupata sonona katika jamii zinazotuzunguka na kuleta matokeo hasi katika maisha yao. Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa wanawake ndio wahanga wakubwa wa janga hili.

‘Depression’ ni neno la kisayansi ambalo kwa tafsiri ya kawaida ndipo tunapoita sonona. Huu ni ugonjwa wa akili ambao mtu anaupata baada ya kupitia matatizo fulani na kumuacha kwenye huzuni au kusononeka kwa muda mrefu. Ila watu wengi bado hawajui kama hali hii nayo ni ugonjwa kama magonjwa mengine.

Pamoja na sababu zinazochangia, lakini kitu kingine muhimu unachopaswa kukitambua ni zipi dalili kuu za sonona? Ninapokuwa ninatathmini sonona nikiwa na mgonjwa, huwa namuuliza maswali haya; kwa kipindi cha siku chache zilizopita umeshawahi kupatwa na hali iliyokufanya ujione kama hauna thamani na kupoteza matumaini? Au unakosa hisia kwenye vitu ambavyo hapo awali vilikuwa vinakupa furaha?

Kama jibu la maswali haya linakuwa ni ‘ndiyo’, basi ni dhahiri una sonona. Dalili nyinginezo zinazopaswa kufuatiliwa ni kama vile kukosa hamu ya kula, kukosa usingizi wa kutosha (aidha kuchelewa kulala au hata kuwahi kuamka), kushindwa kutilia maanani katika mambo muhimu, kujiona kama hauna uwezo wa kufanya jambo fulani na kila unapopaswa kufanya jambo hilo unahisi uchovu, lakini pia  wakati mwingine mtu anashawishika kujinyonga.

Ni dhahiri kwamba sonona ni tishio la maisha, kutokana na ukweli kwamba unasababisha mtu kutofurahia maisha yake binafsi. Katika kufuatilia ni kwa kiasi gani mgonjwa ameweza kuathiriwa na sonona, madaktari huwa tunatumia njia ya mahojiano kati ya daktari na mgonjwa. Njia hii kitaalamu inajulikana kama PHQ-9 (Patient Health Questionnaire).

Kupitia njia hii, daktari anamuuliza mgonjwa maswali tisa maalumu ambayo majibu ya mgonjwa yataonyesha ni kwa kiasi gani  ameathiriwa na sonona kabla ya kumfanyia vipimo. Cha kusikitisha ni kwamba, waathirika wengi wa tatizo hili hawaendi kupata ushauri wa daktari kwa dhana ya kuona aibu au kuona kuwa sonona si tatizo la kulitilia maanani.

Sonona ni ugojwa kama magonjwa mengine ambayo yanahitaji msaada na yasipopatiwa tiba yanaweza kuleta madhara makubwa sana katika maisha ya kila siku.

Kwa mfano, kama una vidonda vya tumbo na umekuwa ukiyadharau maumivu yanayoambatana na vidonda hivyo bila kuyapatia tiba, ukingo wa utumbo mpana unakuwa hatarini zaidi kuathirika na kulazimika kufanyiwa upasuaji. Kwa sonona pia ipo hivyo hivyo.

Daktari huenda asikuambie: “Jizuie na sonona ina madhara” kama hautaonyesha kuhitaji msaada wa daktari. Sonona ni zaidi ya ufikiriavyo, inakufanya upoteze kabisa hisia na kushindwa kufurahia yale mambo yote ya kijamii ambayo kwa kawaida yanaleta furaha katika maisha ya kila siku.

Tiba

Ikiwa mgonjwa hajaathiriwa sana na sonona, ushauri wa kisaikolojia kwa mgonjwa namna ya kukabiliana na tatizo utamsaidia. Aidha, kwa mgonjwa ambaye ameathiriwa zaidi na tatizo hili, tiba ya dawa italazimika kutolewa kwake.

‘Antidepressants’ ni jina la kitaalamu ambalo linajumuisha makundi ya dawa za kutibu sonona. Hata hivyo, dawa hizi pia huwa zinaleta matokeo mengine baada ya kutumiwa kama zilivyo dawa za aina nyingine.

Matokeo kama uchovu, kuharisha au kukosa haja, mdomo kukauka ni baadhi tu ya matokeo ya kawaida mgonjwa anayoyapata baada ya kuzitumia dawa hizi, lakini matokeo haya yanatoweka baada ya siku chache.

Mgonjwa anapaswa kutumia dawa hizi kwa muda hata zaidi ya miezi sita na hatakiwi kuacha kutumia hata kama akianza kupata nafuu ili kupunguza uwezekano wa ugonjwa kujirudia.

Pia zingatia kuwa ukiwa na sonona ni rahisi sana kusikia hali ya uchovu na kukosa ari ya kufanya chochote, kwa hiyo unaweza kushindwa kufanya mazoezi ya viungo. Lakini mazoezi yanasaidia kusisimua vichocheo vinavyoleta hisia za kujisikia vizuri. Hivyo ni muhimu kujilazimisha kufanya mazoezi hata kama unahisi uchovu.

Please follow and like us:
Pin Share