Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe, yumo kwenye hatihati ya kurejea nchini kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuhofia maisha yake.

Kama hilo litafanyika, Zitto atakuwa amefuata nyayo za mwasiasa machachari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ambaye licha ya kupona majeraha ya risasi, amesita kurejea nchini kwa kuhofia maisha yake.

Lakini Zitto, licha ya kuhofia uhai wake, anadai kuwa ameng’amua mpango wa vyombo vya dola wa kumfungulia kesi ya utakatishaji fedha ambayo haina dhamana, hivyo kumfanya atupwe rumande kwa muda usiojulikana. 

Katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VOA) wiki iliyopita, Zitto alisema ana hofu kurejea nyumbani kutokana na vitisho alivyopata, ukiwamo ujumbe mfupi wa maandishi wa simu.

Anasema ujumbe huo ulipelekwa kwake siku moja baada ya Benki ya Dunia kuahirisha kwa muda mkopo wa dola milioni 500 za Marekani (zaidi ya Sh trilioni 1) kwa Serikali ya Tanzania.

“Labda usirudi, ukirudi tutakumaliza,” Zitto aliunukuu ujumbe huo kwenye mahojiano aliyofanya na mtangazaji wa VOA, Dk. Mwamoyo Hamza.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP David Misime, ameulizwa na JAMHURI iwapo wamechukua hatua kutokana na madai ya Zitto na kujibu kuwa si kawaida ya jeshi hilo kutangaza kila kazi inalofanya.

“Kwanza, ili Jeshi la Polisi lifanyie kazi tuhuma zozote inabidi mtu aliyeathirika aripoti kwanza, hapo ndipo tunaweza kuanza kufanya kazi.

“Pili, inabidi ufahamu na umma ufahamu kuwa si kila kitu kinachofanywa na Jeshi la Polisi kinatangazwa. Huo utaratibu wa kutangaza hadharani unaweza kuwa ni wa watu wengine, lakini sisi katika Jeshi la Polisi hatufanyi hivyo,” anasema.

Hata baada ya kuelezwa kuwa jeshi hilo lina wajibu wa kufuatilia mambo hata bila ya mtu kuripoti, Misime anasisitiza: “Sisi hatuendi na mawazo ya mtu anavyofikiri.” 

Chama cha ACT – Wazalendo kimeeleza kusikitishwa na kauli hiyo kwa kile kilichosema inaonyesha namna Jeshi la Polisi linavyokwepa wajibu wake.

“Ni wajibu wa Jeshi la Polisi kulinda maisha ya raia na mali zao. Vitisho hivi vimetolewa hadharani na kila mmoja amevisikia, inakuwaje wanataka mtu akaripoti jambo ambalo limesikiwa na kila mmoja?” anahoji mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho, Ismail Jussa na kuongeza:

“Inavyoonekena hapa Polisi wanataka kukwepa wajibu wao na hili ni jambo la kusikitisha sana.”

Jussa ameliambia JAMHURI kuwa ACT – Wazalendo wanaamini kuwa Zitto atarejea nchini licha ya vitisho hivyo kwa sababu “yeye ni kiongozi shupavu asiyeogopa mambo kama hayo.”

Kuhusu chama hicho kumlinda Zitto iwapo atarejea, Jussa alisema wao hawana uwezo wa kumpa mtu yeyote ulinzi wa maisha yake kwa kuwa dhima hiyo ni ya Jeshi la Polisi.

“Isipokuwa sisi tunaweza kumpa ulinzi kisiasa kwa sababu hiyo ndiyo kazi yetu na haitatushinda. Hatuwezi kushindwa kumlinda kiongozi wetu kisiasa,” anafafanua Jussa.

Anasema chama chao kimesikitishwa na vitisho anavyopata Zitto ambavyo ni ishara kuwa wapinzani wao wameshindwa kufanya siasa za kistaarabu.

“Hizi si siasa tunazozifahamu sisi. Siasa ni uwezo wa kuwashawishi watu kwa hoja, si kutisha wengine,” anasema.

Jussa anasema inasikitisha kuona nchi imefikia hatua ya kufanya siasa za kinyama kwa kumtishia mtu mwingine kwa sababu tu ana mawazo tofauti na wao.

“Wanaofanya hivi wakumbuke tu kuwa hakuna utawala duniani ambao ulidumu kwa kutisha watu, tawala zote za mabavu ziliondoka, hakuna iliyodumu.

“Vyombo vya dola wana dhima na wajibu wa kuhakikisha wote waliotoa vitisho wanachukuliwa hatua. Kama wakishindwa kufanya hivyo hilo ni kosa lao. Sisi kama chama cha siasa tutafanya yale ambayo yapo chini ya wajibu wetu,” anasema Jussa.

Akizungumza na VOA, Zitto anasema kutokana na mfululizo wa vitisho vilivyotolewa na viongozi na wanachama wa CCM, anahofu kurudi nchini kwa kuwa huenda akafunguliwa mashitaka, kufungwa au hata kuuawa.

Anasema anaichukulia kwa uzito hofu yake kwa kuwa upo mfano wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Lissu, kupigwa risasi jijini Dodoma mchana.

Lissu alikumbana na masaibu hayo baada ya kuwa amepokea vitisho kadhaa vya aina hiyo zikiwemo pia kauli kwamba wasaliti kwenye vita huwa wanauawa. Lissu ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema ni mkosoaji wa sera za Serikali ya Awamu ya Tano, hali iliyofanya aonekane kuwa msaliti.

Zitto anadai kupata taarifa kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeandaa mashitaka dhidi yake yanayohusu utakatishaji fedha. JAMHURI halikufanikiwa kumpata msemaji wa taasisi hiyo kuthibitisha au kukanusha madai hayo.

Wakati wa Mkutano wa Bunge wa 18 uliomalizika hivi karibuni jijini Dodoma, Spika Job Ndugai, alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi, kuangalia iwapo kitendo cha Zitto kuiandikia barua Benki ya Dunia kuzuia mkopo kinakwenda kinyume cha sheria za jinai, hasa ikizingatiwa kuwa alitumia nembo ya Bunge kwenye barua hiyo.

Ndugai alitoa mwito huo kwa Profesa Kilangi baada ya mjadala uliotokana na hoja binafsi iliyowasilishwa na Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel (CCM), aliyetaka Zitto achukuliwe hatua kwa kitendo hicho.

Kwenye mahojiano na VOA, Zitto alisema hajutii hata kidogo kutoa rai kwa Benki ya Dunia kusitisha mkopo huo kwa madai kuwa fedha hizo zingetumika kinyume cha makusudio ya awali, ikizingaiwa kuwa huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu.

Alisema mwaka 2018 Benki ya Dunia walizuia fedha kwa Tanzania na kuleta maofisa wao nchini kwa sababu kuu tatu ambazo ni Sheria ya Takwimu, matamshi ya viongozi kuhusiana na watu wanaotengwa; na kauli ya Rais John Magufuli kuzuia watoto waliopata ujauzito kurejea shuleni.

Zitto anasema misaada hiyo ilikuwa ya dola bilioni 1.5 (Sh trilioni 3.45). Baada ya serikali kuanza kutekeleza masharti ya Benki ya Dunia, fedha hizo zilianza kutolewa kwa awamu. Awamu ya kwanza ilikuwa Septemba, mwaka jana baada ya Sheria ya Takwimu kufanyiwa marekebisho.

“Awamu ya pili ilikuwa hizi za mkopo wa elimu na serikali ilikuwa imeiahidi Benki ya Dunia kwamba itaruhusu watoto ambao wamepata ujauzito warudi shuleni. Lakini ukisoma mkataba wa ule mkopo hakuna hiyo ruhusa isipokuwa wametengeneza kitu wanachoita alternative pathway, yaani njia mbadala, na hiyo njia mbadala ni kwamba waende wakasomee vitu kama kusuka, upishi, usafishaji na mambo kama haya. Sisi tunasema hapana. Mtoto wa kike ana haki ya kurudi shuleni kuendelea na masomo kutokana na chaguo lake mwenyewe,” anasema.

Kuhusu uhusiano wa fedha hizo na uchaguzi wa mwaka huu, Zitto anadai kuwa shule zinazopangwa kujengwa zitasemwa zimejengwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilhali ukweli ukiwa kwamba ni mkopo utakaolipwa na Watanzania wote. 

Pia anasema Benki ya Dunia kutoa fedha hizo kipindi hiki ni sawa na kuingilia mchakato wa Uchaguzi Mkuu na kuiunga mkono serikali iliyopo madarakani.

“Hoja ya msingi hapa ni kwamba una serikali ambayo inatumia matrilioni ya fedha kununua ndege ambazo zinatumiwa na asilimia moja tu ya wananchi, halafu inakwenda kukopa kwa ajili ya elimu… kama hii serikali ingekuwa inajali elimu isingehangaika na vitu vinavyotumiwa na asilimia moja tu ya watu, badala yake ingetumia hizo fedha zinazotokana na kodi za wananchi zingepelekwa kuhudumia elimu,” anasema Zitto.

1134 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!