Kiongozi Mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amewataka wasimamizi wa uchaguzi kutoingizwa kwenye mtego wa kuwatangaza washindi wagombea wa CCM hata kama watashindwa katika sanduku la kura la uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika siku ya Jumatano Novemba 27, 2024, kwani kufanya hivyo ni kukiuka misingi ya demokrasia na matakwa ya wananchi hivyo wanapaswa kutenda haki.

Zitto ametoa wito huo siku ya Jumanne Novemba 26, 2024 wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji 2024- 2029 uliofanyika katika uwanja wa Mwanga Community Centre uliopo katika kata ya Mwanga Kaskazini, Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.

“Tunataka uchaguzi wa amani, tunataka uchaguzi wa haki, tunautaka mji wetu, tuurudishe mji wetu, CCM wamekaa na mji wetu (Manispaa ya Kigoma Ujiji) kwenye mitaa miaka mitano, mitaa yetu haiendeshwi vizuri, mikutano mikuu ya mitaa haiitishwi, shughuli za mitaa hazifanyiki”, amesisitiza Zitto.

Amewataka watendaji wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kuacha kukikumbatia chama cha CCM kwani ni chama ambacho kimeshindwa kuwalinda watendaji wa manispaa na watendaji wa kata hivyo katika uchaguzi wa Novemba 27, wasiingize mguu wao uwanjani bali waache vyama vishindane na atakayeshinda ashinde kihalali.

Amemaliza hotuba yake kwa kuwahimiza wananchi wa manispaa hiyo kujitokeza kwa wingi kupiga kura, kuzisimamia na kuzilinda mpaka pale mshindi wa halali atakapotangazwa, huku akiwataka kuwa walinzi dhidi ya nyendo zozote mbaya zile zitakazohisiwa kabla ya uchaguzi.

“Tutakuwa pamoja kesho wote, kila mtu atoke kwenda kupiga kura, na kila mtu alinde kura. Vijana wa amani tuhakikishe mitaa yetu ni salama, tuhakikishe mama zetu, watu wazima, wajawazito wanapata nafasi ya kupiga kura mapema, wazee wetu wa mji wameshatufanyia kazi kubwa sana, wameshaulinda mji wetu, kwahiyo kesho mzee akifika kwenye Kituo cha kupigia kura, mpe nafasi aende akapige kura”, ameeleza Zitto.