RAJAB MKASABA

 

ZANZIBAR

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Viongozi wengine walihudhuria katika hitma hiyo ni  Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubeir, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, viongozi wa Serikali zote mbili, Viongozi wastaafu, Viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge,Wawakilishi, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, wananchi kutoka maeneo mbalimbali pamoja na Mabalozi wadogo waliopo Zanzibar.

Hitma hiyo ya kumuombea dua Marehemu Mzee Abeid Amani Karume  ambayo ni miongoni mwa Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Zanzibar (Karume Day) ilitanguliwa na Qur-an tukufu iliyosomwa na Ustadh Sharif Abdulrahman Muhidin kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na kuongozwa na Sheikh Jafar Abdallah kutoka Masjid Noor Muhammad.

Baada ya hitma hiyo, Sheikh Khamis Gharib kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana alitoa tafsiri ya Suratul Fussilat iliyosomwa na Ustadh Sharif Abdulrahman Muhidin kuanzia aya ya 30 mpaka aya ya 35. Yenye maudhui sawa na siku hii.

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka April 7, viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika hitma hiyo walimuombea dua, marehemu mzee Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa Afisi ya CCM Kisiwandui iliyoongozwa na viongozi wa dini akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi kwa upande wa dini ya Kiislamu, Padri Stanley Lichinga kutoka Kanisa la Anglikana  Zanzibar na Kashap Pandra aliyesoma kwa niaba ya Wahindu.

Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la Marehemu Mzee Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, aliyeweka shada la maua kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Mzee Abdallah Rashid Abdallah aliweka shada la maua akiwawakilisha wazee. Balozi Ali Karume aliweka kwa niaba ya familia ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.

Mwanamwema Shein, Shadya Karume, Mama Fatma Karume, na viongozi wengine wanawake nchini waliungana na akina mama wengine katika hitma hiyo iliyofanyika katika Ofisi hiyo Kuu ya CCM Kisiwandui.

Rais, Dk. Shein amefanya mahojiano na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa Marehemu Mzee Karume aliweka misingi ya utawala bora katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ataendelea kukumbukwa kwa hilo na mambo mengine mengi aliyoyafanya.

Ameeleza kuwa Karume aliongoza ukombozi wa Zanzibar ambao ulikuwa wa lazima na Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalikuwa ya halali na yeye alisimama kidete kuingoza ASP na kupanga na wenzake na hatimaye kuikomboa Zanzibar na Serikali kurudi kwa wananchi wenyewe wa Zanzibar.

Ametoa pongezi kwa viongozi na wananchi waliohudhuria katika dua hiyo na kusisitiza kuwa Mzee Karume ameweka mfumo mpya wa Serikali ambapo Serikali hiyo imeundwa kwa Dikrii namba sita kati ya Dikrii nyingi zilizotungwa ambapo Serikali ambayo ilikuwa na mfumo wa Kidemokrasi na kusisitiza kuwa  Serikali ya Awamu ya Saba imeendelea kufanya kama zilivyofanya Awamu sita zilizopita kwa nyakati tofauti na uwezo tofauti.

Aidha, alisema kuwa wanaosema kuwa neno Mapinduzi lisiwepo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni wapinga Mapinduzi na Muungano na si watu wa maendeleo na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ipo na itaendelea kuwepo kwa sababu imetamkwa katika Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuwatumikia wananchi na ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ameisimamia kuiunganisha yeye pamoja na mwenziwe Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Na huyo anayabeza Mapinduzi basi ujue kuwa pia kafaidika nayo, kwani hakuna mwananchi hata mmoja wa Zanzibar ambaye hajafaidika na Mapinduzi yaliyosimamiwa na Mzee Karume…na hakuna hata mmoja asiyemuombea dua Mzee Karume na yule anayefanya hivyo basi ni wale ambao wanayapinga Mapinduzi,” amesema Alhaj Dk. Shein.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa siku hii ni siku adhimu kwani waliodhani wataidhoofisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, walidhani wananchi wa Zanzibar watavunjika moyo na  wao walidhani kuwa wao wanaweza kuitawala Zanzibar mambo ambayo hayakutokea na hayatatokea na kueleza kuwa wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaikumbuka na wanaithamini sana siku hii.

April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 46 tangu kifo chake.

By Jamhuri