ADARSH NAYAR: Mpigapicha wa Mwalimu

“Nakumbuka nilikuwa mtoto mdogo, nikiwa na miaka zaidi ya 10 hivi, ikatokea siku moja miaka ya 1959 – kabla ya Uhuru, pale kwenye kiwanja cha Dar Brotherhood nikasikia kuna mtu akihutubia.

“Nikasogea na kukuta ana kina Kenneth Kaunda pamoja na Askofu Trevor Huddleston. Ndipo nilipojua mtu yule anaitwa Julius Nyerere.

“Hotuba yake ilikuwa na maneno mazuri sana. Alikuwa akiongea maneno ya kusaidia maskini. Yalinigusa kwa sababu hata mimi na familia yangu tulikuwa maskini…nikaona anazungumza lugha yangu. Tangu siku hiyo nikaanza kumfuata kila alipokwenda katika Jiji la Dar es Salaam.” Haya ni maneno ya Adarsh Nayar, mmoja wa Watanzania wenye asili ya Kiasia waliompenda mno Mwalimu Julius Nyerere; hata wakaamua kuwa karibu naye.

Nayar alimjua Mwalimu kutokana na kazi yake ya upigaji picha. Anajivuna kwa kusema anatoka kwenye familia ya wapigapicha.

 

Mkutano aliohudhuria Dar Brotherhood, ukawa ndio mwanzo wake wa kuwa karibu na Mwalimu Nyerere.

Baadaye akawa mmoja wa watu waliompiga Mwalimu picha zenye mvuto wa kipekee. Picha rasmi ya Mwalimu Nyerere inayotumika katika ofisi na sehemu mbalimbali za umma ilipigwa na Nayar. Lakini kabla ya hapo aliweza pia kumpiga picha nyingine rasmi.

Anakumbuka siku za awali alipomuona Mwalimu kwa kusema: “Kwa kweli ilibidi niwe ninakwenda katika mikutano yake. Nilimuona mapema kabisa kuwa huyu si kiongozi tu, bali ni mwanafalsafa. Staili yake ya uzungumzaji ilituvutia wengi. Mwalimu alikuwa na frequency. Alikuwa na uwezo wa kumfanya mtoto, mzee, msomi na hata asiye msomi kuweza kumwelewa.

“Kila msikilizaji aliweza kumwelewa. Alikuwa na lugha ya kuzungumza UN (Umoja wa Mataifa), alikuwa na lugha ya kuzungumza na wazee wa TANU (Tanganyika African National Union)…frequency yake iligusa kila kundi,” anasema Nayar na kuongeza:

 

“Staili ya Mwalimu ilikuwa akisema chochote anakutazama machoni…ana fix machoni kwako mpaka meseji yake I sink (ikuingie). Akiona hawajapata (hadhira) meseji anatoa mfano wa kwanza, wa pili mpaka wasikilizaji wapate meseji aliyokusudia kuwaambia. Nilipenda sana staili yake.

“Mkienda katika vijiji akiongea na watu wanamuona kwa macho…inakuwa kama wao wanamjua na yeye anawajua. Alikuwa anawasikia sana watu. Hiyo ilikuwa tabia yake…kusikia watu. Hakuwa one way traffic. Mara nyingi alikuwa anauliza ‘matatizo yenu nini?’”

Anakumbuka kuwa Mwalimu aliposafiri mikoani, muda wote alitazama hali ya maisha ya wananchi. “Alipokuwa vijijini akiwa ndani ya gari macho yake yalikuwa nje tu, hakusoma magazeti akiwa katika gari kwa sababu alitaka kuona hali halisi ya maisha ya wananchi wake. Alikuwa hasemi uongo; naamini yote hayo yalitokana na dini yake, kwa sababu alishika dini sana. Mtu anayemuogopa Mungu ni mzuri. Ukiwa na God fearing (kumuogopa Mungu) unakuwa kiongozi mzuri…uwe Mwislamu, Mhindu na kadhalika; inasaidia sana,” anasema Nayar na kuongeza:

 

“Mwalimu alikuwa binadamu wa aina yake. Personality (haiba) yake kumpiga picha ilikuwa nzuri.”

Nayar akiwa Katibu wa Tanzania Press Club, anakumbuka matukio matatu makubwa aliyomshirikisha Mwalimu kwa kuyasimamia kikamilifu.

Anayataja matukio hayo kuwa ni mkutano wa Mwalimu na waandishi wa habari katika Hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam mwaka 1995, sherehe za miaka 75 ya kuzaliwa kwa Mwalimu zilizofanyika Diamond Jubilee jijini humo; na Sherehe za Mei Mosi za mwaka 1995 ambazo Nayar anasema aliratibu safari yote ya waandishi wa habari.

“Hayo matukio nayakumbuka sana. Yalikuwa matukio makubwa kwa sababu kama mikutano hiyo miwili Mwalimu aliitumia kutoa ujumbe mzuri sana kwa Watanzania,” anasema.

Lakini ilikuwaje Nayar akawa karibu na Mwalimu? Anasema katika miaka ya 1960 alifanya kazi katika magazeti ya serikali (Tanganyika Standard), na hapo akawa anapata fursa ya kuhudhuria mikutano mingi ya Mwalimu pamoja na kufanya naye ziara mikoani.

“Ulinzi ulikuwa mkali sana hasa ukizingatia wakati ule, lakini ikatokea nikawa karibu na walinzi. Nakumbuka nilikuwa naelewana vizuri sana na Mpambe Mkuu wa Mwalimu, Peter Bwimbo. Yeye alikuwa akifanya kazi yake, na mimi nilikuwa nafanya kazi yangu ya kupiga picha.

“Hali hiyo iliniwezesha kumsogelea Mwalimu na kupata picha nzuri sana. Mimi na wapigapicha wenzangu tulikuwa na wajibu wa kuhakikisha picha nzuri na zenye ujumbe maridhawa zinatoka kwenye magazeti,” anasema.

Miongoni mwa picha alizopiga ni zile zinazomuonyesha Mwalimu akiwa amevalia sare za jeshi katika Kambi ya Ruvu mwishoni mwa miaka ya 1960.

“Hii picha (anamuonyesha mwandishi), wengine hawana. Nilimpiga JKT Ruvu. Unaona amevaa kofia ya jeshi na mabegani kinaonekana cheo chake,” anasema Nayar.

Nayar anaikumbuka picha rasmi ya Mwalimu inayotumika sasa kwamba aliipiga ili itumike kwenye harambee kuchangisha fedha kwa ajili ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

“Mwalimu alipoiona ile picha hakuwa na mjadala. Akaipenda sana na akapendekeza ndiyo iwe picha yake rasmi.

“Ile picha halisi niliyopiga ninayo, lakini sasa nasikitika kuona mitaani zinauzwa picha za aina hiyo hiyo zikiwa hazina ubora kabisa. Ungewekwa utaratibu wa mahali pa kuipata picha ya Mwalimu yenye ubora badala ya hizi zinazonakiriwa mitaani,” anashauri.

 

Nayar anasema amekuwa kwenye mpango mahususi wa kumuenzi Mwalimu kwa sababu anaona bado eneo hilo, hasa la kuweka kumbukumbu za Mwalimu likiwa halijapewa kipaumbele sawa sawa.

“Kwanini hatuweki makumbusho ya picha tu za Mwalimu? Nchi nyingine wanafanya hivyo kwa waasisi wao. Kunapaswa kuwepo vitalu na documentary ya maisha yake. Mimi nipo tayari kufanya hayo, lakini ufadhili ndiyo shida. Mimi sina uwezo wa kifedha na huu ni mradi mkubwa unaohitaji fedha nyingi,” anasema.

Akirejea maneno ya Mwalimu wakati akipewa Tuzo ya Amani ya Lenin mwaka 1987, Nayar anasema Mwalimu aliamini pasipo na haki hakuna amani.

“Pengo kati ya walionacho na wasionacho linaongezeka, viongozi wanaokuja walione hilo na wajitahidi kulipunguza. Kunatakiwa kwa kweli kuondoa pengo kubwa kati ya maskini na tajiri. This is very bad for peace and security of the country (hii ni hatari kwa amani na usalama wa nchi),” anasema.

 

Nayar anashirikiana na binti wa Mwalimu Nyerere, Anna Watiku, kuandika kitabu cha historia ya Mwalimu.

“Tunaandaa kitabu pamoja na Anna. Kitaitwa ‘Mwalimu Julius Nyerere: My Father’.

“Watanzania walimpenda sana Mwalimu. Walimuamini. Hata alipowaambia waandae mashamba mvua itanyesha wakati fulani, walitii kwa sababu walimuamini sana. Sidhani kama viongozi wa siku hizi wanasikilizwa kama ilivyokuwa wakati wa Mwalimu. Alikuwa akisema hali itakuwa nzuri, wananchi wanamuamini.

“Mwalimu alisaidia karibu nchi nzima kupata elimu ya msingi na baadhi walisoma hadi vyuo vikuu. Sasa watu hawaendi shule kwa sababu hawana fedha. This is shame. Mwalimu alikuwa mtu mzuri sana. Je, tunafanya nini sasa? Ni maneno tu?” Anahoji Nayar.

 

Nayar anasema hakuna wakati mgumu kwake kama siku alipoona jeneza lenye mwili wa Mwalimu pale Msasani, Dar es Salaam.

“Nilizimia pale Msasani, nilipoteza fahamu kabisa, ni tukio lililoniuma na linaendelea kuniuma kuona kweli Mwalimu amefariki dunia na yumo katika jeneza. Nilizimia,” anasema.

Nayar ambaye kwa sasa shughuli zake nyingi anazifanyia London, Uingereza, amepiga picha za Mwalimu kuanzia mwaka 1959 hadi mauti yalipomfika (Mwalimu) mwaka 1999.

Licha ya kuwa Uingereza, anaendelea kuja nchini mara kwa mara akiwa anaishi Upanga, Dar es Salaam kwenye nyumba inayomilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Ni mjamaa kwa maneno na kwa matendo.

“Nataka kuanzisha makumbusho ya Mwalimu Nyerere, yenye picha zake za kawaida na za video.

Nina maelfu kwa maelfu ya picha ambazo hazijapata kuonekana kwa watu wengi. Natamani nipate kiwanja mahali kunakofikika hasa katikati ya Dar es Salaam. Walimwengu wengi watafaidi, maana naamini hakuna mwenye kumbukumbu kama hii,” anasema.