Baada ya kifo cha hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tangu Oktoba 14, 1999, mshairi mmoja aliandika hivi: “Hatutamwona mwingine kama Nyerere.”

Ni kweli taifa letu halitampata Nyerere mwingine, kwa sababu unapomlinganisha Mwalimu Nyerere na watawala wengine waliokalia kiti alichowahi kukikalia unakutana na ombwe kubwa la uongozi, hekima na maadili.

Historia ni mwalimu mzuri na shahidi bora. Ninapoitazama historia ya taifa letu lilipotoka, lilipo, linapokwenda na hali ya taifa letu ilivyo kiuchumi, kisiasa, kielimu na kimaadili ‘ninalia’.

Tuimbe kidogo: “Kama si juhudi zako Nyerere…..Ooooh, kama si juhudi zako Nyerere…Na…Uhuru tungetapa wapi…Na…..Amani tungepata wapi…Oooooh, kama si juhudi zako Nyerere…’’ 

Ni vigumu kumpata kiongozi mwema na ukimpata ni vigumu kumwacha na ukimwacha ni vigumu kumsahau.   Maisha ya Mwalimu Nyerere ni zawadi kwa Taifa la Tanzania na ulimwengu wote kwa ujumla wake. Katika makala hii nitamtazama Mwalimu Nyerere kama mwanafalsafa.

 

Ni kweli Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa wanafalsafa waliopata kuishi hapa duniani. Ninafurahi kuona kwamba dunia inamtambua Mwalimu Nyerere kama mwanafalsafa. Hii ni sifa kwa Taifa letu la Tanzania.

Hivyo, Mwalimu Nyerere ana hadhi sawa ya kifalsafa kama walivyo Plato, Socrates, Pythagoras, Heraclitus, Hegel na wengine wengi. Katika makala hii nafahamu nitatofautiana na mawazo ya walio wengi hasa na ‘watawala wasio na hadhi ya kuitwa watawala’ na ‘wasomi wasio na hadhi ya kuitwa wasomi.’

Ni furaha yangu kuona ninatofautiana na walio wengi, kwani katika kutofautiana huko nitanufaika kwa kujifunza mengi. Maisha yana ladha pale tu tunapotofautiana mitazamo, hatuwezi kufanana mitazamo na maisha yakapata ladha.

Maana yangu ni hii; hauwezi kunilazimisha nikubaliane na mtazamo wako kama mtazamo wako hauna vigezo vya kunishawishi kukubaliana nao. Hali kadhalika na mimi pia siwezi kukulazimisha ukubaliane na mtazamo wangu kama mtazamo wangu hauna vigezo vya kukushawishi ukubaliane nao.

 

Pamoja na ukweli kwamba binadamu wote ni sawa, lakini uwezo wa kufikiri na kufikia uhalisia wa mambo unatofautiana. Mawazo aliyonayo mtu unaweza kumtofautisha na mtu mwingine.

Kila binadamu anaishi na falsafa yake, awe anaijua au haijui, bado ni falsafa. Ikitokea mtu kwa sababu ya ujinga wake asielewe anaishi falsafa gani ya maisha, hilo litakuwa ni tatizo lake binafsi na si tatizo la falsafa anayoishi.

Kama unafahamu unaishi falsafa gani katika maisha, hongera. Falsafa mizizi yake ni kukosoana. Mwalimu Nyerere ni mwanadamu aliyefahamu anaishi falsafa gani.

Mwalimu Nyerere alikuwa si mtu wa kuiga, bali mtu wa kuitafakari jamii yake na kuitatulia matatizo yanayoikabili. Si kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na akili sana, la hasha! Mwalimu aliishi maisha yanayoongozwa na mfumo wa falsafa ya kufikiri.

Hakika Mwalimu Nyerere kama binadamu anaweza kuwa na mapungufu yake, lakini pamoja na mapungufu yake bado anabaki kuwa ‘taa isiyoweza kuzimika katika taifa letu’.

Ninaungana na juhudi za Kanisa Katoliki la Tanzania katika mchakato wake wa kutaka kumtangaza Nyerere kama ‘Mtakatifu’. Sina shaka kabisa na utakatifu wa Mwalimu Nyerere. Maisha yake yanatosha kumtangaza kuwa ‘Mtakatifu’. Hivyo nasubiri kwa hamu kubwa kusikia ‘Mt. Nyerere wa Musoma’.

 

Historia ya Tanzania haiwezi kuwa historia kamili kama jina la Mwalimu Nyerere halihusishwi. Dunia si shimo la kusahau. Watanzania tukisahau juhudi za Mwalimu Nyerere wapo wakaozikumbuka na kuzienzi.

Kwa bahati mbaya sana Taifa letu la Tanzania halijapata namna nzuri ya kumuenzi Mwalimu Nyerere. Tumebaki  kuadhimisha tu kumbukizi la kifo chake na kurudiarudia nukuu za maneno aliyosema pasipo kutafakari kwa undani aliyoyasema yalimaanisha nini.

Please follow and like us:
Pin Share