*Limbu atamba kudhibiti makundi

Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vikitamba kung’ara katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015, Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema muda wa miaka mitatu uliobaki unatosha kujipanga kutwaa uongozi wa nchi.

Kauli hiyo ya ADC imekuja miezi mitatu baada ya kupata usajili wa kudumu (Agosti mwaka huu). Chama hicho kinatazamiwa kuchochea ushindani wa kisiasa utakaosaidia wananchi kufanya uamuzi sahihi wa kuchagua chama kinachofaa kukabidhiwa madaraka ya nchi.

 

Katika mahojiano na JAMHURI jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa ADC, Lucas Limbu, ametamba kuwa chama hicho kinajipanga kuvibwaga kwa kishindo vyama vyenye ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini, CCM na CHADEMA.

“Tumedhamiria kutwaa uongozi wa nchi hii, mwaka 2014 tutawasukumia mbali CCM na marafiki zake wanaojiita wapigania haki za Watanzania wakati si kweli, tunajipanga kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2015 unaiweka ADC madarakani,” anasema Limbu.


“Ingawa ni mapema sana kulisema sisi kama chama cha ADC kutamka, lakini sisi lengo letu la pamoja ni kushinda uchaguzi, ni kuchukua dola ya nchi hii kwa njia ya kidemokrasia, hilo ndilo lengo letu namba moja.


“Kwa sababu hiyo, ‘automatically’ tutapima nguvu yetu ya kisiasa ikoje, kama tutaona tuna nguvu ya kisiasa ya kutuwezesha kuweka mgombea wa urais, na si urais tu, hata wabunge na madiwani, hata viongozi wa serikali za vijiji na mitaa, tutasimamisha wagombea.


“Tulijipima uchaguzi mdogo wa udiwani tukaona tunahitaji kujitangaza kwa Watanzania, tukaona kwamba sisi kama chama cha siasa ambacho ni kipya tuache kwanza, twende sehemu mbalimbali vijijini, mikoani tukazungumze na Watanzania, tuwaelimishe kwanza wajue matatizo ya nchi yao ni yapi, tatizo la viongozi ni nini na tatizo la wanaotafuta uongozi sasa ni nini.

 

“Kwa hiyo, 2015 kwetu sisi ni mbali mno, yaani ni kipindi cha kutosha kutupima, ni muda wa kujipima na kuona namna ambayo tunaweza kuingia kwenye uchaguzi, tena tukashinda kwa kishindo, si tu kuingia kwenye uchaguzi kusindikiza ama kujaribisha, hapana, tutaingia kwenye uchaguzi tukiwa na imani tunakwenda kushinda.

 

“ADC si siasa za watu binafsi, si siasa za mtu mmoja mmoja, si siasa za makundi fulani, jamii inayotuzunguka ndiyo itaamua kwa sababu waliotutangulia (hakuwataja), mwelekeo wao na mawazo yao ni kuhakikisha makundi yao yananeemeka na si Watanzania.

 

Anasema Watanzania hawana budi kujivunia chama cha ADC kwani kwani kina utashi wa kuleta mabadiliko ya kweli nchini katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

 

“Sisi ADC tunasema Watanzania wamepata chombo cha kuwasaidia, tunaomba watuunge mkono kwa nguvu kubwa, wala wasipotoshwe kwamba chama hiki ni kichanga, hakina uwezo na hela.

 

“Viongozi tulioanzisha chama hiki ni watu wenye utashi na nia njema kwa taifa letu la Tanzania. Nia yetu si sisi na familia zetu wala makabila yetu, dini zetu, wala maeneo tunakotoka, hapana,” anasema.

 

Kwa mujibu wa Limbu, miongoni mwa sifa kuu zitakazokiuza ADC kwa Watanzania ni uadilifu na uaminifu wa viongozi wake katika kuutumikia umma. Kwamba ADC hakitatoa mwanya wa matatizo ya ubinafsi, makundi yanayohasimiana, vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za chama na umma.

 

“Tunapiga vita kila aina ya uovu. Kwa mfano, leo kinachoangamiza taifa letu ni matumizi ya fedha, mtu anachukua hela za watu anakwenda kuzigawa kwenye uchaguzi, hatimaye anatakiwa azirudishe, anahangaika kuzirudisha badala ya kuhangaika kutafuta maendeleo ya wananchi.

 

“Kwanza tunataka Watanzania waelewe kuwa mtu anayekwenda na fedha kwenye uchaguzi, maana yake ni kwamba anakwenda kununua fedha zao za maendeleo ya miaka inayofuata. Shughuli za maendeleo ya jamii zinakwama kwa sababu watu wanalipa madeni waliokopa kwa ajili ya kugharimia uchaguzi.

 

“Mimi nikiona makundi yanaanza kuibuka ndani ya ADC nitayapiga vita hadharani wala sitaona aibu, hata kama anayehusika ana mapembe, kwa sababu najua hatima ya haya makundi ni kuwa na uongozi usiofaa, uongozi unaotumikia watu badala ya Taifa.

 

“Sisi tunawaomba Watanzania watuunge mkono, wajiunge na ADC, narudia kusema kwamba chama hiki ni cha Watanzania, tunapinga kila aina ya ubaguzi unaowagawa wananchi,” anasisitiza Limbu.


Utajiri wa viongozi

“Kwenye mabadiliko ya Katiba, tuweke limit (mpaka) ya utajiri wa viongozi wetu. Kiongozi asifike mahali akatajirika tu wakati huko nyuma hakuwa tajiri. Kama mtu aliingia madarakani akiwa na gari moja, anapotoka basi atoke na magari mawili, asitoke na magari saba, asitoke na nyumba kumi.


“Katiba mpya itamke wazi kwamba ikigundulika kiongozi fulani amejikusanyia mali ambazo hazina kiwango, basi anyang’anywe hadharani. Tukifika mahali Watanzania tukawa serious (tukamaanisha) kiasi hicho, mimi naamini watu hawataanza kutafuta uongozi kwa manufaa yao na ‘automatically’ makundi yatakufa,” anasema Limbu.


Wadadisi wa masuala ya siasa na uongozi wanataja sababu kuu ya makundi kuendelea kupata mwanya ndani ya vyama vya siasa, kuwa ni tabia ya baadhi ya watu kutafuta madaraka na maslahi binafsi.


“Lakini mimi na mwenyekiti wangu wa ADC Taifa, Said Miraji, tumekubaliana kwamba hatuwezi ku-entertain (kukaribisha) suala la makundi kwa sababu tukisapata makundi tutakihatibu chama.


“Na kwanini tuwe na makundi, kama mimi leo sipiganii familia yangu, marafiki na jamaa zangu, kwanini niwe na kundi? Kundi linapatikana tu pale ambapo watu wanapambana kwa ajili ya madaraka, maslahi binafsi, familia zao, jamaa na marafiki zao.

 

“Wewe angalia makundi yote yanayosigana katika vyama vyote vya siasa. Ukikuta makundi mawili yanapingana ndani ya chombo hicho ujue nyuma ya pazia hiyo kuna kundi la watu wanashinikiza kupitia kiongozi fulani wapate nafasi ya kuchukua uongozi ili akishinda nafasi yake waweze kuendelea kuchukua na kufuja rasilimali zetu.

 

“Jambo ambalo tunatakiwa tuwe makini sana especially (hasa) sisi ambao tunaanza siasa za kuchipukia, lazima tuwe makini sana na tusiwe tayari kukubali kuingizwa kwenye ‘channels’ za makundi.

 

“Ukikuta mtu amesimama kwenye makundi ujue hapiganii Tanzania, kuna kundi analopigania na hata akichukua madaraka lazima atafanya kazi kwa interest (maslahi) ya makundi yake na watu wake, hatatazama jamii kama jamii,” anaongeza Limbu. Makundi yakidhibitiwa katika vyama vya siasa nchini, maendeleo ya kiuchumi na kijamii yataonekana nchini kuliko ilivyo sasa wakati Watanzania wengi ni masikini kupindukia licha ya Serikali kusema uchumi unakua.


“Uchumi wa Tanzania unakua kwenye makaratasi wakati katika hali ya kawaida ya maisha ya Watanzania uchumi unaporomoka siku hadi siku. Kusema uchumi unakua wakati wengine wanalala njaa ni dhihaka. Ni dhihaka kusema uchumi unakua wakati wengine wanatembea uchi na wananchi hawapati huduma za bora za kijamii kama vile maji, afya, elimu, nakadhalika. “Tunahitaji viongozi ambao wako tayari kutuongoza kwa jina la Tanzania na si kwa jina la makundi yao,” anasema Katibu Mkuu huyo wa ADC.


Muungano wa wapinzani

Kiongozi huyo wa ADC anasema ni vigumu kwa vyama vya siasa vya upinzani nchini kuungana katika uchaguzi, kwa vile hakuna chama kilichodhamiria kufanya hivyo kwa dhati ya moyo.

 

“Ni kweli watu wamekuwa wakiuliza kwanini wapinzani hamuungani mkatengeneza ushirikiano ili kuing’oa madarakani CCM,” anasema Limbu na kuendelea:

 

“Mimi nasema wapinzani hatutafika mahali tukaungana hata siku moja. Vyama vya siasa vya kwetu havitaungana kwa sababu ADC tukiamua kuungana kwa mfano na NCCR-Mageuzi, ama na UDP, ama na NLD, ama na Chadema ama na chama chochote kile, sisi lazima tuue cha kwetu twende tukafanye kazi na chama kingine.

 

“Kwa mfano, kwa hali halisi ilivyo sasa, tukiunga mkono UDP, baada ya uchaguzi rasilimali zote zitakazopatikana kutokana na nguvu za uchaguzi zitakwenda kwenye chama hicho, sasa matokeo yake wale viongozi wa chama husika wataona neema imewaijia wao siyo vyama vingine. “Mfano rahisi tunao, katika chaguzi zilizopita, vipo vyama vilivyounga mkono chama kingine cha siasa, UDP kwa Kanda ya Ziwa waliwaunga mkono Chadema na vyama vingine vya upinzani viliwaunga mkono Chadema.

 

“Mwaka 2005 vipo vyama ambavyo viliunga mkono CUF lakini baada ya uchaguzi kauli iliyotolewa na CUF ikaonekana hivi vyama vingine vilikuwa vinaisaidia CCM, kwamba ni vyama vilivyotumwa na CCM. “Kauli hiyo hiyo hiyo imekuja kuonekana baada ya Uchaguzi wa mwaka 2010. Chadema pamoja na kuungwa mkono na vyama vingine, wakasaidiwa wakapata kura nyingi za urais na wakapata nafasi ya kuwa na idadi ya wabunge wanaoweza kuunda serikali ya upinzani bungeni.

 

“Chadema wakatoa kauli wakasema hivi vyama vingine ni wasaidizi wa CCM, sisi hatuwezi kushirikiana nao, hatuwasingizii. Kwa mfano, mzee Mapesa (John Cheyo – Mbunge wa Bariadi Mashariki kupitia UDP), kule Bariadi aliomba kura za urais apewe Slaa (Dk. Wilbrod). Wagombea ubunge wengine wote wa UDP walikuwa wanasema mpeni kura Slaa.

 

“Lakini leo Mapesa hayumo kwenye serikali ya upinzani ya Chadema, hayumo. Hebu jiulize hata ungekuwa wewe, utapata wapi moyo wa kusema utashirikiana na chama kingine.

 

“Marekani wana vyama 53, lakini vyama vinavyoonekana ni viwili tu, ndivyo vinavyoweka candidates (wagombea) wa urais, kwa sababu vyama vingine vinapata nguvu ya kubebwa na vyama vilivyoteuliwa, vinashirikiana navyo, vinakua na utaratibu wa kusaidia kuleta changamoto kwenye vyama vyenye nguvu.

 

“Vilevile hata Uingereza wanavyo vyama vingi. Sasa sisi kinachotakiwa Wakenya hapa wametuzidi akili. Wale wanaweza wakaanzisha chama leo, keshokutwa wakaingia kwenye uchaguzi. Masharti ya uanzishaji wa vyama vya siasa Kenya siyo magumu kama hapa Tanzania.

 

“Sisi tuna tatizo kwenye mfumo, tunahitaji tubadilishe mfumo wetu hata wa uanzishaji wa vyama vya siasa ili tuweke mazingira rahisi ya watu kushirikiana. Tukitengeneza mazingira hayo hatutahitaji ufadhili kutoka nje. Hatutahitaji nguvu ya fedha kutoka nje.

Ufadhili wa ADC

“Sisi ADC tunajua kupata nguvu ya fedha kutoka nje (ya nchi) ni kosa la jinai. Wanaochukua fedha kutoka nje ya Tanzania kuna ahadi wanazowapa watu wanaowapa fedha.

 

“Mungu huwa hatoi tu msaada hivi hivi na ni mambo haya haya ya siasa. Hizi political foreign aid (misaada ya kisiasa kutoka nje ya nchi) nyingi zina ajenda nyuma ya pazia. Ndiyo maana baada ya uchaguzi utawakuta walioshinda sasa wanaanza kuhangaika kuhakikisha wana-fulfil (wanatimiza) matakwa ya aliyewapa msaada wa fedha kwa ajili ya kugharimia uchaguzi. Lazima wahakikishe wanatimiza.

 

“Utakuta hao wanaoleta misaada ya fedha wana masharti wanayoyatoa kwenye vyama husika kwa siri, nyuma yake kuna masharti yanawekwa, kwamba tunakupa hizi fedha lakini ukishapata madaraka tunataka mgodi fulani.

 

“Matokeo yake watu watafika mahali wanakiri hadharani kwamba mikataba ni mibovu, kumbe waliingia mikataba ile kutimiza masharti ya watu waliowasaidia fedha wakati wa kutafuta ushindi kwenye uchaguzi wa kisiasa. Hayo ndiyo yanayotuharibia nchi leo.

 

“Sasa sisi ADC tuna mpango na mkakati wa kuhakikisha tunawaelimisha wanachama wetu vizuri.


Tuna mpango wa kuendesha semina kwenye matawi na sehemu mbalimbali nchini.

 

“Tunataka kila mwanachama akichangie cha kwa wiki Sh 100. Kama tutatunza hizi fedha vizuri na wanachama wetu wanakuwa waaminifu wa kuchanga hizi fedha, hivi kwanini tuhitaji ufadhili au msaada kutoka nje?

 

“Kwanini tuhitaji fedha za Mzungu? Kwanini tuletewe magari ya kifahari kwa ajili ya kuhamasisha siasa kwenye nchi masikini kama Tanzania? Nchi ambayo leo watu wanasema ni masikini lakini matumizi yao hata nchi tajiri hawafanyi hivyo.

 

“Siku tulipoanza kulisema hili (la kuchangisha Sh 100) vyama vingine navyo vikaanza kutumia utaratibu huu, lakini sisi tunaamini kama Watanzania watatuunga mkono tutajitegemea katika shughuli zetu,” anasema Limbu.

 

3682 Total Views 19 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!