Wakati michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ikiendelea nchini Misri hii leo ili kukamilisha hatua ya makundi, makundi mawili yataingia uwanjani kupepetana ili kuungana na timu nyingine waweze kufuzu hatua inayofuata ya mashindano hayo. Makundi hayo yaliyosalia ni kundi E na kundi F.

Kundi E lina timu za Mali, Angola, Tunisia na Mauritania. Mali yenye pointi nne ambao wanaongoza kundi hilo watakuwa uwanjani leo usiku ili kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya timu ya Angola wenye pointi mbili katika dimba la Ismailia.

 Katika mchezo huu Mali wanahitaji pointi moja baada ya kuwa na mtaji mkubwa wa magoli baada ya kufunga magoli matano hadi hivi sasa. Wakati Mali wanahitaji pointi moja, Angola wanahitaji pointi tatu zinazoweza kuwasaidia kuungana na timu nyingine zilizofuzu katika hatua ya pili ya mashindano hayo ya AFCON.

Ukiachana na mtanange wa Mali na Angola, kutakuwa na mechi nyingine katika kundi hilo. Mechi hiyo inazikutanisha Mauritania na Tunisia katika Uwanja wa Suez Army. Tunisia wanaoongozwa na nahodha wao, Wahbi Khazri, anayechezea timu ya Saint-Etienne ya Ufaransa, endapo wataibuka na ushindi watafanikiwa kufuzu hatua inayofuata katika michuano hiyo.

Timu ya Tunisia kabla ya kumalizia mchezo wa leo tayari wana pointi mbili baada ya kutoka sare dhidi ya Angola na Mali na iwapo Mali watashinda katika mchezo wa leo watakuwa na pointi tano zinazoweza kuwasadia kufuzu hatua inayofuta, lakini kufuzu kwao kutatokana na timu ya Mali au Angola endapo mmojawapo atapoteza au kutoka sare inaweza ikawabeba Tunisia.

Kwa upande wa Mauritania watakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha wanashinda katika mchezo wa leo.  Licha ya ushindi watatakiwa kufunga magoli zaidi ya mawili, kwa sababu katika mechi yao dhidi ya Mali walifungwa magoli 4-1.

Kundi F, ambalo linaundwa na timu ya Cameroon ambayo ni bingwa mtetezi, timu nyingine ni pamoja na Ghana, Benin na Guinea-Bissau, ambao watahitimisha hatua ya makundi hii leo, ambapo kutakuwa na shughuli pevu ya kuhakikisha wanatafuta nafasi ya kufuzu katika hatua inayofuata.

Katika kundi hili kila timu ina nafasi ya kufuzu katika hatua inayofuata, timu ya Cameroon haimo kwenye presha kubwa sana ukilinganisha na timu nyingine, kwani wanaongoza katika kundi E, wakiwa na pointi nne baada ya kushinda katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Guinea-Bissau na  suluhu waliyoipta dhidi ya timu ya Ghana (Black Stars).

Hivyo katika mchezo wao wa leo dhidi ya Benin utakaofanyika katika Uwanja wa Ismailia watakwenda kupambana ili kutafuta walau pointi moja inayoweza kuwasaidia kuungana na timu nyingine ambazo zimekwishafuzu katika fainali hizi.

Katika mtanange mwingine katika kundi hilo kutakuwa na mchezo kati ya Ghana ambao wana pointi mbili watacheza  dhidi ya kibonde wa kundi hilo timu ya  Guinea-Bissau ambao wana pointi moja. Na iwapo Ghana watashinda au kutoka sare ya aina yoyote na Cameroon wakiwafunga Benin wanaweza kusonga mbele katika hatua inayofuata.

Ikumbukwe katika fainali za msimu huu timu nne zitachaguliwa kusonga mbele katika hatua ya kumi na sita bora licha ya kutoshika nafasi ya kwanza au ya pili. Hizo timu nne zitaungana na timu 12 zilizoshika nafasi ya kwanza na ya pili ili kuingia hatua ya 16 bora zitakazopambana ili kuingia hatua ya robo fainali.

Viongozi wa CAF watachagua timu hizo ambazo wao wataona zina vigezo ambavyo wanafikiri zinastahili kupewa nafasi ya upendeleo.

By Jamhuri