GEITA

Na Antony Sollo 

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita limetekeleza agizo lililotolewa na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde, kwa kuwaweka kando kupisha uchunguzi watumishi watatu wa Idara ya Mapato wa halmashauri hiyo wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za umma.

Akizungumza na JAMHURI, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Pastory Mkaruka, anakiri kusimamishwa kazi kwa watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, akiwamo mhasibu wa wilaya hiyo na wenzake wawili waliokuwa wakifanya kazi kitengo cha ukusanyaji wa mapato.

“Ni kweli Naibu Waziri alifanya ziara kwetu na kuna maagizo ambayo aliyaacha halmashauri iyafanyie kazi, na agizo mojawapo ni ukamilishaji mabweni katika Shule ya Sekondari Lulembela na Mbogwe,” anasema.

Kwa mujibu wa Mkaruka, baada ya uchambuzi wa mahitaji yanayotakiwa katika ukamilishaji wa mradi huo, halmashauri imekwisha kuwasilisha maombi ya vifaa kwa uongozi kwa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kwa ajili ya kukamilisha mabweni hayo.

Ameliambia JAMHURI kuwa uongozi wa GGML umekwisha kuingia mkataba na halmashauri kwa ajili ya kugharimia miradi mbalimbali kwa kutoa vifaa badala ya fedha na kufafanua kuwa gharama za vifaa vinavyohitajika kukamilisha ujenzi wa mabweni ni Sh milioni 100.

Kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma uliofanywa na watumishi wa halmashauri kitengo cha mapato, Mkaruka anasema kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi Mei mwaka huu, kimewachukulia hatua za kinidhamu kwa kuwasimamisha kazi na kuwataka kuwasilisha utetezi, siku ya mwisho ikiwa ni Juni 30, mwaka huu.

“Baada ya hapo itaundwa kamati maalumu itakayopitia utetezi wao na ikibainika wana hatia, hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa,” anasema Kaimu Mkurugenzi Mkaruka.

By Jamhuri