Zanzibar

Na Masoud Msellem

Julai 4, kila mwaka dola ya Marekani huadhimisha siku ya kumbukumbu ya uhuru wake. Mwaka huu inaadhimisha uhuru huo ikiwa ni miaka 245 tangu iupate kutoka kwa Himaya ya Uingereza mwaka 1776. 

Uhuru huo ulipatikana baada ya shaka, madhila makubwa na kiwango cha hali ya juu cha mhanga, kitu ambacho bila shaka yoyote kiligharimu maisha ya Wamarekani kwa maelfu kama si malaki.  

Uhuru wa Marekani ni tukio kubwa lililosababisha kuzaliwa kwa dola kubwa, yenye nguvu baada ya kuung’oa ukandamizaji ulioota mizizi na dhuluma iliyojikita kwa muda mrefu kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza. 

Marekani ilitawaliwa kwa karibu miaka 150 kwa mkono wa chuma, ikiwa chini ya utawala wa kikoloni katika majimbo yake mbalimbali. Ni kipindi kigumu katika historia ya taifa hilo. 

Katika kipindi chote hicho ilipitia mateso na ukandamizaji, ikiwamo wananchi wake kutoruhusiwa kupiga kura kuwachagua viongozi wanaosimamia mambo yao, kutozwa kodi kubwa, vikwazo katika biashara na kuporwa rasilimali zake kwa masilahi ya mabepari na kampuni za Kiingereza. 

Hali hiyo ilishitawi zaidi chini ya utawala wa kidhalimu wa Mfalme George III. 

Hatimaye ndani ya karne ya 18, mchakato wa harakati za kutaka kujikomboa kutoka katika  madhila ya ukoloni zilianza kuota mizizi na kushamiri katika nyoyo za Wamarekani, na wimbi zaidi la upinzani dhidi ya ukoloni lilionekana waziwazi na kuungwa mkono na Wamarekani wengi.

Vuguvugu la upinzani wa Wamarekani lilichukua sura pana zaidi mwaka 1773 katika Jimbo la Boston wakati Wamarekani walipoamua kufa na kupona kuitosa majini shehena ya chai ya kampuni ya Uingereza waliyokuwa wakiipakua kutoka melini. Jambo hili lilisababisha msukumo mpya wa kupigania haki na kuudai uhuru moja kwa moja. 

Uingereza ilijibu na kukabiliana na vuguvugu hilo haraka sana kwa vitisho na kutunga shehena ya sheria za ‘kishenzi’ (Intolerable Acts) kwa lengo la kuzima haraka kile walichokiona kuwa ni ‘tishio dhidi ya Utawala wa Mfalme’.

 Hata hivyo, pamoja na hatua hizo za Uingereza, Wamarekani walijifunga kibwebwe, hawakuvunjika moyo wala kurudi nyuma katika mchakato wao wa kupigania uhuru wao huku kwa ushujaa na ujasiri wakaendelea na mapambano yao hadi kuibuka rasmi vita ya moto ya awali inayoitwa ‘Bunker Hill’ katika Jimbo la Massachusetts mwaka 1775.

Chini ya Jemadari George Washington na kwa msaada wa Hispania na Ufaransa, Wamarekani wakaibuka washindi katika vita ile, na haraka sana, Julai 1776, kongamano la Wamarekani wanaowakilisha majimbo 13 walikutana rasmi kutangaza ‘Tamko la Uhuru’ lililoandaliwa na jopo lililokuwa chini ya Thomas Jefferson na Benjamin Franklin. 

Tamko hili liliweka bayana kwamba kuanzia sasa majimbo yao yako huru na wamejifungua kutoka kwenye minyororo ya utawala wa Uingereza.

Wamarekani walithubutu kutangaza uhuru wao kwa ujasiri na ushujaa huku wakielewa wazi kabisa kwamba kutokana na haiba, hadhi, maguvu na mamlaka ya dola kubwa la Uingereza ulimwenguni na zaidi unyeti wa koloni la Marekani kwa dola hiyo, kamwe hawatakuwa tayari kuutambua uhuru huo walioutangaza, lakini Wamarekani hawakurudi nyuma. Walisimama kidete katika msimamo huo. 

Katika mwaka uliofuata, Uingereza ilishindwa vibaya katika vita dhidi ya wapigania uhuru. Na kwa fedheha na idhilali, ikasalimu amri na kuweka silaha chini katika maeneo ya Saratoga na Yorktown. 

Hata hivyo, na kama ilivyotarajiwa, pamoja na ‘Tangazo la Uhuru’ lililotolewa na Kongamano la Majimbo 13 ya Marekani na kushindwa vibaya kwa Uingereza kwa fedheha katika medani ya vita, bado Uingereza kwa kiburi chake na kudanganywa na maguvu yake, ilichukua karibu miaka saba kulitambua tamko lile.

Ilikuwa mwaka 1783 ndipo Uingereza ilipolazimika kuutambua uhuru wa Marekani kikamilifu chini ya Mkataba wa Paris (Paris Treaty).

Baada ya uhuru ilioupata kwa tabu, shaka na gharama kubwa ya mhanga, Marekani ilibidi ikabiliane na changamoto mbalimbali kama vita ya wao kwa wao, kuunganisha majimbo mengine hadi kufikia 50, kujitosa katika uwanja wa mvutano wa kimataifa, zikiwamo vita kuu mbili na kufanya kazi kwa kujituma, hatimaye dola hii kufika ilipo leo.

Kwa bahati mbaya na katika hali ya mshangao, wakati Marekani kila mwaka inaadhimisha siku ya uhuru wake, bado imekosa kujifunza kutokana na tukio hili kubwa katika historia yake ambalo kila mwaka inaliadhimisha.

Tunasema dola ya Marekani si kwamba imesahau historia yake kwa sababu historia ya mtu huwa ni sehemu yake, bali inadanganyika kwa ghururi na maguvu iliyonayo kiasi kwamba inahisi hakuna haja ya kuchukua ‘funzo’ la kivitendo kutoka katika historia hiyo. Na hili ni kosa kubwa na ndiyo sababu ya kuanguka kwake. 

Khalifa wa Nne wa Kiislamu, Imam Ali (RA), katika hekima zake aliwahi kutamka: “Mwenyezi Mungu amrehemu mtu anayejua atokapo, alipo na anayejua aendako.” 

Akasema pia George Alfred Santayana, Mwanafalsafa na mwandishi wa Kimarekani: “Nchi isiyokuwa na kumbukumbu ya historia ni nchi ya wendawazimu.” 

Marekani inayakana yote haya, inadharau na inatupilia mbali kujifunza kutoka katika historia ya harakati zake za kupigania uhuru hususan katika maeneo manne makubwa: 

 Kwanza, ikiwa Marekani ilifika mahala baada ya dhuluma, madhila na ukandamizaji kutoka kwa Uingereza ikapigana ili kutafuta uhuru wake, na baada ya uhuru huo watu wao wakafanya bidii kwa gharama kubwa kuunganisha nchi yao, kwa kupitia ‘Tamko la Monroe’ (Monroe Doctrine) wakakataa katakata na wakazipinga hata nchi za Ulaya kuingilia mambo yao, si tu katika nchi yao bali katika Bara lote la Marekani; vipi leo Marekani inalisahau hili kwa kuzifanya nchi za wengine kama mazizi yao ya ng’ombe kwa kuwaingilia na kuwalazimisha mambo kinyume cha matakwa yao na kuwafanya viongozi na raia wa nchi hizo kama watumishi au watumwa? 

Pili, Marekani lazima itanabahi kwamba mabavu na kiburi cha dola kamwe si dalili ya nguvu ya dola, bali katika mazingira fulani ni sababu ya maangamizi yake. 

Ichukue funzo kuwa wakati wa kuanza kwa vuguvugu la ‘makoloni’ ya Kimarekani kudai uhuru kutoka kwa Uingereza, baadhi ya watu makini katika Dola ya Uingereza kama Edmund Burke waliwahi kuishauri serikali yao kutochukua hatua za kimabavu dhidi ya makoloni yake ya Kimarekani.  

Lakini kwa kiburi, majigambo na majivuno ya Mfalme George III pamoja na baadhi ya mawaziri wake, walilikataa jambo hili. Hatima yake ikawa fedheha na idhilali kwa Dola ya Himaya ya Uingereza. 

Tatu, ikumbukwe kuingia kwa Hispania na Ufaransa katika mchakato wa kuwasaidia Wamarekani kupigania uhuru kulisukumwa na suala moja tu la kimasilahi. Wakiwa na lengo la kuondosha athari ya Uingereza ndani ya makoloni hayo ili madola yao yajenge ushawishi baada yake. 

Hii ina maana kwamba dola zote za kibepari huangalia kitu kimoja tu nacho ni ‘masilahi’ na kamwe si marafiki wa kutegemea. 

Kwa hiyo, hata leo lau itasimama dola nyingine kubwa, yenye nguvu na rasilimali kwa kutumia kipimo cha masilahi, upo uwezekano mkubwa baadhi ya dola za Magharibi ambazo Marekani inachukulia kuwa marafiki zake wa karibu kumuacha na kuiunga mkono dola mpya iliyosimama kwa kutarajia kupata masilahi zaidi kutoka dola hiyo kuliko wanayoyapata kutoka kwa Marekani. 

Kwa kuwa katika mfumo wa ubepari ‘hakuna urafiki wa kudumu bali masilahi ya kudumu’. Na kwa hilo pia ni rahisi kwa dola hizo kugombanishwa kwa ajenda ya masilahi.

Nne, Marekani inafaa pia ijifunze kwamba msukumo uliowafanya watu wao kujitoa mhanga kupigania uhuru ni ile hali ya kimaumbile aliyonayo kila binadamu, hali ya kuwa na ‘hisia ya kutaka kuishi na kuendeleza maisha yake’ (survival instinct). 

Kwa hisia hii wanaadamu wote hutaka na kupenda waishi katika maisha ya furaha, amani na utulivu wakiwa huru kujiendeshea mambo yao wenyewe kadiri inavyowezekana. 

Na inapotokezea kukosekana jambo hilo kutokana na ukandamizwaji au dhuluma, binadamu huyu hufika mahala akaamua kuondosha dhuluma hiyo ili ajiletee maisha mazuri na ya furaha kwa gharama yoyote, kwa kuwa huo ni msukumo wa kimaumbile. 

Kwa bahati mbaya Marekani inajitia upofu na kudharau kuchukua mafunzo hayo kutoka ndani ya historia yake na badala yake inaitupilia mbali kwa kuibakisha historia yake kuwa ‘nadharia’ tu bila  kuibeba kama dira kwa maisha yao. 

[email protected]

0778 870609

By Jamhuri