Miongoni mwa habari zilizopamba gazeti hili leo ni taarifa ya Mfuko wa Vyombo vya Habari nchini (TMF), kutoa ruzuku ya Sh. bilioni 1.7 kwa vyombo vya habari 16.
Awali ya yote tunaupongeza mfuko huo kwa namna inavyoratibu shughuli zake na kuendeleza vyombo vya habari na wanataaluma wake.
Tunasema hayo hasa tukisukumwa na yale aliyozungumza Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura.
Kwenye hafla ya kutiliana saini mkataba wa mwisho na vyombo hivyo pamoja na wanahabari, Sungura alisema ruzuku iliyotolewa inatakiwa kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba wamewaweka wakaguzi wao wa ndani watakaokagua mara kwa mara matumizi ya fedha zilizotolewa kwa nia ya kuhakikisha zinasaidia wananchi.
Ni kweli ulio wazi kwamba wananchi kutoka nchi wafadhili wanatoa fedha hizo wakitaraji kuwa vyombo vya habari vitashiriki kikamilifu kuboresha utawala wa sheria serikalini na hatimaye huduma kwa jamii yenye uhitaji mkubwa.
Kwa ufupi tu, nchi wafadhili ni Denmark, Switzerland, Norway na Uingereza kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo (Tanzania).
Sisi JAMHURI, tukiwa ni sehemu ya vyombo vilivyotia saini mkataba huo wa mwisho, tunapongeza TMF huku tukiahidi kutoa ushirikiano katika kuthamini na kuweka nidhamu kubwa ya matumizi yake.
Hatutaki kuwa mfano wa watakaofuja au kutumia vibaya ruzuku hiyo kwani katu hatutaki kujitafutia ubaya mbele ya jamii.
Tunasema hivyo tukifahamu kuwa jamii inazo changamoto nyingi hali ambayo inachangia maisha ya watu kuendelea kuwa duni, hivyo Gazeti laJAMHURI na vyombo vya habari vinatakiwa kuangalia suala hilo katika kuibua mambo mbalimbali yenye kuzaa mabadiliko.
Tunasema kwamba tunafahamu kuwa mahitaji muhimu ya binadamu hayapatikani katika jamii ikiwamo huduma za afya, shule na vitu vingine vya muhimu kutokana na changamoto za tabia za ubadhirifu.
Tunasema haya kwa sababu ya kufahamu kuwa chombo cha habari kina wajibu wa kurejesha matumaini yaliyopotea kwa jamii.
Hakika tunaahidi kufanya kazi kubwa na ili tufanikiwe, tunaomba wadau watuunge mkono kuhakikisha mashine hizi zinatumika kukusanya mapato ya Serikali.

 

3920 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!