KARATU

Na Bryceson Mathias

Mkazi wa Kijiji cha Bassodowish kilichopo Karatu, Arusha, Paskalina Ibrahimu (36), amefanikiwa kupambana na fisi na hatimaye kumnusuru mwanaye kuuawa.

Hata hivyo, pamoja na mapambano hayo, fisi alifanikiwa kunyofoa pua ya mwanaye huyo, Daniel Paskali, mwenye umri wa miaka saba, na kutoweka nayo.

Akizungumza baada ya harambee ya ujenzi wa kituo cha kulea watoto iliyofanyika mapema mwezi huu katika viwanja vya Titiwi, mama huyo ambaye ni mjane anasema tukio hilo la kutisha lilitokea siku chache baada ya kufiwa na mumewe ambaye ni baba yake Daniel.

Katika harambee hiyo, Daniel, mtoto aliyenusurika kifo, alitoa jogoo kama mchango wake wa ujenzi wa kituo hicho chenye lengo la kuwasaidia watoto kuondokana na madhara kama yaliyomkuta.

“Ni Mungu tu ndiye aliyenipa nguvu za kuinuka haraka na kupambana na fisi wa ajabu aliyeninyemelea na kumvuta miguu mtoto wangu aliyekuwa amekaa mlangoni pembeni yangu wakati ninaosha vyombo.

“Ilikuwa ni saa 12:30 jioni ya Desemba 12, 2019. Akaanza kumburuza Daniel na kukimbia naye. Nikainuka haraka, nikadaka kichwa cha mtoto kwa mkono mmoja na mkono mwingine nikawa ninampiga fisi kwa sufuria huku akimburuza mtoto. 

“Nadhani alihisi maumivu ndiyo maana akamuachia mtoto; lakini akamrukia tena mtoto na kumjeruhi kwa kunyofoa pua; akaenda nayo. Mtoto akabaki anachuruzika damu nyingi. Ilikuwa hatari sana kwa maisha ya mwanangu,” anahadithia Paskalina huku akibubujikwa machozi.

Anasema Mchungaji wa KKKT Basodowishi, Robert Temba, kwa kushirikiana na waumini, wanakijiji wenzake na watu wenye mapenzi mema, wamemsaidia kumpeleka Daniel sehemu mbalimbali kwa matibabu.

Mtoto huyo sasa amewekewa pua ya bandia na wataalamu wa Hospitali ya Serian iliyopo Arusha.

Kwa sasa Daniel ni mmoja wa wanakwaya wa Kwaya ya Watoto.

Bassodowishi ni kijiji kilichopo Kata ya Endamarariek, Karatu, na wakazi wa kijijini hapo wameiomba serikali kuzuia upigaji wa ramli chonganishi na imani za kishirikina, vitu vilivyokubuhu eneo hilo.

Kauli hiyo inachagizwa na dhana iliyopo kwamba ‘fisi wa ajabu’ (wa kishirikina) amedumu kwa miaka mitatu sasa, akiwaua na kuwala zaidi ya watoto 15, huku juhudi za kumsaka na kumuua zikishindikana.  

Akiimba wakati wa harambee hiyo, Daniel, alijikuta akituzwa Sh 78,000 na washiriki, wakimtaka mama yake amnunulie kitu cha ukumbusho wa tukio lililompata.

Akitokwa machozi, Paskalini amewashukuru washiriki hao akiahidi kwanza kupeleka kanisani sadaka ya fungu la 10, ndipo baadaye kutekeleza mapendekezo ya kumnunulia kitu cha ukumbusho.

238 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!