Anne Makinda yamfika

Uamuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Anne Makinda, wa kuwafurusha wakurugenzi na watumishi kadhaa wa Mfuko huo, unaelekea kuitia Serikali hasara ya Sh bilioni 9.
Kiasi hicho cha fedha huenda kikalipwa kwa watumishi hao ambao uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa wamesimamishwa na wengine kufukuzwa kazi kinyume cha sheria.
Muda mfupi baada ya Makinda kushika wadhifa huo, alisitiza ajira za baadhi ya watumishi kwa kile alichosema kuwa kililenga kupisha muundo mpya wa Mfuko.
Licha ya kupunguza, NHIF imewapa watumishi mikataba ya miezi sita ambao kikanuni wamekuwa wakipewa mikataba ya miaka mitatu.
Watumishi ambao ajira zao zilisitishwa mwaka jana ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando, Jackson Buhulula, Hamis Mdee, Deusdedith Rutazaa, Dk. Frank Lekey, Raphael Mwamoto, Beatus Chijumba, Ally Othman, Grace Lobulu, Constantine Makala, Eugen Mikongoti na Rehani Athumani.
Hata hivyo, katika hatua ambayo haijaeleweka bayana, watumishi wanne kati ya hao hawajataka kudai haki zao. Watumishi hao ni Athumani, Mikongoti, Mwamoto na Mdee.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa hadi Novemba, mwaka jana, wafanyakazi wanaotaka wapewe haki zao, madai yao yalikuwa Sh bilioni 9. Kiwango hicho kilitarajiwa kupanda kutokana na malimbikizo ya fedha za nauli na mizigo ya kwenda makwao.
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya Tanzania (TUGHE), Tawi la NHIF, kimekosoa hatua ya Mwenyekiti wa Bodi kusitisha ajira za watumishi hao, kikisema imekiuka kanuni na sheria za kazi.  
“Wote hawa kamwe hawakujulishwa juu ya kusitishwa ajira zao na wala Chama cha Wafanyakazi hakikushirikishwa,” kimesema chanzo chetu.
Katibu wa Mfuko, ambaye yupo kwa mujibu wa muundo wa utumishi wa Mfuko wa mwaka 2008, nafasi yake haijaondolewa kwenye muundo unaokusudiwa kutumika, lakini ajira yake imesitishwa bila kuelezwa kwa kina sababu zilizoiwezesha Bodi kuchukua hatua ya kumwondoa.
“Mwajiri ameshindwa kuonesha sababu za kusitishwa kwa ajira kwenye mkataba wa nafasi ambazo zipo kwa mujibu wa sheria, na pia ameshindwa kuonesha jinsi nafasi za kisheria zisivyo na uhusiano na kubadilika kwa muundo wa Mfuko.
“Hili pia limetokea kwa Meneja Ununuzi wa Umma ambaye nafasi yake ipo kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011,” amesema kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi.
Wakati hao wakiondolewa kwa kigezo cha kupisha muundo mpya, imebainika kuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani ameachwa aendelee na kazi licha ya nafasi yake kulindwa kisheria kama wenzake walioondolewa.
“Endapo mwajiri ataendelea na ukiukwaji wa sheria, watumishi waliositishwa ajira tunaona wana haki ya kudai fidia kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini,” kimesema Chama cha Wafanyakazi.
Mwajiri anatakiwa pia kueleza sababu za msingi zilizompa mamlaka ya kutoa notisi na kusitisha ajira ya mtumishi ambaye alikuwa likizo.
Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini kifungu cha 41(4) (a) (b) kinazuia uamuzi wa aina hiyo. “Endapo mwajiri angekuwa na taarifa za uhakika, mtumishi asingechukua likizo na wala mwajiri asingemruhusu kwenda likizo. Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria mwajiri ana wajibu wa kuthibitisha kipindi cha kumpunguza kazini kama haikuwa nia ya kudhamiria.”
Katika hatua nyingine, imebainika kuwa Bodi, ama ilishindwa, au ilipuuza kuhuisha mikataba ya muda maalumu.
JAMHURI limeelezwa kuwa kitendo hicho kimefanywa kwa Jane Kijazi, Rose Rose Ongara na Godfrey Semwenda.
“Waajiriwa wote hao walimwandikia mwajiri barua ya kudhamiria kuongeza mikataba kwa kipindi cha miaka mitatu. Pamoja na mwajiri kupokea barua zao, hakujibu na kwa namna yoyote hakuonesha kukataa maombi yao.
“Watumishi hao walikuwa na matarajio ya kuendelea na mikataba kwa kuzingatia kifungu cha 19(1)(2) cha mikataba kati yao na mwajiri, kilichoonesha wote – mwajiri na mwajiriwa – walikuwa na matarajio ya kuhuisha mikataba kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia tarehe ya mwisho ya mkataba uliomalizika kwani mwajiri, aliendelea kuwatuma kazi na kuwapa mishahara kwa kipindi chote ambacho mikataba yao iliisha,” kimesema Chama cha Wafanyakazi.
Imeelezwa kuwa mwajiri alitoa mkataba wa miezi sita kinyume cha sheria akiwa tayari ameendelea kuwapangia kazi na kuwalipa mishahara kwa kipindi cha miezi miwili zaidi.
“Kwa kuongezea, Jane Kijazi, Rose Rose Ongara na Godfrey Semwenda, kitendo chao cha kusitisha ajira zao wao wenyewe katika jicho la kisheria kinaonekana kama walilazimishwa kuandika barua za kuacha kazi kwa kuwa mwajiri aliwajengea mazingira magumu ya kazi na ajira yao; na amewafanya wasiweze kuendelea kumudu mazingira ya kazi kwa kuwa ni vigumu kwa mtumishi kuendelea kufanya kazi huku akijua hana uhakika wa ajira na hataweza kufanya kazi kwa furaha,” kimesema Chama cha Wafanyakazi.
TUGHE imesema endapo Bodi ya NHIF inataka haki itendeke kwa pande zote mbili – mwajiri na waajiriwa – suala hili lifikishwe katika Mahakama au katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
Kutokana na msimamo huo, Agosti, mwaka jana, TUGHE ilimwandikia barua mwajiri na kusema: “Tunatumaini kuwa ofisi yako itatumia kila jitihada kuhakikisha kuwa haki ya wanachama wetu inalindwa na kupatikana kwani usitishwaji huu wa ajira zao haukuwa wa haki, labda mwajiri arejee upya utaratibu wa kisheria kuhusu uamuzi wake.”
Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la NHIF, Gabriel Ishole, anasema wanachama wao waliositishiwa ajira hawajaridhika, hivyo ni wajibu wa Bodi yenyewe kuwasilisha malalamiko CMA au mahakamani mapema iwezekanavyo kwa mujibu wa sheria.
Baada ya kuona suala hili ‘limekaa vibaya’, wiki kadhaa zilizopita Bodi ya NHIF chini ya Mama Makinda, Machi 23 na 24, mwaka huu ilikutana jijini Dar es Salaam, dondoo kuu ikiwa kuzungumza na watumishi walioondolewa kazini. Lengo lilikuwa kutaka kujua kile kinachodaiwa na watumishi hao! Wakati Bodi ikikutana, tayari suala hilo lipo CMA.
“Wakati wa mediation (upatanishi)mwajiri alibembelezwa sana juu ya kumaliza suala hili amicably (kiungwana) lakini hakuonesha juhudi zozote. Baada ya suala kufika hatua ya arbitration (usuluhishi) ndipo akashtuka kujua sasa jambo hili litakuwa wazi kwa ‘public’ nzima maana kwenye ‘arbitration’ mtu yeyote anaweza kuja kusikiliza shauri.
“Mpaka leo hii (Mei, 2017) karibu mwaka mzima sasa bado muundo unaotumika ni ule ule wala hakuna muundo mpya kama alivyodanganya Mwenyekiti wa Bodi. Nafasi zinakaimiwa na watu wengine kwa muundo ule ule wa zamani,” kimesema chanzo chetu kutoka NHIF.
Julai, mwaka jana, Mama Makinda alizungumza na waandishi wa habari na ‘kukanusha’ taarifa ya kwamba watumishi hao waliondolewa baada ya kuwapo wizi wa Sh bilioni 3 za NHIF mkoani Mara.
Badala yake, alisema kuondolewa kwao kulikuwa mahsusi ili kupisha muundo mpya wa NHIF na wengine mikataba yao ilikuwa imekwisha.
“Sisi tunashangaa kuona ukiukwaji huu mkubwa wa sheria unafanywa na Mwenyekiti wa Bodi ilhali kuna mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na pia katika Wajumbe wa Bodi kuna mjumbe kutoka Chama cha Walimu Tanzania ambaye anapaswa kujua taratibu na sheria za kazi. Swali, ilikuwaje haya yakafanywa na yeye akiwa kwenye Bodi?” Amehoji mmoja wa watumishi.
Mama Makinda ameulizwa na JAMHURI kuhusu sakata hili, na mwanzo akawa tayari kutoa ufafanuzi wa kina baada ya kurejea Dar es Salaam.
Aliahidi kuwa baada ya kufika Dar es Salaam angempigia simu mwandishi, lakini hakufanya hivyo. JAMHURI lilimtafuta, lakini hakupokea simu ndipo akaandikiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) na yeye akajibu:
JAMHURI: Mheshimiwa shikamoo. Rejea mazungumzo yetu wiki iliyopita. Uliahidi tungeweza kuonana. Nimepiga simu mara kadhaa hukupokea. Tuna habari inayokuhusu wewe kama Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF na wafanyakazi waliosimamishwa/waliofukuzwa. Tungependa kusikia kutoka kwako kabla ya kuichapisha.
MAMA MAKINDA: Nashukuru kwa ujumbe ulioniletea. Lakini simu hujapiga kwani sijaona missed call hata moja. Suala hili lipo CMA. Mimi nisingependa, kwa hatua hii, kuanza kusema nje ya vikao hivyo. Iwapo ninyi mnapenda kuandika ni uamuzi wenu. Jambo hili lipo CMA.