Jumamosi iliyopita, Rais John Pombe Magufuli alivisifia vyombo vya habari. Alisema habari zinazotangazwa na vyombo vya habari zinaisaidia mno Serikali kuboresha utendaji wake. Kwa maneno mazito, Rais Magufuli alisema: “Mmetusaidia sana Serikali hii, naomba msichoke. Naomba msichoke. Mnatoa elimu ya kutosha, mnatoa maelekezo ya kutosha, na sisi ndani ya Serikali huwa tunafuatilia.”

Kauli hii ya Rais Magufuli imeleta faraja ya aina yake kwa wanahabari. Watangulizi wake walikuwa na kauli za kwamba “Serikali haiendeshwi kwa taarifa za magazetini” au nyingine kwamba “Kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala” na nyingine kuwa vyombo vya habari “vinatumiwa kuichimba Serikali”. Zilikuwa kauli za kukatisha tamaa kwa kiwango kikubwa.

Viongozi wengi waliotangulia kazi yao ilikuwa ni kuvichanganisha vyombo vya habari na wananchi mikutanoni. Sisi wa JAMHURI, ukiacha ukweli kwamba katutaja moja kwa moja kuwa habari yetu ya uchunguzi juu ya kusitisha matumizi ya Flow Meters imeifumbua macho Serikali, tumefarijika kusikia kauli ya Rais akisifia kazi ya waandishi wa habari na kuwa wasichoke kutafuta ukweli na kuuchapisha.

Rais Magufuli anajenga matumaini mapya si tu kwa tasnia ya habari ambayo ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa, bali pia kwa nchi nzima. Kwamba vyombo vya habari akiviwezesha kuwa na sheria inayowabana watoa habari wakawajibika kutoa habari badala ya kutumia mhuri wa ‘SIRI’ kuficha ukweli wenye maslahi kwa jamii, Rais ataendesha nchi kwa starehe.

Serikali ikiruhusu vyombo vya habari kuwa huru, vikalindwa na sheria vinapoandika habari za kweli zisizo za kubuni, itakuwa haihitaji kuwa na polisi wengi. Kama ni mapato kuvuja au ukwepaji kodi, vyombo vya habari vitaonesha yanavujia wapi na Serikali itadhibiti kama ilivyofanya kwa Kampuni ya Lake Oil iliyoidai Sh bilioni 8.5 zikiwa kodi ilizokwepa baada ya gazeti hili kuchapisha habari zao.

Rais Magufuli ameanza kuzungumza lugha inayojenga matumaini mapya. Anasema Tanzania si nchi masikini kwani ina rasilimali za kutosha, tofauti na mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete, aliyesema hajui kwa nini Tanzania ni masikini. 

Tunasema Rais atusaidie kupitisha sheria nzuri za vyombo vya habari, sisi tutashirikiana naye kusukuma ajenda ya kuwaondoa Watanzania katika umasikini. Mungu ibariki Tanzania.

1261 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!