JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

Mshindi wa Tuzo ya Amani, mpigania uhuru maarufu na mpinzani wa ubaguzi wa rangi, Askofu Mkuu Desmond Mpilo Tutu wa Afrika Kusini, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90.

Tutu, ambaye kwa miongo kadhaa alishiriki kikamilifu mapambano dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi za utawala wa weupe wachache nchini humo, amefariki dunia Jumapili ya Desemba 26.

Akitangaza taarifa hizo, Rais Cyril Ramaphosa, amesema kifo cha mtumishi huyo wa kanisa ni maadhimisho mengine ya misiba ya kizazi muhimu cha Afrika Kusini.

“Askofu Tutu alikuwa msaada mkubwa katika kuturithisha taifa lililokombolewa, akiwa mmoja wa viongozi maarufu ndani na nje ya nchi,” amesema Rais Ramaphosa.

Alishiriki katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi kwa nguvu moja na kuchochea harakati za kukomesha sera ya ubaguzi iliyotekelezwa na serikali ya Wazungu wachache dhidi ya weusi walio wengi kuanzia mwaka 1948 hadi 1991.

Historia haikumtupa mkono kwa kuwa mwaka 1984, Askofu Mkuu Tutu alitunukiwa tuzo ya Nobel kwa mchango wake katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Tutu amefariki dunia wiki chache baada ya Rais wa mwisho wa enzi za ubaguzi wa rangi, Frederick de Clerk, kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 85.

Raia wote wa Afrika Kusini, weupe kwa weusi, walimchukulia Tutu kama ‘dhamira njema’ ya taifa huku yeye mwenyewe akiitumia imani yake kusaidia kurejesha mapatano katika taifa lililokuwa limegawanyika.

Katika mahubiri yake alipinga wazi utawala wa mabavu wa Wazungu wachache na hata ulipofika kikomo, hakuacha kupambania Afrika Kusini yenye usawa.

Katika siku zake za mwisho alikuwa akisikitika kwamba ndoto yake ya ‘Taifa la Upinde wa Mvua’ (Rainbow Nation) haijatimia.

Kimataifa, mwanaharakati huyu wa haki za binadamu alikuwa akizungumzia masuala mbalimbali kuanzia Waisraeli kuikalia kimabavu Palestina hadi haki za mashoga; mabadiliko ya tabia nchi na mauaji ya ‘upendo’.

Alitumia nafasi yake ya juu katika Kanisa la Anglikani duniani kuelezea matatizo ya raia weusi wa Afrika Kusini.

Alipoulizwa wakati akistaafu uaskofu mkuu wa Cape Town mwaka 1996 iwapo ana kitu chochote anajutia, Tutu alisema: “Kuna nyakati mapambano yalimfanya mtu kuonekana kama vile hawajali wengine. Ninatumaini kuwa niliowaumiza watanisamehe.”

Katika miaka ya 1980, Tutu alisafiri sana duniani na kuonekana kama sura ya vuguvugu la wapinga ubaguzi wa rangi nje ya nchi yake wakati viongozi wa chama kilichochukuliwa kama ni cha waasi (ANC), kama Nelson Mandela, wakiwa wamefungwa.

“Nchi yetu inateketea na kuvuja damu kwa hiyo ninaiomba jumuiya ya kimataifa kuiwekea vikwazo serikali (ya Afrika Kusini),” alisema Tutu mwaka 1986.

Hata kama serikali mbalimbali hazikumjali, juhudi zake zilisaidia kuanzisha vuguvugu dhidi ya ubaguzi wa rangi katika ngazi za chini duniani kote kupinga ubaguzi kwa vikwazo vya uchumi na kitamaduni.

Katika barua yake kwa Askofu Tutu ya Machi, 1998, Rais Mzungu aliyekuwa akitekeleza ubaguzi wa rangi kwa nguvu zote, P.W. Botha, alimuuliza kama alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya Ufalme wa Mungu au kwa ahadi ya ufalme wa chama kilichopigwa marufuku wakati huo, ANC, ambacho sasa ni chama tawala.

Miongoni mwa kazi ngumu alizokuwa akizifanya ni kuhubiri wakati wa maziko ya watu weusi waliouawa kikatili wakati wa kupinga ubaguzi wa rangi.

“Tumechoka kuja makaburini kuhutubia wiki baada ya wiki. Wakati umefika sasa wa kuacha kupoteza maisha ya watu,” amewahi kusema Tutu.

Alisema msimamo wake dhidi ya ubaguzi wa rangi ni wa kimaadili zaidi kuliko kisiasa.

“Ni rahisi sana kuwa Mkristo hapa Afrika Kusini kuliko sehemu nyingine yoyote, kwa kuwa masuala ya kimaadili yapo wazi zaidi nchini humu,” amewahi kuliambia Shirika la Habari la Reuters.

Februari 1990, Tutu alimwongoza Nelson Mandela kwenye kidirisha (balcony) cha Cape Town’s City Hall kutoa hotuba yake ya kwanza hadharani baada ya kukaa gerezani kwa miaka 27.

Miaka minne baadaye alikuwa pembeni ya Mandela wakati akiapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.

“Sauti ya Desmond Tutu itabaki daima kuwa sauti ya wanyonge. Sauti ya watu wasio na sauti,” hivi ndivyo Mandela, aliyefariki dunia Desemba 2013, alivyomwelezea rafiki yake, Askofu Tutu.

Wakati Mandela akitangaza demokrasia nchini Afrika Kusini, Tutu ndiye aliyeongoza Tume ya Ukweli na Maridhiano iliyouweka wazi ukweli kuhusu vita dhidi ya utawala wa weupe wachache.

Mbele ya tume hiyo kulitolewa ushuhuda ambao ulimtoa machozi Askofu Tutu hadharani.

Lakini Tutu alikuwa imara kwenye demokrasia kama alivyokuwa dhidi ya watawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini.

Aliwakosoa viongozi wapya kwa kuendeleza yaliyokuwa yakifanywa na watangulizi wao kwa kujipendelea huku akilaumu uhusiano wa muda mrefu hadharani kati ya Mandela na Graca Machel, ambaye baadaye alimuoa.

Katika taarifa ya tume yake, Tutu aligoma kuwatendea ‘kilaini’ watawala wa ANC, hivyo akaendeleza msimamo kama aliokuwa nao dhidi ya watawala wasiotenda haki.

Hata uzeeni mwake, hakuacha kuzungumzia kero zilizopo, ikiwa ni pamoja na kumlaani Rais Jacob Zuma kuhusu tuhuma za ufisadi.

Mwaka 2014, alikiri kwamba hakuipigia kura ANC, kutokana na sababu za kimaadili:

“Nina masikitiko kwa kuwa nilidhani uzee wangu utakuwa wa furaha, siku za kusifia na kuwashauri viongozi vijana wanaofanya mambo mema,” anasema Tutu, Juni 2014.

Desemba 2003, aliikosoa serikali yake kwa kumuunga mkono aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, pamoja na kudaiwa kukiuka haki za binadamu.

Alitangazwa kuwa Askofu Mkuu wa Kwanza Mweusi wa Cape Town mwaka 1986, na kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani Afrika Kusini. Alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 1996.

Baada ya kustaafu alipata matatizo ya tezi dume na kuacha kuonekana hadharani. Katika moja ya matukio ya mwishoni kuonekana ni pale alipokuwa mwenyeji wa Prince Harry wa Uingereza na mkewe Meghan pamoja na mtoto wao aliyekuwa na umri wa miezi minne, Archie, jijini Cape Town, Septemba 2019, akiwasifu wenzi hao kama watu wanaojali sana.

Tutu alimuoa Leah mwaka 1955. Wawili hawa wana watoto wanne na wajukuu kadhaa.

By Jamhuri