Na Nizar K Visram

Maandamano na mgomo wa wakulima zaidi ya 100,000 nchini India hatimaye umemalizika baada ya serikali kukubaliana na madai yao. 

Wakulima hao walipiga kambi nje ya mji mkuu wa New Delhi, wakitaka serikali ibatilishe sheria tatu ambazo walidai zitabinafsisha uuzaji wa mazao yao na kuzipa kampuni kubwa uwezo wa kuyanunua kwa bei ya chini. 

Matokeo yake ni kampuni hizo kuvamia na kudhibiti sekta ya kilimo nchini India. Hatimaye ni kuhatarisha maisha ya wakulima wadogo zaidi ya milioni 800  nchini.  

Novemba 19, mwaka huu, Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India, alitangaza kuwa atafuta sheria hizo tatu zilizopitishwa na Bunge Septemba 2020 kwa haraka na bila ya mjadala. 

Tangazo la kufuta pia lilikuja ghafla, bila ya mjadala bungeni wala mkutano wa Baraza la Mawaziri.

Ilichukua dakika chache kwa mabunge mawili ya India kubatilisha. Vyama vya upinzani vilitaka kujadili lakini Chama tawala cha BJP kilikataa. 

Tangazo la Modi lilikuja wakati wakulima wakijitayarisha kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano yaanze Novemba 26, mwaka jana. Siku hiyo walikuwa wanaelekea New Delhi walipokumbana na polisi waliotumia maji ya kuwasha na mabomu ya kutoa machozi. Wakazuiwa kuingia New Delhi na tangu wakati huo wakapiga kambi katika vitongoji vya jiji hilo.

Swali moja linaulizwa. Ilikuwaje Modi akakubaliana na madai ya wakulima na ilhali kwa muda wa mwaka mzima yeye na wasaidizi wake wamekuwa wakiwalaani na kuwashambulia? Wachambuzi wanasema ameamua kugeuza msimamo wake kwa sababu za kisiasa.  

Wakulima wakati wanaandamana walikuwa tayari kufanya mazungumzo na serikali. Ndiyo maana wakachagua kamati yao ya uongozi ambayo ilikutana na wakuu wa serikali mara 11. Serikali haikuwa tayari kutimiza matakwa ya wakulima na maandamano yakaendelea usiku na mchana.

Bila ya kutumia nguvu, wakulima zaidi ya 100,000 walilala katika viunga vya New Delhi, huku serikali ikitumia mbinu za kuwakatia maji na umeme, pamoja na kuwakatia mawasiliano ya simu na mtandao. Hata hivyo wakulima hawakuvunjika moyo. Wakati wote kaulimbiu yao ilikuwa: “Kilichoamuliwa bungeni tutakibatilisha mitaani.”

Umuhimu wa akina mama katika kazi za shambani ulijitokeza waziwazi wakati wa maandamano. Ingawa asilimia 80 ya kazi shambani huwa inafanywa na wanawake, ni nadra wao kumiliki ardhi au kupata mikopo ya benki. Licha ya yote haya wanawake walionekana wakiwa mstari wa mbele katika maandamano.

Kitu kingine ambacho kilijitokeza ni umoja na mshikamano. Nchini India, hasa vijijini, jamii huwa imegawanyika katika matabaka ya kurithi. Mtu anazaliwa katika tabaka la mwenye nacho na la asiye nacho. Ni mfumo wa ukabaila wa kijadi (caste system). Lakini katika maandamano haya tofauti hii haikuonekana. 

Wanaomiliki vijishamba na wanaowauzia jasho lao waliungana dhidi ya sheria tatu. Watawala walijaribu kuwagawa kwa misingi ya dini au kabila lakini hawakufanikiwa.   

Wakulima walikuwa na vyama 40. Wakaungana na kuunda shirikisho moja (SKM) likiongozwa na Rakesh Tikait. Wakaandika barua kwa waziri mkuu wakitaka sheria tatu zibatilishwe kupitia Bunge. 

Hata hivyo, wakasema wana madai mengine sita, matatu kati yao yamekuwapo kwa muda mrefu. Ni pamoja na sheria ya kupanga bei ya mazao kwa wakulima wote na kwa mazao yote. Lengo ni wakulima wawe na uhakika wa bei, isiwe chini ya ile iliyopangwa (MSP).  

Barua hiyo pia imetaka serikali ibatilishe sheria inayoondoa ruzuku ya umeme kwa wakulima, na wanafamilia walipwe fidia ya waandamanaji zaidi ya 700 waliofariki dunia. 

Wanataka pia mashitaka dhidi ya waandamanaji yafutwe. Pia wametaka mtoto wa waziri achukuliwe hatua za kisheria kwa kuwakanyaga waandamanaji kwa gari lake.  

Si hayo tu, bali wanataka serikali ya Modi ifute sheria ya uraia (Citizenship Amendment Act) ambayo imekuwa ikipingwa kote nchini kwa muda mrefu. 

Hii ni sheria inayowabagua raia kwa misingi ya dini zao, kinyume cha katiba ya nchi iliyotungwa tangu India ilipopata uhuru mwaka 1947.

Hii inadhihirisha kuwa wakulima walikataa kugawanywa chini ya itikadi za kikabila au kidini au kimajimbo. Watawala walijaribu kutumia itikadi yao ya kidini (Hindutva) ili kuvunja muungano wa wakulima. Hata hivyo umoja wa wakulima (SKM) ulifanikiwa kuitisha mkutano mkuu wa wakulima wa nchi nzima tarehe 5, Septemba (Kisan Mahapanchayat).

Mkutano huo ulionyesha wazi kuwa wakulima si tu walikuwa wakipinga sheria tatu, bali itikadi nzima ya kibaguzi. Walikuwa wanataka India iendelee kuwa na mfumo wa kisekula unowajali raia wote.

Mbinu moja iliyotumika kuwagawa wakulima ni ya ukabila.  Wengi wao walitoka Jimbo la Punjab na ni wa kabila la Singa Singa. 

Wakashambuliwa kuwa wao ni wafuasi wa kundi la Singa Singa wanaotaka kujitenga kutoka India na kuunda taifa lao (Khalistan). Ni vuguvugu hili ndilo lilisababisha kuuawa kwa aliyekuwa waziri mkuu, Indira Gandhi mwaka 1984.

Mbinu hii haikufanikiwa, kwani kiongozi, Rakesh Tikait, hakutoka Jimbo la Punjab bali ametoka Uttar Pradesh. Hakuzungumza lugha ya ukabila au ya udini bali ya tabaka la wakulima. Haikuwa rahisi kuwaunganisha wakulima laki moja kwa muda wa mwaka mmoja, lakini yeye na kamati yake walifanikiwa. 

Mbinu ya kuwapachika waandamanaji lakabu ya Khalistan haikufanikiwa kwa sababu wengi wao hawakutoka Punjab bali walitoka majimbo ya Haryana, Rajasthan, Uttar Pradesh na kwingineko. Mbinu ya Hindutva pia haikufua dafu, kwa sababu walikataa propaganda za kikabila na kidini.

Maandamano ya wakulima yameathiri Chama tawala cha BJP. Waziri Mkuu Modi alitanabahi haya na ndipo akaamua kukubaliana na matakwa yao ili kukiokoa chama chake. Kwani katika uchaguzi wa kienyeji hivi karibuni chama hicho kilipoteza kura nyingi isipokuwa tu katika Jimbo la Assam.

Kilichofanyika ni kuwa umoja wa wakulima (SKM) uliendesha kampeni ikisema: “Tuiadhibu BJP” katika majimbo kama Uttar Pradesh, Punjab na Uttarakhand. 

Hii ikaiathiri vibaya BJP. Hali ilizidi kuwa mbaya wakati mtoto wa waziri, Ajay Mishra, aliposababisha vifo vya waandamanaji wanne kwa kuwagonga na gari lake. Hii ikazidisha hasira miongoni mwa wakulima 

James Manor, mchambuzi wa siasa anasema Modi amehodhi uwezo mkubwa ndani ya BJP kiasi kwamba anachokisema yeye hakipingiki. 

Maandamano haya ya wakulima yametikisa uwezo huu hasa baada ya Modi kukubali kubatilisha sheria tatu. Watu sasa wameanza kumkosoa na vyama vya upinzani vimeanza kutumia mwanya huu ili kujipatia kura.

Pia kuna chaguzi za kienyeji zitakazofanyika karibuni katika majimbo matatu muhimu yaliyo karibu na New Delhi, nayo ni Punjab, Uttarakhand na Uttar Pradesh. Modi asingependa apoteze kura kama alivyopoteza katika majimbo ya Haryana, Himachal Pradesh na Rajasthan.

Yaani katika majimbo matatu BJP tayari imepoteza kura na kama maandamano yangeendelea, kuna uwezekano hali hiyo ikajirudia katika majimbo mengine matatu.  Majimbo haya sita ndiko walikotoka wakulima walioandamana kwa muda wa mwaka mzima.

[email protected]

0693-555373 

By Jamhuri