Wawekezaji waigomea Serikali

DAR ES SALAAM

Na Dennis Luambano

Baadhi ya wamiliki wa hoteli na ‘campsites’ zilizopo mwambao wenye urefu wa takriban kilomita saba wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara iliyopo jijini Arusha wamegoma kuwasilisha serikalini nyaraka zinazoonyesha umiliki wa ardhi, kibali cha ujenzi cha kuta na tathmini ya athari za uharibifu wa mazingira.

Awali, wawekezaji waliojenga kuta na kusababisha bughudha kwa wanyamapori walitakiwa kupeleka nyaraka hizo kwa Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Raphael Siumbu.

Kuta fupi na ndefu zimejengwa na kuziba ushoroba (njia) wa wanyama wanaopatikana Ziwa Manyara na kusababisha vifo vya baadhi yao kwa kukosa maji na malisho wanapoingia ndani ya maeneo hayo.

Tarehe ya mwisho kuwasilisha nyaraka ilipangwa kuwa Desemba 6, mwaka huu. 

Agizo la Siumbu limekuja baada ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, kufanya ziara ya kikazi katika Kijiji cha Migungani B, Mto wa Mbu wilayani Monduli na kushiriki uvunjaji wa baadhi ya kuta za campsite kuruhusu wanyama kuendelea kuishi katika ikolojia ya mwambao wa hifadhi bila kubugudhiwa.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI wiki iliyopita, Siumbu, amesema hadi sasa bado wanachunguza kuona ujenzi wa kuta hizo umefikaje hapo.

“Kwa sababu kama mtu haujafanya uchunguzi hauna haki ya kusema chochote, kwa hiyo tunachunguza tumefikaje hapo. Tulianza lini hadi tumefikia hapo. Ndiyo, DC hajui. Ni mgeni, hata mimi ni mgeni hivyo hivyo ndiyo maana tunachunguza haya yalianza lini, tumefikaje hapa tulipofikia?

“Sasa mimi kwa ugeni huu siwezi nikakurupuka nikaanza kuhukumu mambo ambayo nayaona hapa kwa macho, ni lazima nijue imetokea wapi? Nani amehusika kuwapa vibali hadi tumefika hapa,” anasema.

Siumbu anasema yeye na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisume, wamekwenda katika hoteli na campsite hizo kuangalia hali ilivyo ndipo akachukua hatua ya kuwaagiza wahusika kupeleka ofisini kwake nyaraka na vibali vilivyowapa uwezo wa kujenga kuta.

“Baadhi yao wameleta nyaraka na wengine bado hawajaleta. Kwa hiyo wakishafanikiwa kuleta nitafanya uchunguzi wa kina kuona tumefikaje na nani ametoa hicho kibali kama kweli kipo.

“Na kama mtu hana kibali, basi tutachukua hatua nyingine, kwa hiyo niliwapa muda wa kuleta na walioleta tayari wameleta na ambao hawajaleta, basi tutaona hatua za kufanya baada ya hapo.

“Mimi nilitoa tangazo kwa waliojenga maeneo hayo, nilitoa tangazo la jumla. Sijaweza kuchukua idadi ya watu walioleta nyaraka zao ila taarifa nilizonazo kutoka ofisini ni kwamba baadhi wameshaanza kuleta na wengine bado. Niliwapa muda wa mwisho kuleta ni Jumatatu ya wiki iliyopita.”

Hata hivyo, anasema hana idadi kamili ya hoteli na campsite zilizopo eneo hilo kutokana na upana na ukubwa wake kwa sababu hajazihesabu.

Anasema hoteli na campsite ziko nyingi lakini baadhi zinavunja sheria na kanuni za uhifadhi.

“Kuwapo campsite si tatizo hata kidogo. Tatizo ni kuvunja sheria za ujenzi. Kwa hiyo campsite ziko nyingi sana, tatizo ni kwamba baadhi yao ndani yake wamejenga kuta ndefu zikafunga huo ushoroba.

“Sasa huko kujenga hizo kuta ndilo tatizo, lakini kuwapo campsite si tatizo. Katika ujenzi mle ndani lazima uzingatie sheria za uhifadhi, unaweza kuwa na campsite fulani iko mle ndani lakini hajakiuka masharti ya ujenzi na nyingine ipo lakini imekiuka masharti ya ujenzi, sasa lazima ufanyike uchambuzi, nani amekiuka na nani hajakiuka,” anasema.

Pia anahoji imekuwaje hao wamiliki wakiuke utaratibu kwa sababu kujenga mwambao wa ziwa ni lazima tathmini za athari ya uharibifu wa mazingira zifanywe na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Kutokana na hali hiyo, anasema ndiyo maana anataka wamiliki wampelekee nyaraka zao.

“Nataka kujua nani amempa hilo eneo, anionyeshe documents za aliyempa eneo huyu hapa, nani amempa hati ya umiliki wa ardhi anionyeshe, lakini tatu; anionyeshe kwa sababu eneo lile ni lazima liwe na tathmini ya athari za mazingira.

“Anionyeshe hizo documents kutoka NEMC au mamlaka inayohusika kufanya tathmini ya mazingira, anionyeshe documents zote hizo zinazohusika. Sasa huo uchambuzi wa jumla ndio utakaotuambia, maana anaweza kuwa upande mmoja ana kibali halali lakini upande wa pili hana kibali halali, sasa hayo yanahitaji uchambuzi wa kina,” anasema.

DC Mwaisume ameliambia JAMHURI wiki iliyopita kuwa wamiliki wa hoteli na campsite hizo wamejenga kuta kwa kuwa kila mmoja anataka kutumia fursa ya Ziwa Manyara na kujikuta wakizuia ushoroba.

“Kwa kufanya hivyo upande ule ambao ni kusini tuseme ambako ndiko wanyama wanatokea kwa sababu hapo ndipo kuna ushoroba.

“Wanapotokea kule na wanataka kuja wanapita kandokando ya ziwa halafu wapitilize kwa sababu ni ushoroba ambao unapita moja kwa moja kwenda upande huu wa Monduli na kwenda katika Msitu wa Mingoli hadi Ziwa Natroni kwa ajili ya magadi kisha wakatishe ama warudi Ngorongoro au waende Kenya huko karibu na West Kilimanjaro,” anasema.

Mwaisume anasema katika maeneo yote hayo wamiliki ama wawekezaji hao wamejenga bila kufuata utaratibu wa ujenzi katika ushoroba wa wanyama.

“Hawatakiwi kufanya hivyo, kama unaweka campsite au unajenga hoteli weka lakini usiweke uzio ili wanyama wawe na uwezo wa kupita na waendelee na safari zao. 

“Sasa wao wamezuia kabisa, tena wamejenga ukuta kabisa na wengine wamejenga kuta ndefu na wengine fupi na katika kuta fupi wakiruka na kuingia ndani wanajikuta wameingia katika vichochoro na hawawezi kurudi tena wala kupitiliza.

“Kisha wanatangatanga na kuanza kwenda katika majalala na wengine wakikosa malisho na maji wanakufa kwa hiyo utakuta mwambao wote huo wamezuia,” anasema.

Katika hatua nyingine, serikali imetoa agizo la kusitisha ujenzi holela wa kuta katika eneo la ziwa hilo. 

Agizo hilo limetolewa na Masanja alipofanya ziara ya kikazi hivi karibuni katika eneo hilo.

“Naelekeza uzio wote uliojengwa kuzunguka hili ziwa uvunjwe na mwekezaji yeyote tutakayemsikia anajenga uzio tutamchukulia hatua za kisheria,” anasema.

Pia anasema kumekuwa na migogoro mingi kati ya wananchi na hifadhi baada ya kuvamia maeneo ya wanyama inayosababisha watu hao kuvamiwa na wanyama wakali kama tembo na kuwataka kuchagua maeneo mazuri ya kuishi.

“Ifike mahali wananchi wahamie katika maeneo ambayo watakaa bila kubughudhiwa,” anasema. 

Masanja anasema katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali ina mpango wa kufanya tathmini ya mapito yote ya wanyama na wananchi wawe tayari kuyaachia ili kukuza utalii hapa nchini.

“Nakuelekeza mkurugenzi, fanyeni tathmini katika mapito yote ya wanyama ili kujua majengo na mali zote zilizopo ili tuwahamishe wananchi kwa kuwapa fidia ili wanyama hawa waweze kupita,” anasema.

Pia amewaagiza maofisa uhifadhi kufanya operesheni ya kuwatoa wanyama walionasa katika vizuizi vya kuta za hoteli na campsite zilizopo mwambao wa ziwa hilo.

“Naelekeza maeneo yote yenye hawa wanyama uwepo ulinzi, na ninaelekeza kabla mwezi huu haujaisha watoeni hawa wanyama walio katika vizuizi ili wawe huru,” anasema.