maandaMaanda Ngoitiko ambaye ni kiongozi wa asasi ya Pastoral Women Council (PWC), wakati wowote wiki hii atapewa tuzo ya Front Line Defenders Award for Human Rights inayotolewa na Shirika la The International Foundation For the Protection of Human Rights Defenders at Risk mjini Dublin, Ireland.

Mimi William Mosongo Alais – Diwani wa Kata ya Oloipiri na Ndugu Gabriel Kamomon Olle Killel – Mkurugenzi wa Shirika la KIDUPO Integrated Development Peoples’ Organization, tunakosoa utoaji wa tuzo hii kwa Maanda.

Hii tuzo haina ukweli wowote na faida kwa wafugaji wa Kimaasai. Amebebwa kupata tuzo hiyo na Susanna Nordlung, raia wa Sweden ambaye ni mmoja wa wavurugaji wakuu wa amani katika Loliondo, wakisaidiwa na kampuni ya Ndorobo Safaris.

Maanda ametumiwa na wajanja hao kupata tuzo kwa ajili ya maslahi binafsi ya hao waliopo nyuma ya pazia ambao ni DoroboSafaris na Susanna Nordlund. Hawa wanakusanya mamilioni ya fedha duniani kote na kuyafaidi kwa mgongo wa Wamaasai. Hii tuzo ni kama asante yao kwa Maanda kwa juhudi zake za kuifanya Loliondo isitawalike.

Kwa masikitiko makubwa, Maanda Ngoitiko amepata tuzo hiyo kwa njia ya kutuhumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mashirika yake ya umma kama vile TANAPA na Ngorongoro (NCAA), Thomson Safari, Ortello Busines Corporation, KIDUPO na Diwani wa Kata ya Oloipiri dhidi uporaji wa ardhi ya Wamaasai kama sehemu ya kupata pesa kutoka mashirika mbalimbali ya wafadhili na wahisani bila kusaidia jamii kwa pesa zilizopatikana.

Kwa mfano mwaka 2011 shirika la Pastoral Women Council of Tanzania (PWC) chini ya uongozi wa Maanda Ngoitiko alipata Sh 885,242,212 na mwaka 2012 alipata dola 717,521 za Marekani (Sh 1,112,158,137) bila kufanya miradi yoyote yenye tija ndani ya vijiji alivyoombea pesa hizo. Tunajiuliza, je utetezi huu wa Maanda ni wa dhati au ni wa kunufaika na migogoro anayoanzisha katika Tarafa ya Loliondo? Tunajiuliza tena kama Maanda anapigania kweli ardhi ya vijiji kama anavyodai kwenye tuzo, ni kwa nini anahamasisha na kushinikiza wahamiaji kutoka Kenya na kutoka vijiji ndani ya Tarafa ya Loliondo alivyopora ardhi yao yeye mwenyewe kuhamia maeneo katika vijiji vingine visivyo vyao bila kufuata utaratibu?

Maanda Ngoitiko amepata tuzo hii kwa hujuma na sisi tunaamini kwamba bado ana ajenda ya siri. Sisi tunataka kusema yafuatayo juu ya Maanda Ngoitiko na tuzo yake:

Mimi diwani wa Kata ya Oloipiri napenda kukanusha maneno ya uongo yaliyosemwa na Mheshimiwa Maanda Ngoitiko ili kuhalalisha kustahili kupewa tuzo kama ifuatavyo:

(1) Ninakanusha kuwa Mheshimiwa Maanda hakuzaliwa katika Kata ya Oloipiri, Kijiji cha Sukenya na wala baba yake hakuzaliwa wala hakuzikwa katika Kijiji cha Sukenya. Kiukweli ni kwamba Maanda Ngoitiko amezaliwa katika Kijiji cha Kirtalo, Kitongoji cha Olosirua katika Kata ya Soit-Sambu na pia baba yake amezikwa katika Kijiji cha Kirtalo.

(2) Kuhusiana na tuzo: Sisi tunasema kwamba Maanda Ngoitiko si mtetezi mkweli wa ardhi kwa jamii ya Wamaasai kama inavyosemekana katika tuzo, bali ni mporaji wa ardhi ya Waamasai. Kwa mfano, amejikatia eneo la karibu ekari 3,000 na kuweka uzio katika eneo la Irmasilig, Kata ya Soit- sambu katika Kijiji cha Mundorosi ambako kulikuwa maeneo ya malisho kwa wananchi wa Kijiji cha Mundorosi na Engusero-sambu na hivyo kusababisha mgogoro mkubwa wa ardhi uliosababisha mauaji ya ndugu yake.

Pili, uporaji wa ekari zaidi ya 3,000 uliyofanywa na Maanda ulisababisha kukosekana kwa maeneo ya malisho hivyo kusababisha migogoro ya malisho katika vijiji vingine vilivyotenga maeneo maalumu kwa ajili ya malisho ya mifugo yao. Mfano ni katika Kijiji cha Oloipiri.

 (3) Sisi tunasema Maanda Ngoitiko si mtetezi (activist) wa ardhi ya Wamaasai kama tuzo inavyodai, bali amekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi kati ya vijiji na vijiji, kwa mfano, Kijiji cha Sukenya na Mundorosi na pia kati ya Kijiji cha Kirtalo na Kijiji cha Oloipiri.

Maanda amekuwa mchochezi kati ya koo za Kimaasai. Kwa mfano, koo za Laitayok na koo ya Purko; na pia kati ya koo za Loita na Loitayok katika Kijiji cha Sukenya.

Amekuwa akiibua migogoro baina ya wawekezaji na wananchi. Kwa mfano, vijiji vilivyo karibu na shamba la TCL na vijiji vilivyo karibu na kitalu cha uwindaji cha OBC.

Maanda Ngoitiko amekuwa mchonganishi na mchochezi baina ya serikali na wananchi, kwa mfano, amekuwa akichochea maandamano ya vikundi vya wanawake dhidi  Serikali juu ya masuala ya ardhi.

Maanda Ngoitiko si mtetezi wa Wamasai kuhusu masuala ya ardhi, bali ni mfanyabiashara anayetegeneza migogoro ya ardhi ili kunufaika yeye binafsi na migogoro hiyo, shirika lake pamoja na wadau wa mtandao wa shirika lake wamefanikisha, kwa mfano, ufunguzi wa kesi ya Sukenya dhidi Tanzania Conservation Limited na Kijiji Cha Sukenya.

Sisi tunaamini kwamba Maanda Ngoitiko anayo ajenda ya siri kuhusu OBC na Thomson ambao anawaita “land grabbers” yaani wapora ardhi ya Wamaasai na daima kuwaandika kwenye mitando ya jamii na kwenye tovuti mbalimbali za dunia wakati yeye mwenyewe amepora ekari nyingi za jamii bila kupewa na vilevile kuwa na wawekezaji wengine wengi ambao hawatajwi wala kuandikwa mitandaoni na wamewekeza kwenye vijiji vingine. Kwa mfano, wawekezaji wa Kijiji cha Ololosokwan, Clens Camp na End Beyond na wengine wanaomiliki maeneo makubwa yaliyokuwa ya malisho kama vile Ndorobo Safaris kule Ilmasilig.

Je, tatizo la Thomson na OBC kutetwa mno na Maanda Ngoitiko ni kwa sababu hafaidiki binafsi na miradi kutoka kwenye kampuni hizo?

Maanda Ngoitiko amekuwa mchochezi dhidi ya vijiji na OBC. Kwa mfano, amewahamasisha Wamasai kulima, kuweka maboma, kuweka soko la Karkarmoru na kujaza ng’ombe katika kitalu cha OBC ili washindwe kutimiza majukumu yao na hatimaye wakate tamaa waondoke.

Kitalu cha uwindaji cha OBC kimekuwa na ongezeko kubwa la mifugo kutoka Kenya, kata za Engusero-Sambu na Orgosorok na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, vyanzo vya maji na kusababisha kushuka kwa hadhi ya kitalu na kuwa chanzo cha wafugaji kuingiza ng’ombe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kinyume cha sheria za nchi.

Kwa uchochezi Wamaasai wameaminishwa kwamba kitalu cha uwindaji cha OBC ni eneo la jumla la malisho ya mifugo kwa Maasai wote wakati wa masika na wa kiangazi pia.

Upotoshaji na uchochezi wa Maanda Ngoitiko umesababisha Wamaasai kuamini kuwa kuingiza mifugo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuweka maboma ni haki yao ya asili kinyume cha sheria za nchi juu Hifadhi hii ya Taifa.

Sisi tunasema Maanda Ngoitiko na shirika lake la Pastoral Women Council ni hatari kwa usalama wa Taifa kwa sababu wanashirikiana na wageni kuhujumu na kuharibu sifa nzuri ya nchi yetu. Anashirikiana na baadhi ya watu waliopigwa marufuku kuingia hapa nchini, akiwamo Susanna Norduland ambaye alikuwa international volunteer wa shirika la Maanda la PWC na kuendelea kuwa msemaji wake wakati amepigwa marufuku na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa makusudi Susanna kafungua tovuti lukuki kwa ajili tu ya kuvuruga amani ya Loliondo akishirikiana na Maanda Ngoitiko.

Sisi tunasema kwamba tuzo aliyopewa Maanda Ngoitiko si ya kweli na ya haki kwa sababu amepata kwa kudanganya dunia kwa kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu wawekezaji, Serikali na wadau wengine wanaotetea haki za jamii ya Loliondo, kama Kidupo na Kata ya Oloipiri.

Sehemu ya pili ya waraka huu tutatoa mapendekezo yetu ya nini kifanyike ili kurejesha na kuimarisha hali ya amani ya utulivu katika Tarafa ya Loliondo na Wilaya ya Ngorongoro kwa jumla.

 

>>ITAENDELEA>>

2448 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!